MICHEZO YATAJWA KUIMARISHA MSHIKAMANO KATI YA WAFANYAKAZI

Serikali imesisitiza umuhimu wa michezo kwa wafanyakazi kama sehemu muhimu ya kuimarisha afya na kuongeza ufanisi mahali pa kazi.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe.Rahma Kisuo, wakati akifungua rasmi Michezo ya Mei Mosi Kitaifa 2026 iliyofanyika Aprili 20, 2026 katika viwanja vya Sabasaba mkoani Njombe.

Amesema kuwa afya ya mfanyakazi ni mtaji mkubwa unaochangia maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla, hivyo michezo inapaswa kupewa kipaumbele.

Aidha, Mhe.Kisuo amehimiza wafanyakazi kote nchini kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara badala ya kusubiri vipindi vya mashindano pekee. Amesisitiza kuwa mazoezi yawe sehemu ya maisha ya kila siku ili kuboresha afya na kuongeza tija kazini, huku akizitaka taasisi zote za umma na binafsi kuhakikisha zinatoa nafasi kwa wafanyakazi kushiriki shughuli za michezo.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa wa Njombe Dkt. Stephane Nindi akimwakilisha Mkuu wa mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwa, kufanyika kwa Maadhimisho ya Meimosi Njombe kumetoa fursa za kibiashara kwa wananchi wa mkoa huo.

Katika hatua nyingine, amewapongeza washiriki wa Michezo ya Mei Mosi na kuwataka kudumisha nidhamu, mshikamano na ushindani wa haki.

Amesisitiza kuwa michezo iwe chachu ya kuimarisha udugu na ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi badala ya kuwa chanzo cha migogoro.

Kwa mwaka 2026, michezo hiyo inaongozwa na kauli mbiu isemayo, “Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050,” huku watumishi na wachezaji wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) wakiwa miongoni mwa washiriki wa ufunguzi huo.