UONGOZI wa Gunners FC ya Dodoma umemwachia Henry Mkanwa kibarua cha kuiongoza timu hiyo hadi mwisho wa msimu huu, baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Mathias Wandiba kujiunga na Fountain Gate inayoshiriki Ligi Kuu Bara, akiwa ni msaidizi wa Kocha, Fredy Felix ‘Minziro’.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkanwa aliyezifundisha Biashara United na Pamba Jiji, amesema ataendelea kukumbuka mchango wa Wandiba kutokana na ushirikiano waliokuwa nao tangu wamejiunga na timu hiyo wakichukua nafasi ya Kocha Juma Ikaba aliyeondoka kwa makubaliano ya pande zote mbili.
“Ni fursa nyingine kwake ya kuonyesha uwezo wake, ni kocha niliyefanya naye kazi vizuri kwa kipindi kifupi nilichokuwa naye, namtakia kila la heri na sasa ni muda kwangu wa kuendeleza yale yote mazuri aliyoyaacha,” amesema Mkanwa.
Ikaba aliyezifundisha Gwasa, Usalama na Baobab Queens, aliiongoza Gunners tangu ikiwa Ligi ya Mkoa (RCL) hadi Ligi ya Championship, ingawa aliachana nayo tangu Januari 2026, kisha timu hiyo kukabidhiwa Wandiba ambaye pia ameondoka.
Gunners imepanda Ligi ya Championship msimu huu, baada ya kuongoza First League kundi B na pointi 35, baada ya kushinda mechi 11, sare mbili na kupoteza moja, ikiungana na Hausung ya Njombe, iliyoongoza kundi A na pointi 25.
Baada ya timu hizo kuongoza makundi yao na kupanda Championship, zilicheza mechi ya fainali kusaka bingwa mpya wa First League kwa msimu wa 2024-2025 nackikosi hicho cha Gunners kilitwaa ubingwa huo kwa kuifunga Hausung mabao 3-0.
Timu hiyo inayopambana leo na Mbuni FC ya Arusha kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, katika mechi 21 ilizocheza msimu huu imeshinda sita, sare tano na kupoteza 10, ikiwa nafasi ya 10 na pointi 23 na imefunga mabao 18 na kuruhusu 29.
