Dar es Salaam. Benki ya NMB imeahidi kutoa Sh500 milioni katika kipindi cha miaka miwili kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), kusaidia upanuzi wa huduma za upandikizaji figo na uboho, hatua inayolenga kuimarisha huduma za afya za kibingwa nchini.
Ahadi hiyo imetangazwa kwenye hafla ya uchangishaji fedha iliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo Sh250 milioni zimekabidhiwa kama sehemu ya utekelezaji wa msaada huo wa miaka miwili.
Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika hivi karibuni, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema uwekezaji katika huduma maalumu za matibabu ni muhimu kwa kuwa unasaidia kupunguza gharama kubwa za kuwapeleka Watanzania nje ya nchi kutafuta tiba hizo.
Akizungumza kwa niaba ya NMB, Mkurugenzi wa Uhusiano kwa Wawekezaji, Uendelevu na Mawasiliano, Innocent Yonazi, amesema mchango huo unaonesha dhamira ya benki hiyo ya kuendelea kuunga mkono vipaumbele vya maendeleo ya Taifa, hususan katika sekta ya afya.
Amesema NMB imeendelea kuelekeza sehemu ya faida yake kwenye shughuli za uwajibikaji kwa jamii, huku afya ikiwa miongoni mwa maeneo ya kipaumbele.
Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Abeid Makubi amesema msaada huo utasaidia kuongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma hizo muhimu kwa Watanzania wengi zaidi, hasa wasioweza kumudu gharama za matibabu ya kibingwa.
Hatua hiyo pia inatajwa kuwa chachu ya kupunguza utegemezi wa rufaa za matibabu nje ya nchi, huku ikiimarisha uwezo wa ndani wa Tanzania katika huduma za kibingwa zenye kugusa maisha ya wananchi wengi.

