Wananchi wanufaika elimu ya akiba Tabora

Tabora. Zaidi ya kaya 4,500 katika Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora zimenufaika na mradi wa Dreams Tanzania, uliotoa elimu ya ujasiriamali, matumizi sahihi ya fursa, pamoja na mbinu za kuweka akiba kwa malengo ya muda mfupi, mrefu na ya dharura.

Mradi huo unatekelezwa katika vijiji mbalimbali wilayani humo, ikiwemo Ulyankulu, Mishamo, Makingi na Katumba, ukiwa na lengo la kuimarisha uchumi wa kaya na mtu mmoja mmoja.

Jumla ya vikundi 20 vimehitimu mafunzo hayo yaliyolenga kuzikwamua kaya na umasikini ili waweze kumudu gharama za maisha.

Baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya namna ya kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza Aprili 15, 2026, katika mahafali ya kuhitimu mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Makazi Ulyankulu, Samwel Makungu, amewahimiza wahitimu kutumia kwa vitendo elimu waliyoipata ili iweze kuleta tija iliyokusudiwa.

“Elimu hii iwasaidie kweli na muendelee kuifanyia kazi kwa vitendo kama ambavyo mnafanya sasa, msije mkaacha, tunataka tupate matajiri katika maeneo haya na inawezekana kabisa,” amesema.

Amesema vijijini fursa zipo nyingi ikiwemo ufugaji, kilimo biashara za mazao na mahitaji muhimu ambavyo vinaweza kuwapa kipato wakati wote na wakaweza kukidhi mahitaji muhimu ya familia zao.

“Mmefundishwa kutumia fursa zilizopo kwenye maeneo yenu ili kujiingizia kipato cha familia zenu na sasa mko vizuri maana watoto wenu wanakwenda shule na nyinyi mnapendeza sana kwa sasa,” amesema.

Kaimu mkuu wa Makazi Ulyankulu Samwel Makungu akizungumza katika mahafali ya wahitimu wa mafunzo kutoka mradi wa Dreams Tanzania.

Aidha, meneja msaidizi wa mradi wa Dreams Martine Mgala amesema mradi wa Dreams ulianza mwaka 2024 na ni mradi utakaodumu kwa miaka minne ambapo mpaka sasa tayari kaya 5,000 zimeshafikiwa na mradi huo.

“Kwa kadiri mradi unavyoendelea tunategemea kufikia kaya nyingi zaidi kwa sababu pia wananchi wanaelewa na wameifurahia fursa hii ya mafunzo na wengine maisha yameanza kubadilika,” amesema.

Amesema changamoto kubwa iliyokuwepo ni wananchi hao kushindwa kujua na kuzitumia fursa zinazowazunguka kwenye jamii yao, lakini sasa wameamka na wamechangamkia fursa na zinawasaidia kukidhi mahitaji yao.

“Wanatoa na ushahidi kwamba sasa wanapata mahitaji ya familia na wanashirikiana kati ya baba na mama kuhakikisha wanainua kaya zao kiuchumi,” ameongeza.

Kaimu mkuu wa Makazi Ulyankulu Samwel Makungu akikabidhi cheti kwa mmoja wa wahitimu wa mradi wa Dreams Tanzania.

Kwa upande wake Shukuru Kabugire ambaye ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo, amesema mafunzo waliyopewa na mradi wa Dreams yamewasaidia sana kwani wamebadilisha maisha yao na ameweza kupata mahitaji muhimu ya familia yake.

Ana Gervas mkazi wa Kanindo Ulyankulu Wilaya ya Kaliua mnufaika wa mafunzo hayo, ameshukuru mradi wa Dreams kwa kuwapa elimu hiyo kwani imekua mkombozi wao kutoka kwenye umasikini ambao wamedumu nao kwa muda mrefu.

“Tulihisi umasikini ndio maisha yetu, lakini Dreams Tanzania imekuja kutufungua mawazo na macho yamepata kuona na sasa tunatumia fursa na maisha yetu ni mazuri,” amesema.