Uhaba wa fedha za maandalizi miradi ya ubia tishio

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiazimia kukuza uchumi wake kutoka Dola 90 bilioni za Marekani (Sh234,000 trilioni) za sasa hadi kufikia Dola 1 trilioni miaka mitano ijayo, wataalamu wa uchumi wameonya kwamba, uhaba wa fedha za maandalizi ya miradi ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) unaweza kukwamisha azma hiyo.

Wataalamu hao wamesema kutengwa kwa bajeti finyu katika hatua za awali za miradi ya PPP, kunaweza kudhoofisha uwezo wa nchi kuandaa miradi yenye tija na mvuto wa kibiashara, inayoweza kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka sekta binafsi.

Hatua ya maandalizi inayolalamikiwa inahusisha upembuzi yakinifu, uandaaji wa mifumo ya kifedha, miundo ya kisheria, tathmini ya mazingira na uchambuzi wa ugawanaji wa vihatarishi. Hatua hizi ndizo huamua kama wazo la mradi linaweza kugeuka kuwa fursa halisi ya uwekezaji.

Hoja hiyo imeibuka kufuatia bajeti ya Sh144.85 bilioni iliyowasilishwa na kuidhinishwa bungeni wiki iliyopita na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo.

Katika bajeti hiyo, Sh126.83 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh18.83 bilioni kwa miradi ya maendeleo.

Licha ya ukubwa wa matamanio ya nchi, takwimu zinaonesha kuwa maandalizi ya miradi ya PPP imekuwa ikitengewa wastani wa Sh1 bilioni tu kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Chini ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa (FYDP IV) wa mwaka 2026 mpaka 2031, gharama za utekelezaji zinakadiriwa kuwa Sh477 trilioni.

Kati ya hizo, asilimia 70 inatarajiwa kutoka sekta binafsi, huku miradi ya PPP pekee ikitarajiwa kuchochea zaidi ya Sh170 trilioni.

Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wajibu, Ludovick Utouh ameliambia Mwananchi leo Jumapili Aprili 19, 2026 kuwa ni lazima Bunge lijengewe uwezo wa kuelewa umuhimu wa miradi ya PPP.

“Kanuni iliyofanyiwa majaribio inasema lazima utumie fedha ili upate fedha. Kama tunataka PPP iwe chanzo cha uhakika cha fedha za maendeleo, ni lazima tuwekeze ipasavyo katika kuandaa miradi hiyo,” amesema Utouh.

Ameongeza kuwa, mtazamo na imani dhidi ya sekta binafsi lazima vibadilike ili kuifanya sekta hiyo kuwa mshirika wa dhati wa maendeleo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na mtaalamu wa PPP, Abihud Bongole akizungumzia hilo, amesema viwango vya kimataifa vinashauri kutenga angalau asilimia mbili ya gharama ya mradi kwa ajili ya kazi za maandalizi.

“Bila fedha za kutosha za maandalizi, miradi haiwezi kufikia kiwango cha kukopesheka au kuvutia wawekezaji,” amesisitiza Bongole.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuku cha Dar es Salaam (UDSM), David Rwehikiza ameonya kuwa upungufu wa fedha unadhoofisha mapendekezo ya miradi ya PPP, yawe yale yanayoibuliwa na Serikali au yale yanayoletwa na wawekezaji binafsi.

Licha ya hofu hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha PPP, David Kafulila amesema maboresho makubwa yanaendelea kufanyika ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji.

Amebainisha kuwa marekebisho ya kisheria yanafanyika ili kupunguza urasimu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Tunafanya kazi kuhakikisha miradi inafikia hatua ya kibiashara kwa haraka zaidi,” amesema Kafulila na kuongeza kuwa, tayari wataalamu 75 wa PPP wamepewa mafunzo ya kuongeza tija.

Baadhi ya miradi mikubwa ya PPP inayofanyiwa maandalizi sasa ni pamoja na Barabara ya Mzunguko ya Dar es Salaam, barabara kuu ya Igawa–Tunduma na Barabara ya Kibaha–Chalinze–Morogoro kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).