Dodoma. “Elimu siyo mfumo unaolinganishwa na mifumo ya mashine. Elimu ni mfumo wa watu; ni mfumo unaohusu watu wenyewe.”
Maneno haya yalipata kutamkwa na gwiji wa elimu na ubunifu, Ken Robinson, akizungumzia kile alichokiita “Bonde la Kifo cha Elimu” mwaka 2013.
Robinson, sasa marehemu, anatukumbusha kwamba elimu ni mfumo unaoundwa mahususi kwa lengo la kuwezesha ujifunzaji wa mtu aitwaye mwanafunzi, akisimamiwa kwa karibu na mtu anayeelewa vyema namna ujifunzaji huo unavyotokea.
Mtu huyu ambaye ndiye msingi wa elimu, tumempa jina la mwalimu. Elimu, kwa mantiki hiyo, si mashine inayoweza kurekebishwa kwa mabadiliko ya kimuundo pekee, bali ni mabadiliko yanayohusisha watu wenyewe na mahusiano yao.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na mijadala motomoto kuhusu mitalaa iliyoboreshwa kwa ngazi ya elimu ya awali, msingi, na sekondari.
Umuhimu wa mijadala hii unachochewa na ukweli mchungu kwamba, kwa muda mrefu, wanafunzi wamekuwa wakihitimu ngazi mbalimbali za elimu bila kuwa na matokeo ya maana wanayoweza kuonesha kama kielelezo cha kupita kwenye mfumo huo.
Kwa mfano, tunashuhudia wahitimu wengi wa vyuo vikuu wenye shahada mbili au tatu, lakini wakidaiwa kushindwa kutatua matatizo yanayoikabili jamii yetu.
Ombwe hili kati ya mahitaji ya jamii na ujuzi unaokuzwa shuleni lilikuwa msingi mkuu wa kuanzishwa kwa mchakato wa kupitia upya mitalaa.
Akilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza Aprili 22, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alisema: “Tupitie upya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na kufanya marekebisho kwenye mitalaa iliyopo ili ielekezwe kwenye kutoa elimu ujuzi.”
Kauli hii ya Serikali ni jibu la moja kwa moja kwa malalamiko ya wadau wengi wa elimu kuwa wahitimu wenye elimu rasmi, kwa maana ya vyeti na maarifa ya kinadharia, hawakuwa na uwezo wa kutumia maarifa hayo katika mazingira halisi.
Hii inahusisha uwezo wa kuanzisha biashara, kuwa na ufanisi kazini, na kutatua changamoto za kijamii.
Hatimaye, mchakato wa kupitia upya mitalaa ulikamilika mwaka 2023, na kufuatiwa na kuanza kwa mipango ya utekelezaji wake.
Hata hivyo, ukisikiliza mijadala mingi inayoangazia namna bora ya kuutekeleza mtalaa huo, utaona imejikita zaidi kwenye mabadiliko ya kimuundo; kama vile kuongezwa kwa masomo ya ufundi, kuhimizwa kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), lugha ya kufundishia, na masuala mengine ya kiufundi.
Kwa upande mwingine, hata mafunzo ya walimu yamejikita zaidi kwenye miundo ya mihutasari na hatua za kuandaa somo, mambo ambayo kwa mwalimu yanaonekana kuwa ya kiutawala zaidi kuliko ya kiutendaji.
Sina hakika ni kwa kiasi gani tunapozungumzia elimu tunamaanisha “ujifunzaji.” Je, masuala ya kisera na rasilimali katika elimu tunayoyajadili mara kwa mara yanatafsirika moja kwa moja kwenye ujifunzaji wa mwanafunzi binafsi?
Katika makala haya, ningependa kujenga hoja kuwa mazungumzo yanayolenga mabadiliko kuelekea “elimu bora,” bila kwanza kuuliza ni vipi mabadiliko hayo yanatafsirika kwenye namna mwanafunzi anavyopokea, anavyochakata, na anavyotumia maarifa, hayawezi kutusaidia kikamilifu.
