Walichokisema viongozi wa Chadema baada ya kifungo

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeitisha kikao maalumu cha Kamati Kuu ya chama hicho kujadili na kutafakari mapito waliyopitia kwa siku 309 bila kufanya shughuli za kisiasa, pamoja na kuweka uelekeo mpya.

Hatua hiyo imekuja kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Rufani kuondoa zuio lililokuwa limewekwa na Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, lililokizuia chama hicho kufanya shughuli za kisiasa.

Uamuzi huo umetolewa leo, Jumatano Aprili 15, 2026, na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, likiwemo Jaji Augustine Mwarija, Jaji Issa Maige na Jaji Abraham Mwampashi, waliokiruhusu chama hicho kuendelea na shughuli zake za kisiasa bila kikwazo.

Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walivyowasili makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam leo Jumatano Aprili 15, 2026. Picha na Michael Matemanga

Shauri hilo lilitokana na mapitio ya mahakama yaliyoibuliwa kufuatia kesi ya msingi iliyohusu madai ya mgawanyo usio sawa wa rasilimali za chama kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama Kuu, Dar es Salaam, na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, pamoja na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Dar es Salaam, Aprili 15, 2026, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, amesema kikao hicho kinatarajiwa kufanyika Aprili 28 na 29, 2026, kwa ajili ya kutafakari mapito hayo na kutoa mwelekeo wa baadaye.

Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa chama hakiongozwi na Katibu Mkuu peke yake, bali kina viongozi wengi, akiwemo Mwenyekiti wa chama, Tundu Lissu, ambaye kwa sasa yupo gerezani, pamoja na Makamu Mwenyekiti (Bara), John Heche na wengine.

“Viongozi hao wanaiongoza Kamati Kuu, ambayo ni chombo kinachosimamia sekretarieti ya chama, inayofanya kazi kwa niaba ya Baraza Kuu, ambalo linasimama kwa niaba ya wanachama wa nchi nzima.

“Kulingana na ukubwa wa mapito tuliyopitia kwa kuzuiwa kufanya shughuli za kisiasa kwa siku 310, na majukumu yaliyoko mbele yetu, natangaza kuitishwa kwa kikao maalumu cha Kamati Kuu kuanzia Aprili 28 hadi 29, 2026,” amesema.

Mnyika amesema wajumbe wa Kamati Kuu kutoka maeneo mbalimbali nchini wanapaswa kufika makao makuu ya chama hicho kwa ajili ya kikao hicho maalumu, ambapo watatafakari kwa pamoja.

“Tutatathmini uendeshaji wa chama, na yapo mambo yatakayozungumzwa kwa umoja wetu baada ya kikao hicho,” amesema.

Pia amesema kufuatia uamuzi huo wa mahakama, ofisi za makao makuu ya chama zimefunguliwa rasmi, na shughuli za kuingia na kutoka zitaendelea kama kawaida.

Amesema zuio lililokuwepo limeondolewa, hivyo ofisi na mali za chama zinapaswa kutumika na kuendelea kutekeleza katiba ya chama baada ya kusimama kwa muda.

“Naomba wanachama wetu na Watanzania kwa ujumla waendelee kuichangia Chadema kupitia njia rasmi ili tuweze kutekeleza majukumu yetu,” amesema Mnyika.

Viongozi wa Chadema wakiwa katika Makao Makuu ya chama hicho leo Jumatano Aprili 15, 2026, jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti (Bara), John Heche, amesema siku ya leo ni ya furaha kwa chama hicho baada ya kurejea rasmi katika shughuli za kisiasa.

“Hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jiwe lingine. Tunawashukuru wanachama kwa uvumilivu wao; waliotuzuia walidhani tutasambaratika, lakini wamekiimarisha zaidi chama,” amesema.

Amesema chama hicho hakiwezi kufutika kwa kuwa kinabeba ajenda za maisha ya wananchi, ikiwemo ajira kwa vijana na makazi bora.

“Kujaribu kuua ndoto ya Watanzania ya maisha bora haiwezekani. Kwa siku 310 nchi ilikuwa kimya huku kukiwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kupanda kwa gharama za maisha,” amedai.

Ameongeza kudai kuwa katika kipindi hicho hakukuwa na sauti madhubuti ya kisiasa, na hata vyama vingine havikujitokeza kuzungumza kwa kiwango kinachotarajiwa.

“Sasa tumerudi, kazi ipo na tutaifanya kwa vitendo. Tunawashukuru wanachama wetu kwa uvumilivu wao, na pia tunaishukuru mahakama kwa uamuzi wake,” amesema.

Amesema mapambano yao yanaendelea, huku msimamo wao ukiwa ni Mwenyekiti wao, Tundu Lissu, aachiwe huru ili washiriki kikamilifu katika siasa za kuikomboa nchi.

Wanachama wa Chadema wakifanya usafi katika Makao Makuu ya chama hicho leo Jumatano Aprili 15, 2026, jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Awali, Mwanasheria wa chama hicho, Dk Rugemeleza Nshala, alisema taarifa ya kuondolewa kwa zuio ilitolewa baada ya kupigiwa simu na karani wa mahakama.

“Nilipigiwa simu na karani aliyejitambulisha kwa jina la Tina akitaka kunisomea uamuzi wa mahakama. Nilishangaa, kisha nikawataarifu wenzangu, na tukathibitisha kuwa amri ya zuio ilikuwa batili,” amesema.

Amesema kutokana na uamuzi huo, chama hicho kipo huru kufanya shughuli zake za kisiasa bila usumbufu wowote.

Pia, amesema kesi inayokihusu chama hicho sasa itasikilizwa na jaji mwingine wa Mahakama Kuu baada ya kuondolewa kwa jaji aliyekuwa akiishughulikia awali.

“Kesi hii inarudishwa kwa jaji mwingine wa Mahakama Kuu ili aamue hoja ya msingi iwapo iliwasilishwa ndani ya muda au nje ya muda wa kisheria. Upande wa wenzetu wanadai iliwasilishwa kwa wakati, lakini sisi tunasisitiza kuwa ilikuwa nje ya muda,” amesema.

Ameongeza kuwa kesi hiyo haitakuwa tena chini ya Jaji Hamidu Mwanga, huku akibainisha kuwa viongozi wa chama pamoja na timu ya wanasheria watachukua hatua stahiki kulingana na yaliyojitokeza katika mwenendo wa shauri hilo.