Global Publishers
April 19, 2026
0 Comments
Klabu ya Simba imeendeleza mbio zake za kuwania ubingwa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye dimba la Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha alama 42 baada ya mechi 19 na kusalia nafasi ya pili, ikiwa nyuma kwa alama tano dhidi ya vinara Young Africans SC. Kwa upande wa Namungo, wameendelea kubaki nafasi ya 10 wakiwa na alama 22.
Simba ilianza mchezo kwa kasi na kufungua ukurasa wa mabao mapema dakika ya 12 kupitia kwa Libasse Gueye, kabla ya kiungo mshambuliaji Anicet Oura kuongeza bao la pili dakika ya 25 na kuwapa wageni udhibiti wa mchezo.
Namungo walijaribu kurejea mchezoni na kufanikiwa kupata bao dakika ya 33 kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Chrispine Makambo, na kufanya kipindi cha kwanza kumalizika kwa Simba kuongoza 2-1.
Kipindi cha pili kilishuhudia Simba wakidhibiti mchezo zaidi, kabla ya Ellie Mpanzu kufunga bao la tatu dakika ya 74 na kuhitimisha matumaini ya Namungo kusawazisha.
Matokeo hayo yanaipa Simba nguvu mpya katika mbio za ubingwa, huku wakizidi kuwakaribia wapinzani wao wakuu, Yanga, wakati ligi ikiendelea kupamba moto.
