KIPA wa TRA United raia wa Gabon, Jean-Noel Amonome, amesema licha ya kutoruhusu bao katika mechi tisa za Ligi Kuu Bara msimu huu kwa maana ya kufikisha (Clean Sheets tisa), ila, malengo yake ni kuhakikisha pia anaendelea kuleta ushindani.
Nyota huyo aliyejiunga rasmi na TRA United zamani Tabora United, Januari 3, 2025, akitokea, AS Arta/Solar7 ya Djibouti, alisema ushindani wa makipa uliopo kwa sasa unamuongeza morali ya kuzidi kupambana, jambo ambalo ni muhimu katika timu.
“Kama tunafunga bao moja na kuzuia vizuri bila ya kuruhusu wapinzani wetu kusawazisha ni jambo nzuri, hizi clean sheets zangu ni mchango mkubwa wa timu kiujumla na sio mimi peke yangu, hivyo, ni ushirikiano wetu uwanjani,” alisema Amonome.
Kipa huyo aliyewahi kucheza FC 105 Libreville ya kwao Gabon, AmaZulu FC, Royal Eagles na Uthongathi FC zote za Afrika ya Kusini, alisema unapocheza Ligi yenye ushindani ni lazima uonyesha thamani yako, itakayokusaidia kukuza karia yako pia.
Katika msimu wake wa kwanza tangu ajiunge na kikosi hicho Januari 3, 2025, Amonome, alimaliza na ‘Clean Sheets’ mbili za Ligi Kuu Bara, ingawa, msimu huu wa 2025-2026, tayari ana tisa, akipitwa moja tu na Djigui Diarra wa Yanga mwenye 10.
Clean Sheets hizo tisa za, Amonome, ni sawa na za kipa wa matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, Aishi Manula, huku ikikumbukwa msimu uliopita wa 2024-2025, Moussa Camara wa Simba aliye majeruhi kwa sasa alikuwa kinara akimaliza na 19.