Askari wawili JWTZ watakiwa kukabidhi pasi, wawekewa vikwazo vya kusafiri 

Moshi. Mahakama imewaamuru Askari wawili wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) wanaokabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi, kukabidhi polisi pasi zao za kusafiria na kutosafiri nje ya Mkoa Kilimanjaro bila kibali cha Mahakama.

“Waombaji watasalimisha hati zao za kusafiria kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa, kama zipo. Hawatatoka nje ya Mkoa wa Kilimanjaro hadi uamuzi wa mwisho wa kesi yao utakapotolewa,” inaeleza amri hiyo ya Mahakama.

Amri hiyo inawahusu pia raia watatu ambao pamoja na askari wanakabiliwa na tuhuma za kupatikana na meno ya tembo 16 na vipande 15 vyenye thamani ya Sh591.3 milioni, kinyume cha Sheria ya Uhifadhi wanyamapori.

Hayo yamo katika uamuzi wa masharti ya dhamana yaliyotolewa Aprili 14, 2026 na Jaji Adrian Kilimi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Moshi kutokana na maombi ya dhamana yaliyowasilishwa kortini na watuhumiwa hao.

Maombi hayo ya jinai namba 2953 ya 2025, yalifunguliwa katika mahakama hiyo na washtakiwa hao watano, dhidi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP).

Askari hao ni Sajini  Andrew Ndaga mwenye namba MT. 76601 na Sajini Taji (staff Sergeant),Uchumu Rajabu mwenye namba MT. 76764 na raia watatu, ambao ni Mzee Ally Mzee, Juma Chaupe na Ally Ayubu, maarufu Hakimu.

Kesi hiyo ya jinai namba 27119 ya mwaka 2025 ipo mbele ya Hakimu mkuu mkazi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Moshi, Ally Mkama lakini washtakiwa walilazimika kuomba dhamana Mahakama Kuu yenye mamlaka hayo.

Katika shitaka la kwanza linalowakabili Sajenti Ndaga na Stesheni Rajabu na raia Mzee Ally Mzee, inadaiwa Oktoba 21, 2025 eneo la Sango Wilaya ya Moshi, walipatikana na meno ya tembo 16 na vipande 15 vya meno hayo.

Meno hayo ambayo ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni sawa na tembo 12 waliouawa wenye thamani ya Dola 240,000 za Marekani sawa na Sh591.3 milioni za Tanzania, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Katika kosa la pili, linalowakabili Sajenti Ndaga na raia wawili ambao ni Juma Cheupe na Ally Ayubu, maarufu Hakimu, wanakabiliwa na makosa ya kujihusisha na kufanya biashara ya nyara za Serikali kinyume cha sheria.

Maelezo ya kosa hilo yanadai kuwa katika tarehe tofauti kati ya miezi ya Julai na Oktoba 2025, katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walijihusisha na biashara ya nyara za Serikali kinyume cha sheria.

Ilidaiwa na upande wa mashitaka kuwa, katika tarehe hizo na maeneo hayo, waliuza, kununua, kuhamisha, kusafirisha na kupokea meno ya tembo 16 na vipande 15 vya meno ya tembo, sawa na tembo 12 waliouawa.

Meno hayo ambayo ni mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yalikuwa na thamani ya Dola 240,000 sawa na Sh591.3 milioni za Tanzania.

Maombi ya dhamana yalivyokuwa

Kupitia kwa wakili wao, Denis Maro, washtakiwa hao walifungua maombi ya jinai namba 2953 ya 2025 wakiomba kupatiwa dhamana na Mahakama Kuu ya Tanzania, ambayo kisheria ndio yenye mamlaka ya kutoa dhamana hiyo.

Wakili Maro aliwasilisha hoja kuwa chini ya kifungu cha 29 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa, mahakama hiyo ndio ina mamlaka ya kutoa dhamana ambapo thamani ya mali inayohusika inazidi Sh300 milioni.

Aliongeza kusema kuwa chini ya kifungu 151(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sura ya 200, Urekebu wa mwaka 2023, imeipa mamlaka mahakama hiyo kutoa dhamana ilimradi tu sheria inaruhusu dhamana hiyo.

Kuhusu masharti yanayopaswa kuzingatiwa na mahakama, wakili Maro alisema kifungu 36(4)(e) inatoa mazingira ambayo dhamana inaweza kukataliwa lakini kifungu kidogo cha (5) kimetoa mwongozo wa masharti ya dhamana.

Wakili aliongeza kuwa, waombaji hawakukiuka masharti yoyote ya kisheria, hivyo wanastahili kupata dhamana hadi kesi yao itakapoamuliwa na DPP  (Mkurugenzi wa Mashtaka nchini) hajapinga maombi yao na pia dhamana ni haki ya msingi ya mtuhumiwa.

