Mbeya. Zaidi ya kaya 300 zilizokumbwa na mafuriko wilayani Mbarali, mkoani Mbeya zimerejeshewa matumaini baada ya kupatiwa msaada wa mahitaji mbalimbali zikiwepo blanketi na magodoro.
Imeelezwa kuwa mafuriko hayo yalitokea Februari 17, mwaka huu kufuatia mvua kubwa kunyesha na kusababisha baadhi ya nyumba kubomoka na kuripotiwa kifo cha mtu mmoja.
Pia, mafuriko hayo yalileta athari za uharibifu wa miundombinu kwenye mashamba, makazi kubomoka sambamba na mifugo kufa baada ya kusombwa na maji.
Kufuatia athari hiyo Shirika la msalaba mwekundu limeguswa na kutoa misaada mbalimbali ili kupunguza makali ya maisha kufuatia madhara yaliyojitokeza.
Akipokea misaada hiyo jana Aprili 19, 2026 Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Brigadia Jenerali Maulid Surumbu alisema ni hatua muhimu katika kurejesha matumaini kwa waathirika wa mafuriko.
Mbunge wa Mbarali, mkoani Mbeya, Bahati Ndingo (kushoto), akipeana mikono na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli (kulia). Katikati ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Brigedia Maulid Surumbu.
“Tusiishie hapa tunaomba wadau wengine kuguswa kusaidia waathirika wa mafuriko ili kurejesha matumaini kwa kutambua bado wana mahitaji,” amesema.
Brigadia Surumbu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha wanakuwa salama na kupata mahitaji mbalimbali muhimu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli alisema wataendelea kuchukua hatua mbalimbali za muda mfupi na mrefu kwa waathirika wa mafuriko.
“Tutaendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa kaya zilizokumbwa na mafuriko kuhakikisha wanarejea katika hali ya kawaida sambamba na kuwa na mipango ya muda mfupi na mrefu katika kukabiliana na athari za mafuriko katika vipindi vya mvua,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Msalaba mwekundu, Samuel Katambala alisema hatua hiyo ni kutokana na ushirikiano wao na Serikali na kusisitiza wataendelea kushirikiana pindi majanga hayo yakijitokeza.
Naye Mbunge wa Mbarali, Bahati Ndingo alilishukuru shirika hilo kugusa wananchi waliokumbwa na athari ya mafuriko huku akisisitiza kuendelea kuomba wadau mbalimbali kuwasaidia.