Waarabu wamfuata Bacca Yanga, masharti matatu yatajwa

UBORA wa beki wa kati, Ibrahim Abdallah Hamad ‘Bacca’ anaoendelea kuuonyesha Yanga, umetajwa ndiyo sababu ya Waarabu kutoka Morocco, Raja Club Athletic kuhitaji kumsajili, lakini ili kufanikisha dili hilo, kuna masharti matatu yametajwa lazima yafuatwe.

Mwanaspoti limepata taarifa kutoka Morocco zikidai, aliyekuwa kocha wa Simba, Fadlu Davids ambaye hivi sasa anaifundisha Raja Athletic, amependekeza jina la Bacca kusajiliwa katika klabu hiyo msimu ujao na viongozi wanaangalia namna ya kufanya kwa kufuata utaratibu ili kuona uwezekano wa kumsajili.

Chanzo kutoka Morocco kilisema: “Kocha Fadlu ndiye aliyehitaji huduma ya Bacca, anatambua uwezo wa mchezaji huyo kwani amefundisha Simba inayocheza Ligi ya Tanzania Bara na amemuona, ili kufanikisha hilo lazima utaratibu uzingatiwe, lakini anahitajika kwa kiwango kikubwa kuja kucheza hapa Morocco.”

Wakati Waarabu hao wakianza harakati hizo za kupambania saini ya Bacca, Mwanaspoti limepata taarifa, beki huyo ambaye ni askari wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) mwenye cheo cha sajenti, inapotokea anahitajika na klabu nyingine nje au ndani ya Tanzania, basi lazima waajiri wake wajulishwe kila kitu ili aweze kuruhusiwa.

Bacca ambaye alitua Yanga Januari 14, 2022 akitokea KMKM, mkataba wake ndani ya kikosi hicho unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, hivyo klabu inayomhitaji lazima ifuate utaratibu wa kumnunua.

Mwanaspoti lilimtafuta Kapteni (N) Hussein Ali Makame ambaye ni Mkuu wa teknolojia na michezo KMKM kuelezea utaratibu wa vitu gani vinapaswa kuzingatiwa kwa timu inapohitaji mchezaji ambaye ni askari kutoka kikosi chao.

Kiongozi huyo alitaja masharti matatu yanayopaswa kufuatwa na kwanza ni KMKM lazima ijulishwe juu ya dili hilo ili kutoa ruhusa kutokana na Bacca bado ni askari.

Pili, katika mauzo ya mchezaji huyo, kiasi cha fedha kitakacholipwa, lazima pia KMKM ipate kwani ndio utaratibu waliouweka, huku jambo la tatu ni kumruhusu mchezaji kipindi cha mapumziko arudi nyumbani na atatakiwa kutembelea ofisini ili asisahau kazi yake, ikiwemo kuhudhuria mafunzo.

“Kama kweli ishu hiyo ipo ya hao Waarabu kumhitaji Bacca, basi uongozi wa Yanga utatujulisha, ila hadi sasa hatuna taarifa yoyote kuhusiana na Bacca kutakiwa na Raja.

“Askari yeyote kutoka KMKM iwe mchezaji ama kazi nyingine, mfano baharia akipata dili la kampuni za nje anaruhusiwa kwenda lakini ile kampuni itatambua sisi ndiyo waajiri wake na lazima tutapata pesa kiasi kutoka kwao, tunaamini kwa kufanya hivyo tunawaongezea ujuzi na uzoefu mwingine,” amesema Capteni Makame.

Kigogo huyo amesema kuna mabaharia ambao wanafanya kazi Dubai ambao wametoka KMKM, mwingine ni mwanariadha ambaye yupo kambi ya Arusha anakwenda nje na kurejea mkoani humo, lakini bado ni askari.

“Mfano tuliamini kumruhusu Bacca kwenda Yanga kutapandisha kiwango chake na kweli imekuwa hivyo hadi anaitwa timu ya taifa ya Tanzania, ikitokea amepata timu ya nje ambayo ina manufaa ataruhusiwa,” amesema.

Amesema masharti ambayo wanapewa wachezaji inapotokea wakawa mapumziko, wanapaswa watembelee ofisini ili wasisahau kazi yao, ikiwemo kuhudhuria mafunzo.

“Mfano kuna mafunzo ya kiofisa sitataja yatakuwa lini, jina la Bacca limetoka, tutaujulisha uongozi wa Yanga pia tutaangalia ratiba ya mchezaji, ili angalau ahudhurie ufunguzi hata kwa wiki moja, ili ikitokea nafasi ya kupandishwa cheo iwe rahisi kwake,” amesema kapteni huyo na kuongeza.

“Jambo lingine la msingi tunawasisitiza askari ambao wanafanya kazi nje ya ofisi za KMKM ni nidhamu ya juu na kuwa mfano wa kuigwa popote wanapokuwepo.”