Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza fedha zilizokuwa zimepangwa kugharamia sherehe ya maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka huu zitumike kukarabati miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea nchini.
Agizo hilo la Rais Samia limetolewa katika kipindi ambacho mvua zinaendelea maeneo mbalimbali nchini na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu hiyo, ikiwemo madaraja.
Wabunge wakati wakijadili bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2026/27 ya Sh12 trilioni, walipaza sauti wakiitaka Serikali kuchukulia tatizo hilo kama jambo la dharura, kwani wananchi wanateseka na uharibifu huo.
Leo, Jumatatu, Aprili 20, 2026, akiwa ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, Dk Mwigulu ametoa taarifa ya maelekezo hayo ya Rais Samia kuhusu fedha hizo kupelekwa kugharamia ukarabati wa barabara.
“Maadhimisho ya sherehe za miaka 62 ya Muungano yatafanyika katika ngazi ya mikoa yote nchini, ambapo viongozi wakuu wa kitaifa watafanya shughuli za kutembelea, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo,” amesema Dk Mwigulu.
Aidha, Dk Mwigulu amesema imeelekezwa wakuu wa mikoa watembelee, waweke mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo pamoja na kushiriki shughuli za usafi wa mazingira, kupanda miti na kufanya mashindano ya michezo mbalimbali.
“Ninamshukuru mheshimiwa Rais Dk Samia kwa kuelekeza fedha ambazo zingetumika kwa kufanya maadhimisho haya kwa gwaride na michezo ya halaiki, zitumike katika shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo ukarabati wa miundombinu ya barabara zilizoharibiwa na mvua zinazoendelea nchini,” ameongeza Dk Mwigulu.
Pia, Dk Mwigulu ameagiza majengo yote ya Serikali kunakshiwa kwa rangi za bendera ya Taifa kuanzia Aprili 20, 2026 hadi Aprili 26, 2026, siku ya kilele.
“Majengo yote ya Serikali Tanzania Bara yapambwe kwa vitambaa vya rangi ya bendera ya Taifa, picha za waasisi wa Muungano na picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Dk Mwigulu.
Ameongeza kuwa kwa upande wa Zanzibar, majengo yapambwe kwa vitambaa vya rangi sahihi za bendera ya Taifa, picha za waasisi wa Muungano na picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na picha ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi.
“Nitumie fursa hii kuwahamasisha wananchi wote kushiriki ipasavyo kwenye shughuli za kijamii, midahalo na makongamano katika kila mkoa ili kujadili maendeleo endelevu yaliyofikiwa na nchi yetu katika kipindi cha miaka 62 ya Muungano.
“Aidha, ni muhimu wananchi wote waendelee kuulinda Muungano wetu ili kudumisha umoja, amani na mshikamano wetu,” amehimiza Waziri Mkuu.
Shughuli nyingine zitakazoambatana na maadhimisho hayo ni pamoja na mashindano ya michezo na sanaa mbalimbali; mashindano ya uandishi wa insha kwa shule za msingi na sekondari, mahojiano maalumu na wazee maarufu, midahalo na makongamano kuhusu Muungano na hatua ya maendeleo iliyofikiwa hadi sasa.
Maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano yanaenda na kauli mbiu ya: “Amani, umoja na mshikamano ni msingi wa maendeleo endelevu.”