Elimu ni mfumo wa kutoa maarifa, kukuza ujuzi, na stadi. Mfumo huu unaweza kutazamwa kupitia nyanja mbili: elimu rasmi na elimu isiyo rasmi. Elimu rasmi ni ile inayotolewa kupitia shule, vyuo, na taasisi rasmi kwa kutumia mitalaa iliyopangwa, walimu waliofunzwa, mitihani, na vyeti.
Elimu isiyo rasmi ni ile inayotolewa nje ya mfumo rasmi, mathalani kupitia semina, mafunzo kazini, ufundi stadi (kama ufundi magari au umeme wa mitaani), au hata mafunzo ndani ya jamii na familia.
Elimu hii, mara nyingi, haina vyeti rasmi lakini inatoa maarifa na stadi zinazotumika moja kwa moja maishani.
Ujifunzaji, kwa upande mwingine, ni mchakato wa ndani unaotokea kwa mtu binafsi. Ujifunzaji ni namna akili inavyopokea taarifa, inavyozichambua, inavyozihifadhi, na inavyozitumia. Ujifunzaji unaweza kutokea ndani ya mfumo wa elimu rasmi, isiyo rasmi, au hata bila kuwepo kwa mfumo wowote wa elimu.
Mwanafunzi, kwa mfano, anaweza kupata elimu rasmi ya kilimo chuoni, lakini ujifunzaji wa kweli unatokea anapokuwa shambani akijaribu kulima na kushuhudia matokeo halisi.
Fundi wa mitaani anaweza kuwa na elimu isiyo rasmi pekee, lakini ujifunzaji wake mkubwa ukamfanya afanikiwe zaidi kuliko mhitimu wa chuo kikuu. Kwa ufupi, elimu (rasmi au isiyo rasmi) inahusu utoaji, wakati ujifunzaji unahusu upokeaji na utumiaji.
Mazungumzo yetu mengi kuhusu elimu yanahusu mfumo, sera, bajeti, shule mpya, madarasa, vitabu, na mabadiliko ya kimuundo, badala ya utekelezaji wa ndani ya darasa na jinsi mwanafunzi anavyojifunza.
Tunazungumza kuhusu “mtalaa mpya” na “elimu ya umahiri,” lakini mara nyingi hatuulizi mabadiliko haya yanabadilisha vipi mazoea ya ufundishaji na ujifunzaji.
Tunafahamu kuwa tangu mwaka 2005, nchi yetu imejaribu kufanya marekebisho ya mitalaa yakilenga kugeuza elimu kuwa mfumo madhubuti wa kujenga umahiri.
Lengo limekuwa ni kuweka mazingira yanayowaondoa wanafunzi kwenye tabia ya kukariri taarifa wasizozielewa, na kuwaelekeza kwenye ujifunzaji wa kweli unaolenga kukuza stadi za kufikiri kwa kina, kutatua matatizo, na kujitegemea. Hata hivyo, ukiangalia tafiti zilizoangazia matokeo ya mabadiliko hayo, bado tunapata matokeo yaleyale ya kusuasua.
Walimu, kwa mfano, wanaamini kilichobadilika ni matamko ya wanasiasa na wasimamizi wa elimu, pamoja na aina ya mihutasari wanayoitumia kufundishia kile kile wanachokijua.
Hivyo, wanaendelea kufundisha vile vile, kwa mbinu zilezile zinazowawezesha wanafunzi kujifunza kwa mtindo uleule wa kizamani.
Kwa maana nyingine, tumejikuta tumewekeza fedha nyingi kujadili elimu ambayo haitafsiriki moja kwa moja kwenye ujifunzaji unaotokea darasani.
Tumefanikiwa kuboresha mitalaa. Mabadiliko haya ya mwaka 2023 yanatuhakikishia kulenga kuimarisha umahiri na stadi za karne ya 21, kama vile fikra tunduizi, ubunifu, utatuzi wa matatizo, uvumbuzi, ugunduzi, na ushirikiano.
Mfumo unaopendekezwa na mtalaa huu ni ule unaoanzia kwenye umahiri wa msingi, kisha kufuatiwa na shughuli za ujifunzaji zinazolenga kukuza umahiri huo.
Haya ni mabadiliko makubwa ya kimuundo yanayotutoa kwenye mtaaaa uliosisitiza ufundishaji wa maudhui ambayo, mara nyingine, hayakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na malengo ya mtalaa husika.
