Kikwete bega kwa bega na sekondari ya Kibaha

Kibaha. Katika hatua inayotarajiwa kuleta nafuu ya msongamano wa wanafunzi, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ameahidi kuungana na wadau mbalimbali kufanikisha ujenzi wa jengo la ghorofa katika Shule ya Sekondari Kibaha.

Akizungumza leo Aprili 15, 2026 wakati wa uzinduzi wa harambee ya ujenzi huo ulioenda sambamba na mahafali ya 59 ya kidato cha sita, Kikwete amesema yuko tayari kushirikiana na uongozi wa shule pamoja na wadau wengine kuhakikisha mradi huo muhimu unatekelezwa kwa mafanikio.

“Nipo tayari kuungana na uongozi wa shule hii kuhakikisha mipango yote inakamilika hususan ujenzi wa jengo hili la ghorofa. Tayari nimeanza mchakato wa kuunda kamati ya kusaidia hatua hii,” amesema Kikwete.

Mbali na ahadi hiyo, ameutaka uongozi wa shule hiyo kulinda na kutunza miundombinu iliyopo ili iendelee kuwanufaisha wanafunzi wa sasa na vizazi vijavyo. Pia amesisitiza umuhimu wa michezo kama sehemu ya malezi na maendeleo ya wanafunzi.

Kwa upande wake, mkuu wa shule hiyo, George Kazi amesema taasisi hiyo inakabiliwa na upungufu wa madarasa 10 pamoja na maabara moja, hali inayosababisha msongamano mkubwa wa wanafunzi darasani.

Amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo, shule imeanzisha mradi wa ujenzi wa jengo la ghorofa lenye thamani ya Sh3.8 bilioni.

“Tumeanza jitihada za ujenzi wa jengo hili kutokana na changamoto ya madarasa na maabara. Tunamwomba Rais mstaafu atuunge mkono ili kufanikisha mradi huu,” amesema Kazi.

Amebainisha kuwa katika hatua za awali, shule ilifanya harambee iliyowashirikisha wazazi na wadau mbalimbali na kufanikiwa kukusanya Sh26 milioni, fedha ambazo tayari zimetumika kuweka msingi wa jengo hilo.

Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk Jakaya Kikwete akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa shule ya Sekondari Kibaha Mkoa wa Pwani George Kazi leo April 15, 2026 juu ya ujenzi wa jengo la ghorofa Moja kabla ya kuanza kwa uzinduzi wa harambee ya ujenzi wa ghorofa hiyo shuleni hapo ulioambatana na sherehe za mahafari ya59 ya  kidato cha sita ya Shule hiyo. Picha na Sanjito Msafiri

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, Robert Shilingi amesema wanaendelea kuweka mikakati ya kuboresha miundombinu ya shule hiyo, ikiwemo kuanzisha madarasa ya kisasa yanayotumia teknolojia ya kidijitali ili kuongeza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji.

Mmoja wa wazazi wa wanafunzi wanaosoma shule hiyo,  Rehema Simon ameupongeza uongozi wa shule kwa ubunifu wa kuanzisha miradi ya maendeleo, akisema hatua hiyo itasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Shule ya Sekondari Kibaha ni miongoni mwa taasisi zenye historia ndefu katika sekta ya elimu nchini, ikiwa imechangia kwa kiasi kikubwa kutoa wahitimu waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali.

Hata hivyo, ongezeko la wanafunzi na mahitaji ya elimu ya kisasa limeongeza shinikizo la miundombinu, hali iliyochochea kuanzishwa kwa miradi ya maboresho ikiwemo ujenzi wa majengo mapya.