LHRC: Haki ya kuishi imekiukwa zaidi 2025

Dar es Salaam. Wakati mijadala ya kijamii na sera nyingi ikiendelea kulenga kuwalinda wanawake dhidi ya ukatili wa kijinsia na ubaguzi, ripoti mpya ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) imeibua taswira tofauti, ikionesha kuwa mwaka 2025 watoto na wanaume ndio walioathirika zaidi na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini.

Akiwasilisha ripoti hiyo leo, Jumatatu, Aprili 20, 2026, jijini Dar es Salaam, mtafiti kutoka LHRC, Fundikila Wazambi, amesema takwimu zinaonesha watoto walikumbwa zaidi na vitendo vya ukatili wa kingono na kimwili, huku wanaume wakiongoza kwa kuathirika na matukio ya vurugu za kisiasa, ukamatwaji holela na ukiukwaji wa haki jinai.

Amesema kwa mwaka huo, haki ya kuishi ndiyo iliyokiukwa zaidi, hali iliyochangiwa na mauaji yasiyo halali, ikifuatiwa na ukiukwaji wa haki ya usawa mbele ya sheria, uhuru dhidi ya ukatili na haki ya kuabudu.

Hata hivyo, Mwananchi lilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, kuzungumzia ripoti hiyo, lakini amesema hawezi kutoa maoni kwa sasa kwa kuwa bado hajaiona na kuisoma.

“Nitatoa maoni baada ya kuisoma kwa kina ili kuepuka kutoa kauli nje ya muktadha,” amesema Kamanda Misime.

Mwananchi pia ilimtafuta Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ambaye amesema atatoa ufafanuzi baada ya kuisoma ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matukio ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 yalikuwa kichocheo kikubwa cha kuongezeka kwa ukiukwaji wa haki za binadamu, hasa kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi kutoka Jeshi la Polisi, ambayo yalisababisha vifo vya raia.

“Taarifa na vielelezo vilivyopatikana vinaonesha kulikuwa na matumizi makubwa ya nguvu pamoja na mauaji yasiyo ya kisheria, hali iliyoathiri moja kwa moja haki ya kuishi,” amesema Wazambi.

Ameongeza kuwa mazingira ya vurugu yalichangiwa na mambo kadhaa, ikiwemo kubanwa kwa haki za kiraia, matukio ya utekaji na kupotea kwa watu, pamoja na ukamataji na kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria.

“Ukikosea kwenye hatua ya ukamataji ni rahisi pia kukosea kwenye hatua ya kuzuia. Haya ni mambo yanayohitaji marekebisho ya mifumo,” amesisitiza.

Hata hivyo, ili kubaini ukweli wa matukio yaliyoripotiwa na kuchukua hatua stahiki, Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume huru ya uchunguzi kuchambua sakata hilo.

Kwa mujibu wa taarifa za Serikali, tume hiyo ipo katika hatua za mwisho kukamilisha majukumu yake, huku ripoti yake ikitarajiwa kuwasilishwa Aprili 24, 2026. Matokeo ya uchunguzi huo yanatarajiwa kutoa mwanga kuhusu chanzo cha matukio hayo na kupendekeza hatua za kisheria na kiutawala.

Ripoti ya LHRC inaeleza kuwa uchaguzi huo uliacha alama mbaya katika historia ya haki za binadamu nchini, ukiashiria dosari katika misingi ya haki na uhuru wa kisiasa.

Imebainisha kuwa hali ilikuwa tofauti Zanzibar, ambako matukio kama hayo hayakuripotiwa kwa kiwango kikubwa, jambo linaloelezwa kuchangiwa na tofauti za kisheria na kiutawala kati ya pande mbili za Muungano.

Katika mapendekezo yake, LHRC imesisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa uwajibikaji kwa taasisi zote za dola kuanzia ngazi za chini hadi juu, sambamba na kufanya marekebisho ya sheria ili kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu.

Akifafanua matumizi ya ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Anna Henga, amesema mbali na kuelimisha jamii, nyaraka hiyo hutumika kama ushahidi katika kesi mbalimbali za ukiukwaji wa haki za binadamu mahakamani.

Kwa mtazamo wa muda mrefu, LHRC imeelekeza umuhimu wa kupatikana kwa Katiba mpya, ikisisitiza kuwa baadhi ya changamoto za ukiukwaji wa haki zinatokana na mifumo ya kisheria iliyopo ambayo haiwezi kurekebishwa kikamilifu bila mabadiliko ya kikatiba.

“Katiba mpya inaweza kuwa suluhisho la changamoto nyingi, kwani baadhi ya matatizo yanajengwa na mfumo mzima wa sheria uliopo,” amesema Dk Henga.

Ameongeza kuwa kusikiliza na kutatua malalamiko ya wananchi kwa wakati ni hatua muhimu ya kuzuia migogoro na kuimarisha mshikamano wa kijamii.

“Tunapaswa kushughulikia chanzo cha matatizo badala ya kushughulikia dalili zake. Hapo ndipo tutakapopata suluhisho la kudumu,” amesisitiza.