Serikali: Tuitumie AFCON 2027 kukuza utalii

Arusha. Serikali imewataka wadau wa sekta ya utalii kuanza maandalizi ya mapema ili kunufaika na fursa ya michuano ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 pamoja na matukio mengine ya kimataifa yatakayofanyika nchini.

Matukio hayo ni pamoja na mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu na hafla ya utoaji tuzo za World Travel Awards Grand Final itakayofanyika Desemba 2026.

Akizungumza leo Jumamosi Aprili 18, 2026 jijini Arusha wakati wa mafunzo kwa waongoza watalii, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji amesema matukio hayo ni fursa muhimu ya kukuza sekta ya utalii nchini.

Amesema ni muhimu kwa wadau kubuni vifurushi maalum vya utalii vitakavyoendana na ratiba za wageni watakaohudhuria matukio hayo ili kuwavutia kutembelea vivutio mbalimbali vya nchini.

“Ni vyema kutangaza mapema kupitia majukwaa mbalimbali ili wageni wapate taarifa kwa wakati na waweze kupanga safari zao kwa urahisi,” amesema Kijaji.

Amesema waongoza watalii ni wadau muhimu katika kukuza sekta hiyo, wakichangia ongezeko la idadi ya watalii na mapato ya nchi.

Kuhusu mafunzo hayo, Kijaji amesema ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha wahudumu wa sekta hiyo wanakuwa na ujuzi unaokidhi ushindani wa soko la kimataifa.

“Tanzania inajulikana kama The World’s Best Safari Destination, hivyo huduma zetu zinapaswa kuendana na hadhi hiyo,” amesema.

Ameongeza kuwa waongoza watalii wanapaswa kuzingatia usalama wao na wa wageni ili kuhakikisha utalii endelevu.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, jumla ya waongoza watalii 2,000 watanufaika na mafunzo hayo kwa awamu mbalimbali, huku watoa huduma za malazi na vyakula nao wakitarajiwa kupatiwa mafunzo kama sehemu ya mpango huo.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia utalii, Nkoba Mabula amesema mafunzo hayo ya awamu ya pili yamehusisha waongoza watalii 250, baada ya awamu ya kwanza iliyofanyika Aprili 16, 2026 kuwahusisha washiriki 270.

Amesema mafunzo hayo yatafanyika kwa awamu nane, yakilenga kuwafikia jumla ya waongoza watalii 2,000, kwa ushirikiano kati ya Wizara na Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato).

“Mafunzo haya yatasaidia kufikia lengo la Serikali la kuvutia watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030,” amesema Mabula.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tato, Wilbard Chambulo amesema mwaka jana waongoza watalii 1,000 walipata mafunzo hayo na mwaka huu wanatarajia kuwafikia 2,000.

Amesema ubora wa huduma unaotolewa na waongoza watalii una mchango mkubwa katika ukuaji wa sekta hiyo.

“Mtalii anaweza kusahau hoteli au chakula, lakini hawezi kumsahau mwongoza utalii. Hiyo ndiyo nafasi na nguvu waliyonayo,” amesema Chambulo.

Amesisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama wa wageni wakati wa safari, akionya dhidi ya maamuzi hatarishi yanayoweza kuhatarisha maisha.