Maoni kinzani ongezeko la nauli

Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) ikitangaza ongezeko la nauli litakaloanza kutumika Mei Mosi, 2026, sintofahamu imetawala miongoni mwa baadhi ya watoa huduma kuhusu viwango vipya.

Baadhi yao wanadai viwango vilivyotangazwa havijaakisi matarajio yao pia haviendani na uhalisia wa kupanda kwa bei ya mafuta na gharama nyingine za uendeshaji, huku wengine wakichagua kubaki na siri moyoni kuhusu suala hilo.

Upande wa watumiaji wa usafiri wamesema viwango vipya vimezingatia usawa kwa pande zote.

Aprili 17, 2026, Latra ilitangaza marekebisho hayo yaliyohusisha ongezeko la nauli za daladala kwa Sh100 kutoka kiwango cha sasa. Kwa upande wa mabasi ya masafa marefu ya daraja la kati (Semi-Luxury), nauli imeongezeka kutoka Sh67.84 hadi Sh74.18 kwa kilomita kwenye barabara za lami.

Hatua hiyo imekuja kufuatia mchakato wa ukusanyaji maoni ulioanza Aprili 8, 2026, ambapo Latra iliitisha kikao cha wadau wa sekta ya usafirishaji. Awali, wadau walitarajiwa kuwasilisha maoni yao hadi Aprili 21, lakini viwango vipya vimetangazwa kabla ya muda huo kukamilika.

Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali la Aprili 17, 2026 (Taarifa ya Kawaida Na. 5996), Latra imepitia na kurekebisha viwango vya nauli za usafiri wa ardhini kwa kuzingatia mabadiliko ya gharama za uendeshaji.

Hata hivyo, baadhi ya watoa huduma waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina wameeleza kutoridhishwa na ongezeko hilo, wakidai halilingani na uhalisia wa kupanda kwa bei ya mafuta na gharama nyingine za uendeshaji.

Mmoja wa viongozi wa Chama cha Wamiliki wa Daladala jijini Dar es Salaam, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema walifanya kikao juzi na Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba mjini Dodoma na kufikia makubaliano ya ongezeko hilo, licha ya kutoridhishwa nalo kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji.

Amesema kiwango cha ongezeko la Sh100 hakikidhi mahitaji yao, kwani walipendekeza angalau Sh250 kwa kila kilomita. Hata hivyo, walishauriwa kusubiri na kufuatilia mwenendo wa bei ya mafuta katika mwezi ujao kabla ya kufanya maamuzi zaidi.

“Kiwango hiki cha Sh100 ni kidogo kulinganisha na matarajio yetu. Tulihitaji Sh250 kwa kilomita, lakini tumeombwa kwanza tuangalie mwenendo wa bei ya mafuta mwezi ujao lakini ukweli vinaenda kutuumiza,” amesema.

Kiongozi huyo amesema ingawa wamekubali ongezeko hilo, bado hawajaridhika nalo kwa kuwa halikuzingatia kikokotoo rasmi cha nauli. Alibainisha kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa kuzingatia maelekezo ya juu, si kwa ridhaa yao kamili.

“Ni kweli mafuta yamepanda na gharama za uendeshaji zimeongezeka. Hata hivyo, katika kikao kile tulikubaliana na kuombwa tusiendelee kulizungumzia kwa sasa, ingawa ukweli ni kwamba gharama bado ziko juu,” amesema.

Ameongeza hali ya sintofahamu ni kubwa miongoni mwa wadau, huku baadhi ya mikoa ikionyesha kutoridhishwa zaidi ikilinganishwa na Dar es Salaam, ambako viongozi walichukua msimamo wa utulivu.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, wameamua kukubaliana na hali hiyo kwa sasa wakisubiri kuona mwenendo wa bei ya mafuta mwezi ujao, huku wakiacha wazi uwezekano wa kurejea mezani kujadili upya iwapo gharama zitaendelea kuongezeka.

“Kama kiongozi, nimekubaliana na hali iliyopo kwa sasa. Tunasubiri kuona bei ya mafuta itakuwaje mwezi ujao; kama itaendelea kupanda, tutalazimika kurejea tena kwenye majadiliano,” amesema.

