Tarime. Wananchi wilayani Tarime Mkoa wa Mara wameiomba Serikali kutoa fedha za dharura ili kukarabati Barabara ya Tarime- Nyamwaga ambayo hivi sasa imeharibika kufuatia mvua zinazoendelea na kusabababisha ajali, majeruhi na vifo kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Ombi hilo wamelitoa jana Aprili 19, 2026 kwa Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega aliyefanya ziara kukagua barabara na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi juu ya ubovu wa barabara hiyo.
Akizungumza baada ya kukagua barabara hiyo, Waziri Ulega amesema Serikali imeziweka kwenye kipaumbele barabara za kimkakati za Mkoa wa Mara ambazo ujenzi wake ulisimama na zile ambazo zimeharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
“Barabara za Mkoa wa Mara ziko kwenye kipaumbele cha Serikali na zitapewa fedha hivi karibuni kwa ajili ya kuendelea na ujenzi pamoja na ukarabati kwa zile ambazo zimeathiriwa na mvua, hivyo niwaombe wana Mara muwe na imani lazima mkandarasi atarudi hapa ili kuendelea na kazi,” amesema.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akizungumza kwenye mkutano na wananchi wa Isenye mkoani Mara baada ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara ya Tarime–Mugumu (km 87.14) na Sanzate–Natta (km 40). Kushoto ni Waziri wa Ulinzi, Dk Rhimo Nyansaho.
Ulega amesema Serikali imedhamiria kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuboresha na kuimarisha barabara kwa maelezo kuwa, zina mchango mkubwa katika mapinduzi ya kiuchumi na kijamii.
Awali, wakiwasilisha malalamiko yao kwa Waziri Ulega, wakazi hao wamesema kwa sasa barabara hiyo inapitika kwa tabu, mbali na kusababisha ajali na vifo, pia hali hiyo imekuwa ni chanzo cha kuharibika kwa vyombo vya usafiri na kusababisha hasara kwa wamiliki wa vyombo hivyo.
Mwita Santuri amesema kwa sasa barabara hiyo imegeuka kuwa kero kubwa kwa watumiaji kutokana na ubovu wake, hali ambayo pia imesababisha wakazi hao kutumia gharama kubwa na muda mrefu kwa safari ambazo ni za umbali mfupi.
“Kwa kawaida kutoka Tarime hadi Nyamwaga kama barabara ingekuwa nzuri tungekuwa tunatumia dakika 15 lakini kutokana na hali ilivyo tunatumia zaidi ya saa moja na nauli wakati mwingine ni zaidi ya Sh5,000 hii ni hasara kubwa sana kwetu tunaomba Serikali iingilie kati tunaumia,” amesema Mwita.
John Wambura ambaye ni dereva bajaji amesema kutokana na ubovu huo, bajaji nyingi zimesitisha safari katika barabara hiyo, hivyo kusababisha uchumi wao kuathirika kutokana na kushindwa kufanya kazi kwa mujibu wa leseni zao za usafirishaji.
“Bora ingebaki kama ilivyokuwa mwanzo kuliko sasa, imekwanguliwa na kuachwa bila matengenezo hali ambayo imezidi kuiharibu zaidi, tunaomba barabara hii ifanyiwe kazi kwa dharura, kwani hali ni mbaya kwetu sisi ambao tunategemea biashara ya usafirishaji ili tuweze kuendesha maisha yetu,” amesema.
Ghati John amesema kina mama wengi wamekuwa wakipata wakati mgumu hasa wakiwa njiani kwenda kujifungua, hali ambayo imesababisha baadhi yao kujifungulia njiani baada ya kushindwa kufika kwa wakati hospitalini kwaajili ya kujifungua.
Waziri wa Ulinzi, Dk Rhimo Nyansaho akizungumza kwenye mkutano na wananchi wa Isenye mkoani Mara baada ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega kukagua kwenye ujenzi wa barabara ya Tarime–Mugumu (km 87.14) na Sanzate–Natta (km 40).
“Hii ndio barabara tunayotumia kwenda katika hospitali yetu ya Nyamwaga na kutokana na ubovu huu, baadhi wajawazito wanalazimika kujifungulia njiani na kuhatarisha maisha yao na watoto wao pia Serikali ichukulie suala hili kwa umuhimu wake,” amesema Ghati.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema Barabara ya Tarime -Nyamwaga ni miongoni mwa barabara muhimu wilayani Tarime huku ikitegemewa katika usafirishaji wa mazao na shughuli zingine za kiuchumi na kijamii.
Amesema ubovu wa barabara hiyo kwa namna moja ama nyingine ni kikwazo kwa ukuaji wa uchumi wa wakazi wa wilaya hiyo na mkoa wa Mara kwa jumla.