Utitiri masharti ya mikopo kwa vijana watikisa Bunge

Dar es Salaam. Uamuzi wa Serikali kuzigawanya fedha za uwekezaji wa vijana katika wizara mbalimbali za kisekta umepingwa na wabunge, wakisema umesababisha milolongo na kuendelea kuwaacha vijana wakilalamika.

Mbali na milolongo na urasimu, wabunge hao wamesema kumekuwa na masharti mengi ya upatikanaji wa fedha hizo kwa vijana, jambo linalowafanya baadhi yao wasikidhi vigezo na hivyo wasinufaike.

Fedha zinazozungumziwa na wabunge hao ni zile Sh200 bilioni zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana na kugawanywa katika wizara za madini, kilimo, mifugo, vijana na maendeleo ya jamii.

Michango ya wabunge hao imeibuka baada ya hotuba ya mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2026/27 ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana.

Katika hotuba hiyo, Waziri Joel Nanauka ameomba Bunge limuidhinishie Sh35.9 bilioni. Kati ya hizo, Sh30.1 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh5.85 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wizara hiyo.

Hayo yaliibuka bungeni jijini Dodoma leo, Aprili 20,2026, wabunge hao walipochangia hotuba hiyo ya Nanauka. Katika hotuba hiyo, wizara imeomba fedha kutekeleza mipango ya vipaumbele vinne.

Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Ndanda (CCM), Faraji Nandala, amesema bado kuna malalamiko mengi kwa vijana, hasa urasimu unaotokana na fedha hizo kupelekwa wizara nyingine za kisekta.

“Vijana wanalalamika, hizi fedha kwanza hawana taarifa na hawajui mchakato mzima wa kuzipata. Idadi ya vijana walioomba hadi sasa ni 30,383, na ukiangalia walengwa ni vijana milioni 21. Sasa idadi ya walioomba haifiki hata asilimia moja ya walengwa,” amesema.

Pia, amesema kama Serikali inataka kuwasaidia vijana, ipitie upya masharti na kuyapunguza, ikiwemo kuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na leseni.

“Hizi fedha zingegawanywa kwa majimbo kisha kata, ambapo zingeshuka hadi ngazi ya kijiji ili vijana wapate, na siyo kuwa wizarani kama ilivyo sasa,” amesema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka akizungumza bungeni leo, Jumatatu Aprili 20, 2026, wakati akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/27, bungeni jijini Dodoma.

Mbunge wa Kalambo (CCM), Edefonce Canoni, amesema ni vema fedha zirudishwe katika Wizara ya Vijana ili kuwe na urahisi wa usimamizi, lakini pia kuwafanya vijana watambue zinakopatikana.

“Wakienda benki wanakutana na masharti mengi, hii inasababisha fedha hizi kukwama benki. Sasa zikibaki huko ni kwa manufaa ya nani?

“Sheria na usimamizi ubadilishwe, na masharti yawe nafuu. Kama ni dhamana, wabunge tupo, madiwani wapo na wenyeviti wapo. Masharti yapunguzwe vijana wapate fedha hizo,” amesema.

Amesema si lazima kuundwa vikundi kwa kuwa wengine wanaweza kuingia hawana sifa.

Mbunge wa Viti Maalumu, Latifa Juwakali, amesema kitendo cha fedha kupelekwa katika wizara za kisekta kinaleta maswali, nani msimamizi wake.

“Kwenye wizara hizo aulizwe nani? Tunatakiwa kuanzisha mfumo maalumu wa kuwasaidia, ikiwemo kupata elimu. Siyo vijana wote wanaweza kuandika maandiko, bado kuna haja ya kuwasaidia kwa sababu nafasi na muda upo,” amesema.

Mbunge wa Kasulu Vijijini, Edibily Kinyoma, ameshauri mifuko na fedha zote zinazohusu maendeleo ya vijana ziwe katika Wizara ya Vijana, kwa kuwa italeta urahisi hata kwa waziri kusema fedha zimefanyiwa nini pale atakapoulizwa.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zainab Abdallah Issa, amesema ipo haja ya kuwa na benki ya maendeleo ya vijana kwa sababu asilimia 76 ya nguvu kazi ya nchi ni vijana.

“Vijana wanatakiwa kupata fursa ya mitaji kupitia benki hiyo. Kama tumeweza kuwa na benki ya maendeleo ya kilimo, kwa nini tushindwe ya vijana?” amehoji.

Mbunge wa Ilemela, William Kafiti, ameomba Serikali iendelee kutoa fedha katika vyuo vya maendeleo ya vijana vilivyopo Morogoro na Songwe ili waendelee kunufaika hasa katika maeneo ya ujasiriamali na kilimo.

“Serikali ije na mpango wa kuwandaa vijana. Mfano, leo vijana wanaomaliza kidato cha nne, sita na chuo wanaofeli wanakwenda wapi? Nini mpango wa Serikali kuwainua vijana hawa?” amesema.

Akiwasilisha hotuba yake, Nanauka amekiri kuwepo kwa changamoto ya ongezeko la mahitaji ya mikopo ya vijana lisilolingana na fedha zilizopo, hali inayosababisha wengi kushindwa kufikiwa.

Amesema vijana wengi wanakabiliwa na upungufu wa ujuzi unaohitajika katika soko la ajira, pamoja na uelewa mdogo wa masuala ya msingi ya maisha kama afya ya uzazi, uzalendo na athari za dawa za kulevya.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, wizara imepanga kushirikisha wadau wa maendeleo kuongeza rasilimali, pamoja na kuimarisha utoaji wa mikopo nafuu, mafunzo ya ujasiriamali na uanzishwaji wa vituo vya ubunifu.

Nanauka amesema wizara imeweka vipaumbele vinne, vikiwemo uwezeshaji wa kiuchumi kwa vijana, kuimarisha ushiriki wao katika maamuzi, kukuza elimu ya uraia na kuboresha ustawi wa vijana kupitia stadi za maisha na msaada wa kisaikolojia.

Aidha, amesema Serikali imeanza kupitia upya Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa ili kuongeza ushiriki wa vijana katika kupanga na kuamua masuala ya maendeleo yao.

Kwa mujibu wa Nanauka, maoni kutoka kwa wadau, hususan vijana, yanaendelea kukusanywa ili kuhakikisha sheria hiyo inakidhi mahitaji halisi ya kundi hilo.

Hata hivyo, pamoja na mipango hiyo, wabunge wamesisitiza kuwa bila kurahisisha mifumo ya upatikanaji wa fedha na kupunguza urasimu, juhudi za uwezeshaji wa vijana zinaweza kuendelea kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.