Kiongozi mwingine wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) amesema kiwango kilichotangazwa ni kidogo, lakini wamechagua kukaa kimya kwa sasa bila kubishana na Serikali.

“Ukweli ni kwamba kiwango kilichopandishwa ni kidogo ikilinganishwa na tulichoomba. Lakini hatuwezi kubishana na Serikali; wakati ukifika tutazungumza,” amesema.

Wakati hayo yakielezwa, Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (Latra CCC), Daud Daudi, amesema viwango vipya vimezingatia usawa kwa pande zote.

“Tangazo la Serikali kuhusu nauli za mabasi ya mjini limeongeza zaidi ya Sh100, jambo linaloonekana kuwa la haki kwa mtumiaji. Mtoa huduma aliomba nyongeza ya asilimia 130, lakini ameidhinishiwa asilimia saba; hivyo, masilahi ya mtumiaji yamezingatiwa,” amesema.

Amesema Serikali imezingatia maslahi ya watumiaji, na kwa mujibu wa tangazo hilo, viwango vipya vitaanza kutumika baada ya siku 14 iwapo hakutakuwa na changamoto yoyote.

“Kwa maeneo ya mikoani, nauli zimeongezwa hadi asilimia 19 kwenye barabara za lami,” amesema.

Daudi ameongeza viwango hivyo vina mantiki hata kiuchumi: “Mafuta yamepanda kwa asilimia 33, lakini nauli imeongezeka kwa asilimia tisa, jambo linaloonekana kuwa sahihi.”

Amebainisha kuwa watoa huduma waliomba nauli ifikie Sh250, jambo ambalo lingesababisha ongezeko kubwa zaidi ya nauli ya sasa.

Daudi ametoa rai kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri kuzingatia mwongozo huo wa Serikali, na kuwataka wale wachache waliopandisha nauli kiholela kurejea katika viwango halali.

Mkazi wa Tabata Kisiwani, Dar es Salaam, Gerald Saimoni amesema kulingana na uhalisia ulivyo wafanyakazi ilitakiwa kuongezewa mshahara ili kuleta ahueni katika kupunguza gharama za uendeshaji maisha ya kila siku.

“Nauli imepanda, mafuta yamepanda vyakula vimepanda lakini mshahara wangu kama mfanyakazi umebaki vilevile hii ina maana tunaenda kuumizana mtaani kutakuwa kugumu,”amesema. 

Kwa baadhi ya safari, viwango vipya vya nauli ni kama ifuatavyo: safari ya Dar es Salaam hadi Kigoma kupitia Kahama (kilomita 1,513) imeongezeka kutoka Sh103,000 hadi Sh112,234. Safari ya Dar es Salaam hadi Musoma kupitia Mwanza (kilomita 1,360) imeongezeka kutoka Sh92,000 hadi Sh100,884.

Safari ya Dar es Salaam hadi Bukoba kupitia Chato (kilomita 1,437) imepanda kutoka Sh97,000 hadi Sh106,596, huku ile ya Dar es Salaam hadi Songea kupitia Njombe (kilomita 950) ikiongezeka kutoka Sh64,000 hadi Sh70,471.

Safari ya Dar es Salaam hadi Mbeya kupitia Morogoro (kilomita 823) imepanda kutoka Sh56,000 hadi Sh61,050, wakati ile ya Dar es Salaam hadi Arusha kupitia Bagamoyo (kilomita 625) imeongezeka kutoka Sh42,000 hadi Sh46,362.

Vilevile, safari ya Dar es Salaam hadi Dodoma kupitia Morogoro (kilomita 424) imepanda kutoka Sh29,000 hadi Sh31,452, na ile ya Dar es Salaam hadi Mtwara kupitia Lindi (kilomita 573) imeongezeka kutoka Sh39,000 hadi Sh42,505.

Safari ya Dar es Salaam hadi Mwanza kupitia Dodoma (kilomita 1,144) imepanda kutoka Sh78,000 hadi Sh84,861.9, huku ile ya Dar es Salaam hadi Sumbawanga kupitia Mbeya (kilomita 1,130) ikiongezeka kutoka Sh77,000 hadi Sh83,823.4.