Migogoro ya ardhi yatawala tena mkutano wa  Mwigulu Dodoma

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ametoa maelekezo kwa viongozi ngazi ya wilaya na mkoa wakiwemo maofisa sekta ya ardhi kushughulikia migogoro ya ardhi iliyoibuliwa wakati wa mkutano wake mkoani Dodoma. 

Maelekezo hayo yametolewa leo Aprili 19,2026 kufuatia wananchi kuwasilisha malalamiko kadhaa mbele ya mtendaji yuyo Serikali mingi kati ya hiyo ikiwa inayohusu ardhi.
Akiwa kwenye ziara ya kawaida ya kukagua miradi ya maendeleo. Dk Mwigulu alitumia nafasi hiyo kusikiliza kero za wananchi wa  Wilaya ya  Chamwino mkoani Dodoma ambapo wananchi waliwasilisha kero zao nyingi zilihusu kuwapo kwa migogoro ya ardhi ya wao kwa wao na mingine inahusu wao na mamlaka husika.

Katika mkutano huo,  Dk Mwigulu amekiri robo tatu ya hoja alizozipokea ni migogoro ya ardhi huku akishangazwa na utendaji wa maofisa wa ardhi.

“Nimepokea hoja na robo tatu zinahusu migogoro ya ardhi watu wanaongelea wameporwa ardhi zao. Wenzetu watu ardhi kila siku mnaenda ofisini na mishahara mnalipwa.” 

Wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alipokuwa akizungumza  baada ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji  wa Miji 28,  Chamwino Dodoma, Aprili 19, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

“Mnaenda kazini Jumatatu hadi Ijumaa na watu wana migogoro wakisema mnachukua maeneo yao hamuwalipi, mnafanya nini,” amehoji Dk Mwigulu.

Kufuatia hali hiyo, Dk Mwigulu ameelekeza utatuzi huku akiahidi kufuatilia hatua kwa hatua kuhakikisha wananchi wanaishi bila ya migogoro hiyo. 

Migogoro hiyo ya ardhi, Dk Mwigulu amewahi kukutana nayo tena akiwa kwenye ziara mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Rukwa.

Tayari Dk Mwigulu amekwishaziagiza wizara kadhaa ikiwemo ya ardhi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuangazia tatizo la migogoro hiyo  nchini.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amesema Tanzania ni nchi iliyopiga hatua katika meneo ya maji, umeme, usafirishaji, afya hivyo ni jambo la kuthamini kama Taifa. 

Kuhusu sekta ya maji, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema uhitaji wa huduma hiyo Chamwino ni lita milioni saba na uzalishaji ni lita milioni nne hivyo kuna upungufu. Aweso amesema upo mradi unajengwa na sasa umefikia asilimia 70 ambapo ukikamilika utazalisha lita milioni 12 na wananchi wa Chamwino watapata maji asilimia 100.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu  Nchemba  akiweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Miji 28, Chamwino Dodoma, Aprili 19, 2026. Wengine kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Chamwino, George Malima, Naibu Waziri TAMISEMI (Afya), Dk Jafar Seif Rajab, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule na kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

 “Maelekezo ya Waziri     Mkuu ni mradi kukamilika kwa wakati na naahidi utakamilika. Mradi huu ni mkubwa na wananchi watataka kuuunganishiwa maji na haitazidi siku saba hilo kufanyika. Ikitokea mtendaji yeyote anamzingua mwananchi tutamzingua,” ameahidi. 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema  wanaendelea kushughulikia kero mbalimbali za wananchi wa mkoa huo, pia utekelezaji wa agizo la Rais juu ya kubana matumizi ikiwemo mafuta. 

Awali, akisoma ombi la Mbunge wa Chamwino Deogratius Ndejembi, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Janeth Mayanja, amesema mbunge huyo ameomba Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ipandishwe hadhi kuwa Halmashauri ya Mji au Manispaa kutokana na maendeleo yaliyopo sasa.

“Mbunge ameomba Serikali iongeze majengo katika Hospitali ya Uhuru ili ipandishwe hadhi wananchi wa Jimbo la Chamwino wapate huduma,” amesema mkuu huyo wa wilaya.