Hata hivyo, pengo kuu bado linaonekana katika hatua ya utekelezaji darasani. Walimu wengi hawajapata mafunzo ya kutosha kuelewa nini hasa kimebadilika katika ujifunzaji.
Je, katika mtalaa huu, mwanafunzi anajifunzaje tofauti na ilivyokuwa awali? Vipi kuhusu upimaji wa ujifunzaji huo? Tunafanyaje ili kujua kuwa mwanafunzi amejifunza kweli? Haya ni masuala yanayohitaji kuwekwa sawa wakati huu wa kuanza utekelezaji.
Kuna changamoto pia katika mfumo wa kutahini ujifunzaji. Je, kutegemea majibu ya kukariri yanayotolewa mwisho wa mzunguko wa masomo kunamsaidia mwanafunzi kujifunza?
Katika mtazamo wa elimu kama mfumo, tunaridhika zaidi kwa kuwadhibiti walimu na kurundika mamlaka kwa wasimamizi wa elimu, ambao mara nyingi hawajui kinachofanyika darasani lakini wanapenda kuona matokeo makubwa kwenye karatasi.
Elimu, katika muktadha huu, inaonekana kutomwamini mwalimu anayemfundisha mwanafunzi, na badala yake hurudisha mamlaka ya utahini kwa watu wa nje ambao hawakuhusika na mchakato wa darasani.
Je, tukiendelea na utaratibu huu, tunaweza kweli kumsaidia mwanafunzi kujifunza kwa ufanisi?
Aidha, mijadala yetu ya elimu inaonekana kupuuza sayansi ya ujifunzaji. Je, mtoto hujifunza katika mazingira gani?
Saikolojia ya elimu inaonesha kuwa ujifunzaji bora unahitaji mtoto kuhusisha kile anachokijua na kile anachojifunza; mtoto anapaswa kushirikishwa moja kwa moja katika kuchakata taarifa badala ya kuwa mpokeaji tu wa dhana zilizokwishaandaliwa.
Kwa maana nyingine, mtoto hujifunza kwa kushiriki kugundua kile anachopaswa kukikumbuka na kukitumia, na si kwa kusikiliza tu maelezo ya kitabuni au ya mwalimu.
Je, ni kwa kiasi gani mitalaa hii mipya inatoa nafasi kwa walimu kusimamia mchakato huo wa ujifunzaji? Je, tumewapa walimu mafunzo yanayowajengea uwezo wa kutafsiri miundo hii? Je, tumewapa rasilimali za kutosha kutekeleza kile kinachotarajiwa?
Elimu bila ujifunzaji?
Mjadala wa elimu uwe ni bungeni, kwenye makongamano ya kitaaluma, vyombo vya habari, au kwingineko, utabaki kuwa mazungumzo matupu kama hatutazingatia ujifunzaji. Pengine ni wakati wa kubadili mkondo wa mjadala huu.
Badala ya kuimba kauli mbiu za “tutoe elimu zaidi,” tuelekee kwenye mjadala wa “tufanye nini ili ujifunzaji uwe na maana zaidi.”
Tunahitaji kuuliza maswali magumu: Je, mwanafunzi anajifunza vipi? Tunafanya nini ili aweze kujifunza? Je, mwalimu anaamini katika sayansi ya ujifunzaji? Tufanye nini ili mwalimu aelewe kile hasa kilichobadilika na kukitafsiri katika vitendo vya darasani?
Tukitaka wanafunzi wajifunze kweli, hatupaswi tu kubadili mitalaa. Tunahitaji kubadili mazoea yetu ya kielimu pamoja na kuimarisha miundombinu ya madarasa na vifaa.
Tunahitaji kujadili ubora wa mafunzo endelevu kwa walimu ili kuwasaidia kuelewa wajibu wao katika ujifunzaji. Mwalimu asipojua namna ya kuwezesha ujifunzaji, ni rahisi kumsikia akizungumzia elimu, lakini akishindwa kuiwezesha na hatimaye atashindwa kupima ikiwa mwanafunzi ameelimika kweli.
Mwandishi ni mdau wa elimu, mshauri elekezi, na mhadhiri wa saikolojia ya ujifunzaji katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
