Mbeya. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya kimeishauri Serikali kuharakisha mchakato wa kukamilisha mradi wa barabara ya njia nne kutoka Igawa hadi Songwe yenye urefu wa kilometa 32.
Hatua hiyo imetajwa kunusuru miundombinu ya barabara za pembezoni ambazo zimeanza kuharibika kufuatia magari yenye uzito mkubwa kupita.
Ushauri huo umetolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa Mkoa wa Mbeya (MNEC), Ndele Mwaselela wakati akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi, Aprili 18, 2026.
Mwaselela amesema kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kumepelekea msongamano wa magari kwenye Barabara Kuu ya Tanzania na nchi jirani ya Zambia (TANZAM), jambo linalosababisha madereva kutumia njia za pembezoni.
“Barabara za pembezoni kwenye mitaa zimeanza kuharibika kufuatia magari yenye uzito mkubwa kupita kukwepa foleni katika barabara ya TANZAM,” amesema.
Mwaselela amesema kama chama wataendelea kulisemea, lakini wameona tayari wabunge wameanza kulizungumzia bungeni jambo ambalo litaweka msukumo kwa Serikali.
“Hivi karibuni tutakuwa na kikao na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan. Moja ya hoja ni kuwasilisha ombi hilo la kukamilika kwa barabara ya njia nne,” amesema.
Mwaselela amesema kimsingi wana kila sababu ya kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuleta miradi ya kimkakati Mkoa wa Mbeya, jambo ambalo litachochea shughuli za kiuchumi na mapato ya Serikali.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela, akizungumza na Mwananchi ofisini kwake. Picha na Hawa Mathias.
Aidha, amesisitiza kufuatia uwekezaji huo viongozi kuwa mstari wa mbele kuisemea miradi hiyo kwa wananchi.
Kuhusu miradi ya soko na kituo kikuu cha mabasi ya mikoani, amesema kwa sasa miradi hiyo ipo katika hatua nzuri sambamba na kuishukuru Serikali kwa uwekezaji huo wa ujenzi wa soko la kisasa la Matola na kituo kikubwa cha mabasi ya mikoani.
“Tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali iliyopo madarakani kwa Mkoa wa Mbeya. Tumepata miradi mikubwa ya kimkakati ambayo ikikamilika itachochea shughuli za kiuchumi na mapato,” amesema.
Aidha, ametaja miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Igawa–Songwe, soko la kisasa la Matola na kituo kikuu cha mabasi ya mikoani eneo la Old Airport.
Dereva wa masafa marefu, Daudi Mwakyusa amesema kusuasua kwa kukamilika kwa mradi huo imekuwa mwiba mkali kwao kukaa barabarani kwa muda mrefu.
“Kimsingi barabara hii imekuwa kikwazo kikubwa kwetu madereva wa masafa marefu. Ukifika kipande cha Mbeya na Tunduma ni sehemu yenye kikwazo sana kwetu,” amesema.
Naye dereva wa bajaji, Anthony Joel, ametaja sababu ya kupita maeneo ya pembezoni ni kukwepa foleni katika barabara kuu ya TANZAM.
“Unajua shida ni ufinyu wa barabara na kama unavyojua wengi wetu bajaji ni za mkataba au marejesho ya kila siku. Ukisema kusubiri foleni si jambo jema,” amesema.
Mjasiriamali wa nyanya katika soko la Sido jijini hapa, Salome Noel, amesema kusuasua kwa ujenzi wa miundombinu hiyo ni changamoto kubwa inayokwisha shughuli za kiuchumi.
Hivi karibuni, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo, alihoji katika vikao vya Bunge Dodoma kutaka kujua mradi huo muhimu utakamilika lini kutokana na umuhimu wake.
Fyandomo alieleza licha ya kuchelewa kukamilika kwa mradi huo, Serikali ilitoa shilingi bilioni 183, ambapo mpaka sasa mkandarasi amelipwa shilingi bilioni 44.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema kutokana na umuhimu wa barabara hiyo changamoto iliyopo ni kuhamisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ya maji machafu na taka.
Amesema mpaka sasa wamefikia asilimia 44.7 huku sehemu nyingine bado zinaondolewa, na kusisitiza kuwa ni lazima ziondolewe ili kuendelea na ujenzi wa barabara hiyo.
