Simba kuna mawili, Barker aifungia busta Namungo

WAKATI Simba ikijiandaa kucheza dhidi ya Namungo huko kusini mwa Tanzania, kocha wa kikosi hicho, Steve Barker amekuja na mambo mawili, kwanza amewachimba mkwara mastaa wake, pili  amefurahia urejeo wa Shomary Kapombe na Yusuph Kagoma.

Kapombe na Kagoma walikosekana katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate kutokana na kila mmoja kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

Barker amewataka mastaa wake kujikita zaidi katika mpango wanaojiandaa nao ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo huo kabla ya kwenda Zanzibar kwa ajili ya Kombe la Muungano ambalo litaanza Aprili 21 hadi 29, 2026.

“Tunaenda kucheza mchezo mgumu lakini sisi ni Simba, tunahitaji kufanya vizuri katika mchezo huo ili kuendelea na hesabu zetu, nimekuwa nikiongea na wachezaji wangu kila wakati kuhakikisha tunafanya vizuri katika kila mchezo na nina furaha kwa namna ambavyo wamekuwa wakipokea maelekezo na kuyafanyia kazi,” alisema na kuongeza;

“Kila siku tumekuwa na kazi moja tu kuboresha kiwango chetu na kila mchezo ni nafasi kwa kila mchezaji kuonyesha vile anaweza kuwa msaada kwenye timu, kila mtu ana nafasi yake na kila mmoja anatakiwa kuwa tayari muda wowote kutumika, ukitazama katika mechi uliopita tulimkosa Shomary na Kagoma, ilikuwa ni nafasi kwa wengine nao kupambania timu.”

Simba yenye pointi 39 ikishika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, inahitaji ushindi dhidi ya Namungo Jumapili hii saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa mkoani Lindi ili kupunguza tofauti ya pointi kati yao na Yanga ambayo inaongoza ligi ikiwa na pointi 47.

Kocha huyo aliongeza kwamba: “Namungo ni wapinzani wanaohitaji heshima pamoja na mwenendo walionao lakini hatutapunguza kasi yetu. Tunahitaji kutengeneza nafasi na kuona vile ambavyo tunaweza kuimaliza mechi.”

Namungo ambayo ipo nafasi ya 10 na pointi 22, itakuwa ikisaka ushindi wa kwanza baada ya michezo tisa huku ikipoteza mitano mbele ya TRA  United ikifungwa mara mbili kwenye ligi na Kombe la FA (2-0), Yanga (1-0), Tanzania Prisons (3-2), Pamba Jiji (1-0) na kutoa sare minne dhidi ya Fountain Gate (1-1), Mtibwa Sugar (1-1), Singida Black Stars (1-1) na JKT Tanzania (2-2). 

Takwimu zinaonyesha katika mechi 13 ambazo Namungo imecheza dhidi ya Simba tangu imeanza kushiriki Ligi Kuu Bara 2019-2020, haijawahi kupata ushindi zaidi ya kuambulia sare tano na kupoteza nane zikiwamo tatu za mwisho ambazo zote imepoteza kwa mabao 3-0 kila moja ambazo zote ni chini ya Kocha Juma Mgunda.

Mgunda ana kazi kubwa ya kufanya mbele ya Simba aliyowahi kuinoa, kuhakikisha Namungo inapata ushindi wa kwanza mbele ya Wekundu hao wa Msimbazi.

Hata hivyo, haitakuwa rahisi kutokana na takwimu za Simba ugenini msimu huu haijapoteza hata mechi moja kati ya kumi ilizocheza ikishinda tano sawa na sare, ikifunga mabao 12 na kuruhusu matatu tu.

Namungo nayo nyumbani sio kinyonge kwani imepoteza mechi moja pekee dhidi ya Yanga kwa bao 1-0, huku ikishinda nne sawa na sare. Imefunga mabao kumi na kuruhusu sita katika mechi tisa.

“Tunajua tuna mchezo mgumu na mzito, ni mchezo wa kutafuta alama. Tunacheza na nani, hiyo inajulikana. Kikubwa tu niseme tumefanya maandalizi mazuri ya kucheza na timu nzuri yenye ushindani, hivyo tupo tayari kushindana.

“Najua kabisa tunakwenda kucheza mechi ambayo ni ngumu na yenye ushindani, tunacheza na timu yenye wachezaji wazuri na benchi la ufundi zuri, ina kila kitu, lakini nikuhakikishie tu na sisi tupo vizuri kwa sababu tumejinadaa kucheza nayo, kwa hiyo kuelewa kilichopo mbele yetu ni faraja. Kwa hiyo maandalizi ya kwenda kucheza na timu nzuri yenye kila kitu yamekamilika,” alisema Mgunda.