Akijibu hoja za maombi hayo, wakili mwandamizi wa Serikali, Grace Kabu aliunga mkono ombi lililopo kwa kuwasilisha kwamba, DPP hakuwasilisha hati ya kiapo kwa kuwa alikusudia kutopinga maombi hayo ya dhamana ya washtakiwa.

Hata hivyo, wakili huyo alisisitiza kuwa iwapo mahakama hiyo itakubali kutoa dhamana kwa waombaji (washtakiwa), izingatie masharti yaliyoainishwa chini ya kifungu cha 36(5(a) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa.

Kwa mujibu wa wakili Kabu, sheria inataka pale ambapo thamani ya mali inayohusika katika kosa hilo inazidi Sh10 milioni, mwombaji wa dhamana lazima aweke nusu ya thamani ya mali au kutoa mali isiyohamishika yenye thamani sawa.

Wakili huyo wa Serikali alisema kuwa kwa kuwa hati ya mashtaka inaeleza kuwa thamani ya nyara hizo za Serikali ni Sh591 milioni, hivyo nusu yake ni Sh295.6 milioni na ndicho kinapaswa kuwekwa mahakamani au mali isiyohamishika.

Uamuzi wa jaji ulivyokuwa

Katika uamuzi wake huo ambao umewekwa katika tovuti ya TanzLII ambayo ni ya Serikali ya Tanzania inayochapisha maamuzi, sheria na kanuni bure mtandaoni, Jaji Kilimi, alisema suala la kuliamua mbele yake ni kama maombi hayo yana sifa.

Jaji alisema thamani ya nyara za Serikali ambazo waombaji wanadaiwa kukutwa nazo ni Sh591.3 milioni na kama alivyoeleza wakili wa Serikali Grace Kabu, masharti ya dhamana yameainishwa katika kifungu cha 36(5)(a) cha sheria.

“Kwa kuegemea kifungu hicho, nimezingatia kosa waliloshtakiwa nalo na nimeridhika kosa ambalo waombaji wanashtakiwa nalo ni kosa linaloweza kudhaminiwa kwa masharti yaliyoainishwa na sheria hapo juu.”

“Zaidi ya hayo, kwa kuwa shtaka hilo linahusisha waombaji watano, wanapaswa kugawana mzigo huo chini ya kanuni ya kugawana iliyoelezwa na mahakama ya rufaa katika shauri la Silvester Dawi na Stephen Mwambene dhidi ya Jamhuri.”

Jaji aliongeza kusema kuwa kwa kuwa kiwango cha thamani ya fedha katika kosa linalowakabili kinazidi Sh10 milioni kulingana na hati ya mashitaka, basi waombaji wataachiwa kwa dhamana kwa masharti matano endapo watayatimiza.

Kwa kuwa nusu ya kiwango cha thamani ya mali ni Sh295,686,000 milioni, kila muombaji atatakiwa kuweka mahakamani fedha taslimu Sh59,137,200 milioni au aweke hati ya mali isiyohamishika ambayo thamani yake si chini ya kiasi hicho cha fedha.

“Mali zisizohamishika ziungwe mkono na Ripoti ya Uthamini kutoka kwa Mthamini wa Serikali au hati zinazohalalisha mali iliyoidhinishwa kutoka kwa mamlaka inayofaa inayoonyesha kiasi sawa au zaidi cha pesa kilichotajwa hapo juu,”alisema.

Mbali na sharti hilo, lakini kila mwombaji lazima awe na wadhamini wawili wa kuaminiwa ambao kila mmoja atatakiwa kusaini bondi ya Sh59.1 milioni ambayo ni nusu iliyobaki ya kiasi hicho na wawe na vitambulisho na barua ya utambulisho.

Katika sharti la tatu, Jaji alisema waombaji watasalimisha hati zao za kusafiria kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa, kama zipo na Hawatatoka nje ya Mkoa wa Kilimanjaro hadi uamuzi wa mwisho wa kesi yao utakapotolewa.

“Pale itakapokuwa muhimu kusafiri, wataomba kwa maandishi kwa Naibu Msajili wa Mahakama hii, ambaye anaweza kutoa kibali kinachofaa,”alisisitiza Jaji.

Jaji alitaja sharti lingine kuwa ni waombaji watatakiwa kuhakikisha wanahudhuria katika tarehe za kesi zitakazopangwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na wadhamini wao ni lazima waidhinishwe na Naibu Msajili.

“Waombaji wataendelea kuzuiliwa hadi masharti yanayohusu amana ya fedha au hati miliki ya mali isiyohamishika yaliyotajwa yatakapotmizwa,”alisisitiza Jaji Kilimi.

Kulingana na kalenda ya usikilizwaji wa mashauri ya jinai na madai (cause list) iliyopo katika mfumo wa E-Service Portal wa mahakama, kesi ya msingi imepangwa kuanza kusikilizwa Aprili 28, 2026 mbele ya Hakimu Mkama.