Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Bukoba, imemuachia huru Deus Fredrick maarufu kama Dogoboy, aliyekuwa ameshtakiwa kwa mauaji ya mkewe, Olivia Osward baada ya kumtuhumu kushirikiana na mke mwenzake kumuibia Sh20,000.
Deus aliyekuwa na wake wawili Olivia (marehemu kwa sasa) na Milia Jenifa, aliwashuku kumuibia fedha hizo, kisha aliwafungia na kuwatesa kwa siku tatu, kitendo kilichosababisha kifo cha mmoja wao kutokana na majeraha aliyopata.
Hukumu hiyo iliyomwachia huru, imetolewa Aprili 17, 2026 na Jaji Lilian Itemba, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya jinai na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Jaji Itemba amesema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama imebaini kuwepo kwa shaka kubwa lililodhoofisha kesi ya upande wa mashtaka.
Dogoboy alishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, ilidaiwa Aprili mosi 2024, katika Kijiji cha Kigorogoro wilayani Kyerwa, alimuua mkewe Olivia.
Ili kuthibitisha kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi saba huku mshtakiwa huyo akiwa shahidi pekee wa utetezi.
Shahidi wa sita, Milia (mwathirika wa tukio hilo) alidai kuwa, mumewe ambaye ni mfanyabiashara aliwashuku kuwa wamemuibia Sh20,000 na kuwafungia katika moja ya vyumba na kuwatesa na baada ya siku tatu, usiku wa manane, Olovia alikuwa katika hali mbaya na kuomba apelekwe hospitalini.
Alidai kuwa, Deus alikodi pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na shahidi wa tatu, Granus Kanisius na kumpeleka duka la dawa; walishauriwa kutokana na hali yake wampeleke Kituo cha Afya Murongo.
Shahidi wa pili, Dk Dickson Emmanuel aliyechunguza mwili wa marehemu alidai ulikuwa na majeraha mengi, kuvunjika kwa mguu na kuthibitisha kuwa chanzo cha kifo kilikuwa ni kukosa hewa kutokana na kunyongwa.
Shahidi wa kwanza ambaye alimpokea Olivia, kituoni hapo alidai wakati akimfanyia uchunguzi alibaini kuwa amefariki na kwa kuwa, mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha aliripoti tukio hilo polisi.
Shahidi wa nne ambaye ni mdogo wa shahidi wa sita, Anitha Mnyanenza alidai Machi 31,2024 alienda kumtembelea dada yake na kukutana na mshtakiwa ambaye alimwambia dada yake hayupo, kisha akampa chakula akalala.
Alidai usiku alisikia sauti ya dada yake akizungumza chumbani na asubuhi iliyofuata alimweleza kuwa amefungiwa huko chumbani,, alilazimika kwenda kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kitongoji, cha Omugengabo, Philbert Binamungu ambaye alivunja mlango na kumtoa Milia.
Shahidi wa saba, Sajenti Asifiwe alimkamata mshtakiwa hospitalini, alidai Deus alimwambia Olivia alivamiwa na majambazi lakini hakuna wizi uliofanyika nyumbani kwao.
Alidai kuwa, mshtakiwa atakuwa alimnyonga mkewe wakiwa njiani kuelekea hospitalini na kuwa, umbali wa kutoka nyumbani ilikuwa kama kilomita 35 na kuwa dereva wa bodaboda atakuwa alidanganya kuwa Olivia alifikishwa hospitalini hapo akiwa hai.
Katika utetezi wake mshtakiwa huyo alieleza Mahakama kuwa, yeye ni mfanyabiashara wa mazao ya kahawa pamoja na biashara zingine na kudai alikuwa akiishi na mkewe Olivia pamoja na wafanyakazi wake wa saluni na katika mashamba hayo.
Aidha alidai Milia alikuwa mmoja wa wapangaji wake aliyekuwa akiishi na mumewe.
Deus alikana kumuua mkewe, akisisitiza hakuwa na migogoro na kwamba madai hayo yalikuwa ya uongo.
Alidai siku ya tukio kulitokea ugomvi baina ya mkewe na Milia na kuwa kutokana na ugomvi huo alimkuta Olivia akilia na Milia alikuwa amekimbia eneo hilo na , ndiye aliyemshambulia mkewe.
Deus aliiambia Mahakama kuwa, chanzo cha mgogoro huo ni godoro alilokuwa amehamisha Milia wakati hakuwa amelipa kodi, na kuwa kutokana na majeraha aliyomkuta nayo mkewe, alimpeleka duka la dawa, zahanati na hatimaye Kituo cha Afya cha Murongo ili apate matibabu.
Zaidi ya hayo, mshtakiwa alidai kuwa kifo cha mkewe kilitokana na uzembe wa kimatibabu, akieleza kuwa kulikuwa na ucheleweshaji mkubwa wa huduma hospitalini na kutokuwepo kwa daktari kwa muda mrefu.
Aliongeza kuwa, marehemu alitapika mara kwa mara na hata kuanguka kutoka kitandani kabla ya kufariki dunia.
Jaji Itemba amesema masuala ya kuamuliwa na Mahakama ni iwapo mshtakiwa ndiye aliyesababisha kifo cha Olivia, kama alifanya hivyo kwa kukusudia kuuua.
Amesema haipingiki kuwa kifo cha Olivia hakikuwa cha kawaida na katika uchambuzi wake, alibaini kuwepo kwa upungufu mkubwa katika ushahidi wa upande wa mashtaka.
Ameeleza kuwa, kulikuwa na nadharia mbili zinazokinzana kuhusu chanzo cha kifo, moja ikidai kuwa marehemu alikufa kutokana na kipigo na nyingine ikisema alinyongwa.
Mahakama ilieleza kuwa, ushahidi huo hauwezi kuwa sahihi kwa wakati mmoja na hivyo kuibua shaka kubwa.
Aidha, Mahakama ilikosoa upande wa mashtaka kwa kushindwa kuwaita mashahidi muhimu, hususan wahudumu wengine afya waliompokea Olivia.
Jaji ameeleza kuwa, ushahidi wao ungeweza kusaidia kubaini hali halisi ya marehemu alipofika hospitalini, jambo ambalo lingeweza kuondoa utata uliopo.
Katika uamuzi wake, Jaji Itemba amesisitiza kanuni ya msingi katika sheria za jinai kuwa, pale ambako kuna shaka katika ushahidi wa upande wa mashtaka, mashaka hayo yanapaswa kuwa faida kwa mshtakiwa.
“Nimezingatia utetezi wa mshtakiwa na ni maoni kwamba upande wa mashtaka umeshindwa kubaini chanzo cha kifo bila shaka yoyote,ushahidi wa kitabibu kuhusu kunyongwa haujakamilika na kuna mashaka kadhaa yaliyotolewa na mashtakiwa kuhusu chanzo cha kifo kuwa uzembe,mashaka ambayo hayakupingwa au kufafanuliwa na mashtaka,” amesema.
Amenukuu maamuzi ya kesi mbalimbali za awali zilizosisitiza umuhimu wa ushahidi thabiti na usio na utata katika kuthibitisha kosa la jinai.
“Katika mazingira haya, Mahakama inaridhika kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi bila shaka yoyote,” alisema Jaji.
Kutokana na hitimisho hilo, Mahakama ilimkuta mshtakiwa hana hatia ya kosa la mauaji chini ya kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, na kuamuru aachiliwe huru mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa mashtaka mengine halali.
