Kelele za nje mwiba ustawi wa familia

Dar es Salaam.Familia ni kitovu cha jamii. Ndani yake ndimo maadili hupandwa, tabia hujengwa na kizazi huandaliwa. 

Hata hivyo, katika dunia ya sasa, familia imejikuta ikizingirwa na kelele nyingi za nje. 

Kelele hizi hazimaanishi sauti za masikio pekee, bali ni pamoja na ushawishi wa watu, mitazamo ya jamii, shinikizo la mitandao ya kijamii, ushauri usioombwa na matarajio yasiyo na mipaka. 

Kadri kelele hizi zinavyozidi kuingia ndani ya familia, ndivyo ustawi wa familia unavyozidi kudhoofika.

Mwandishi na mtafiti wa masuala ya familia, James Dobson, anaeleza kuwa familia huharibika taratibu pale inapopoteza uwezo wa kufanya uamuzi wake kwa uhuru. 

Anasema kuwa familia inayoruhusu sauti nyingi za nje kuamua mwelekeo wake, hujikuta ikipoteza mshikamano wa ndani. 

Anaonya: “Familia inaposhindwa kulinda mipaka yake, jamii huingia na kuanza kuiongoza.” 

Kauli hii inaonyesha hatari ya familia kuacha nafasi yake ichukuliwe na ushawishi wa nje.

Katika mazingira ya sasa, wazazi wengi wanalelewa na jamii badala ya wao kulea watoto. Mitandao ya kijamii, marafiki, majirani na hata watu wasio na mchango wa moja kwa moja katika familia wamekuwa na sauti kubwa katika uamuzi wa kifamilia. 

Mtoto anapokosea, jamii inatoa hukumu; wanandoa wanapokosana, kila mtu ana maoni. Hali hii inajenga mazingira ya hofu, lawama na mashindano badala ya upendo na maelewano.

Hekima ya dini unafundisha: “Linda sana moyo wako kuliko vyote uvilindavyo, maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.” (Mithali 4:23 )

Familia ni moyo wa jamii, na pale moyo huu unaposhambuliwa na kelele za nje, jamii nzima huathirika.

Ushawishi wa watu na mitandao unavyoyumbisha

Mwandishi na mshauri wa uhusiano wa kifamilia, Gary Chapman, anaeleza kuwa familia nyingi zinavunjika si kwa sababu ya ukosefu wa upendo, bali kwa sababu ya kelele za nje zinazopotosha mawasiliano ya ndani. 

Anaamini kuwa pale wanandoa au wazazi wanapowasikiliza watu wa nje zaidi kuliko kusikilizana wao kwa wao, migogoro huanza kukua.

 Chapman anasema: “Familia haiwezi kustawi pale inapopewa maagizo na watu wasioishi ndani yake.”

Katika enzi ya mitandao ya kijamii, kelele hizi zimeongezeka maradufu. Familia zimeanza kupimwa kwa vigezo vya picha, maneno na maisha yanayoonyeshwa mtandaoni. 

Wazazi wanajilinganisha, wanandoa wanashindana, watoto wanakua wakiwa na shinikizo la kufikia viwango visivyo halisi. Kelele hizi zinapochukua nafasi ya mawasiliano ya wazi na ya kweli ndani ya familia, migogoro huanza kujitokeza bila sababu za msingi.

Mtafiti wa masuala ya ndoa na familia, John Gottman, ambaye amefanya utafiti mwingi kuhusu ustawi wa uhusiano, anaeleza kuwa ushawishi hasi kutoka nje unaweza kuvuruga familia kwa kasi kubwa. 

“Shinikizo la nje lisilodhibitiwa lina uwezo wa kuharibu uhusiano wa karibu kuliko migogoro ya ndani,” anaeleza.

Kauli yake hii inaweka wazi kuwa familia inaweza kushinda changamoto zake za ndani, lakini ikashindwa kabisa kupambana na kelele za nje zisizo na mipaka.

Kwa tafsiri ya mawazo ya Gottman, familia zinazofanikiwa ni zile zinazojenga utamaduni wa mazungumzo ya ndani, kuheshimiana na kufanya umuzi kwa pamoja. 

Pale familia inaposhindwa kufanya hivyo, nafasi hiyo huchukuliwa na watu wa nje, ambao mara nyingi hawajali athari za muda mrefu za ushauri wao.

Katika jamii nyingi, ndugu na marafiki wamekuwa chanzo kikubwa cha kelele hizi. Wengine huingilia malezi ya watoto, wengine huingilia uhusiano wa wanandoa, na wengine hueneza maneno yanayovunja heshima ya familia.

 Ingawa mara nyingi huonekana kama msaada, ukweli ni kwamba ushawishi huu huacha majeraha ya kudumu.

Hekima ya kulinda mipaka ya familia

Mwandishi na mchungaji, Timothy Keller anaeleza kuwa familia imara hujengwa juu ya misingi ya uamuzi wa pamoja na mipaka iliyo wazi. 

 Anasema kuwa familia inayoruhusu kila mtu kuingilia uamuzi wake hupoteza mwelekeo na utulivu. Keller anasisitiza kwa maneno haya: “Familia inayosikiliza kila sauti ya nje hupoteza sauti yake ya ndani.”

Kauli hii inabeba uzito mkubwa katika wakati huu ambapo kila mtu ana maoni kuhusu kila jambo. Kulinda familia hakumaanishi kujitenga na jamii, bali ni kuchagua kwa busara ni sauti zipi ziruhusiwe kuathiri uamuzi wa ndani. Familia inahitaji marafiki, jamaa na washauri, lakini si kila mmoja anapaswa kuwa na nafasi ya kuamua hatima yake.

Kelele za nje ni mwiba unaochoma ustawi wa familia taratibu bila wengi kugundua. Mwiba huu huanza kwa maneno madogo, ushauri wa juujuu au matarajio ya jamii, lakini huisha kwa migogoro mikubwa, kuvunjika kwa uhusiano na watoto kukosa mwelekeo sahihi.

Ukweli ni kwamba familia inahitaji utulivu ili kustawi. Utulivu huu haupatikani kwa kufuata kila kauli ya nje, bali kwa kujenga mawasiliano ya wazi, heshima na uamuzi wa pamoja ndani ya familia. 

Jamii inapaswa kujifunza kuheshimu mipaka ya familia, na familia zifundishwe umuhimu wa kulinda mipaka hiyo.

Suluhisho si kupuuza jamii, bali ni kuipa familia nafasi ya kwanza. Familia yenye sauti yake ya ndani iliyo imara inaweza kusikia kelele za nje bila kuathiriwa. Lakini familia inayopoteza sauti yake, humezwa na makelele na hatimaye kupoteza msingi wake.