Dar es Salaam. Wakati awali mpango ilikuwa kuwawekea meza za muda wafanyabiashara wa Simu 2000, Ubungo jijini Dar es Salaam waliounguliwa na vibanda vyao ili kuendelea na shughuli zao, hilo limebadilishwa na sasa wamejengewa vibanda.
Jioni ya Aprili 4, 2026, wafanyabiashara hao, waliokumbwa na ajali ya moto ulioteketeza zaidi ya vibanda 500 vingine 280 vikinusurika huku baadhi yao wakipoteza mali zote zilizokuwemo ndani.
Hata hivyo Aprili 6, 2026 Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alifika sokoni hapo na kuzungumza na wafanyabiashara hao huku akiagiza kusafishwa haraka kwa eneo hilo, ili shughuli za biashara zianze kwa hatua ndogondogo wakati uchunguzi ukiendelea.
Jana jioni Jumamosi, Aprili 18, 2026, Mwananchi ilifika sokoni hapo na kukuta shughuli za ujenzi wa vibanda zikiendelea kwa kasi ambapo inaelezwa tayari vibanda 100 vimeshajengwa.
Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, aliyekuwa kaweka kambi katika eneo hilo, alisema wameamua kujenga vibanda badala ya kuweka meza kama walivyoamua awali na wafanyabiashara hao ili kurahisisha kurudi kwako.
Moja ya sababu ya kufanya hivyo alisema kwa kuwa watakaa eneo hilo kwa miezi mitatu huku wakisubiri eneo walilotengewa likamilike ni ngumu kuwaacha wachomwe na jua na kunyeshewa na mvua.
Muonekano wa vibanda vya muda vinavyojengwa katika soko la Simu 2000, Ubungo, Dar es Salaam.
“Tumeona bora tujenge vibanda vya muda, wajihifadhi hapa kwa kuendelea na shughuli zao lakini wakati huohuo wawe katika mazingira walau ambayo ni salama, kuliko ambavyo tungeweka meza ni wazi mvua ingekuja ingewanyeshea halafu tungekuwa hatujawasaidia bado,” alisema Msando.
Aidha alisema vibanda hivyo pia vitaezekwa kwa bati huku akiwaondoa hofu mamlaka zinazosimamia ujenzi wa miundombinu ya stendi ya Simu 2000, kuwa wafanyabiashara hao watakaa hapo moja kwa moja kwa kuwa eneo lao la pembeni walilotengenewa likikamilika watahamia huko.
Pia, Msando alisema kwa kuwa wafanyabiashara hao wanaanza upya ndani ya miezi mitatu hawatalipa ushuru wowote ili kuwapunguzia maumivu ya ufanyaji biashara.
Wakati kuhusu suala la kupatiwa mikopo, alisema hilo ni la mchakato na wanachoangalia kwa sasa ni wapate kwanza maeneo kwa kuwa hata wakipewa mikopo halafu hawana pa kuweka biashara zao, lakini kutambulika kila mmoja alipo ni kazi bure.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa wafanyabiashara katika kamati ya ujenzi huo, Musa Ndile alisema kuanzia leo wanaanza kupaua kazi itakayofanywa usiku na mchana.
“Tunashukuru kwa hatua ambayo tumefikia ya ujenzi, ambapo kwa msaada wa usimamizi wa Mkuu wa Wilaya hatujatoa hata shilingi yetu na leo tunaanza kupaua, mategemeo yakiwa kuanzia kesho wafanyabiashara waanze kurejea,” alisema Ndile.
Mwakilishi huyo alisema mpaka sasa tayari zaidi ya mabanda 100 yameshajengwa na baada ya siku tatu eneo hilo litakuwa limeenea lote mabanda hayo, ambapo matarajio ni kujenga vibanda 280 hadi 300.
Kwa upande wao wafanyabiashara, Hajira Shomari, alisema wanashukuru kwa hatua ambazo zimechukuliwa na serikali licha ya kuwepo kwa changamoto za kutakiwa kila siku kwenda eneo hilo.
Muonekano wa vibanda vya muda vinavyojengwa katika soko la Simu 2000, Ubungo, Dar es Salaam.
“Kila siku tunahitajika kuwepo hapa kwa kile tulichoelezwa huenda tukahitajika na uongozi wakati wowote, ambapo ujio wetu hapa lazima uingie gharama za nauli na kula, lakini kwa kuwa tuna uhitaji hatuna namna,” alisema Hajira.
Naye John Boaz, alisema wapo tayari kurejea kwa sababu ndio ajira yao licha ya kuwa wasiwasi wao biashara haiwezi kuwa kama zamani kwani watu wengi walipata taarifa kuwa kumeungua.
Kuhusu mikopo, Boaz alisema kuna mkanganyiko mpaka sasa, kwani wameshaambiwa na wakubwa kwamba kila mtu atarudi kwenye halmashauri zao kwa kuwa sio wote wanaishi Ubungo, hivyo kuwa salama zaidi katika kumfuatilia.
Katika ushauri wake Boaz alisema anaona kuna ugumu katika kupata mkopo kwa njia hiyo na kushauri mamlaka zingewaandikia wajumbe wa mitaa wanaopotoka wafanyabiashara hao kwa kuwataarifu ni waathirika wa ajali ya soko la Simu 2000 ili suala hilo washughulikiwe kwa haraka.
“Kwenda tu kwa mjumbe mwenyewe kujitambulisha na kusema kuwa ulipata ajali ya moto Simu 2000, hawawezi kukuamini lakini pia watu wengine wanaweza kutumia kama upenyo wa kufanya udanganyifu,”amesema mfanyabiashara huyo.
