Dar es Salaam. Matumizi ya majengo yanayoendelea kujengwa katika eneo la Kariakoo yameendelea kuzua maswali mazito miongoni mwa wananchi.
Nani anawajibika kwa hali hiyo, ni wapi mifumo ya usimamizi imekwama na kwa nini sheria zilizopo haziwalindi wananchi dhidi ya hatari zinazoibuka mara kwa mara?
Uchunguzi wa Mwananchi wa miezi mitatu Desemba 2025 na Februari 2026 unaonesha tatizo hilo halitokani na ukosefu wa sheria wala mifumo ya usimamizi, bali linachangiwa kwa kiasi kikubwa na umiliki wa baadhi ya majengo katika eneo hilo, yanamilikiwa na watu wenye ushawishi mkubwa (vigogo).
Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wasimamizi wa baadhi ya majengo ya eneo hilo anasema licha ya kuwepo kwa watu wengi wanaodai umiliki wa maeneo ya Kariakoo, bado kuna majengo yanayomilikiwa na vigogo jambo linalofanya iwe vigumu kuyasimamia au kusimamisha matumizi yake kisheria.
Moja ya jengo linaloendelea la ujenzi eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
“Sheria zipo na zinapaswa kufuatwa, lakini majengo mengi ya maeneo haya yanamilikiwa na vigogo. Hivyo, inakuwa vigumu kwa mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria kwa sababu wanagusa masilahi ya watu wenye nguvu,” anasema.
Akizungumza na Mwananchi, mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kariakoo Magharibi, Said Omary anasema kutokana na muundo wa uongozi wa Serikali za mitaa, hawana mamlaka ya kusimamisha ujenzi moja kwa moja, zaidi ya kutoa taarifa katika ofisi za kata ili hatua zaidi zichukuliwe.
Pia, anasema kukosekana kwa uwajibikaji miongoni mwa viongozi katika ngazi mbalimbali ndicho chanzo kikuu cha majanga yanayojitokeza mara kwa mara katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Omary, tatizo si uhaba wa sheria, bali ni utekelezaji wake ambao umekuwa dhaifu, hali inayochangia hatari kubwa kwa wananchi na kuibua lawama dhidi ya viongozi na Serikali kwa jumla.
Anasema sheria na taratibu za ujenzi zipo wazi na zinafahamika na wahusika wote, lakini changamoto kubwa ni kutozingatiwa kwa misingi iliyowekwa pamoja na kuingiliwa na masuala ya kisiasa.
“Sheria zipo na kila mmoja anazijua, lakini utekelezaji wake ndio changamoto, siyo kwamba tatizo halipo, bali siasa imetengeneza utaratibu wa kutofuata misingi na hii ndiyo shida. Hali hii inasababisha lawama kuelekezwa kwa viongozi na Serikali,” anasema.
Anasema lawama nyingi zinazotolewa kuhusu ujenzi unaoendelea na ajali zinazotokea zinatokana na ukosefu wa ukaguzi wa mara kwa mara pamoja na kutoshirikishwa kwa viongozi wa ngazi za chini.
Anasema kama mwenyekiti wa mtaa, hajawahi kushirikishwa katika utoaji wa vibali vya ujenzi, hali inayomfanya hata kutotambulika anapofika katika maeneo ya majengo yanayoendelea kujengwa.
“Ukifika kwenye jengo, mhusika anauliza mimi ni nani kwa sababu hajaelezwa. Kinachotokea ni kuona watu wanabomoa na kupandisha majengo yao, lakini linapotokea tatizo, mwenyekiti ndiye anayetafutwa kutoa maelezo,” anasema.
Wakati mwenyekiti akieleza hayo, mmoja wa makandarasi ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema wanapofuatwa na watu wanaojitambulisha ni wakaguzi au ndiyo wasimamaizi wa maeneo hayo hutumia mwanya huo kuzungumza na mwenye mradi na humalizana wenyewe.
“Kazi yangu ni kusimamia miradi na kuwepo na nyaraka muhimu na mara nyingi unapotokea ukaguzi, hata kama sipo napigiwa simu nikifika baada ya utambulisho huwakabidhi kwa wenye miradi kwa sababu sina majibu ya moja kwa moja,” anasema.
Moja ya jengo linaloendelea la ujenzi eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Anasema kumekuwa na makundi tofauti yanayofika katika maeneo yao ya ujenzi ambapo kwa wiki wamekuwa wakijitambulisha kutoka katika taasisi tofauti, hivyo ni ngumu kwa wao kujadiliana nao.
Kutokana na maelezo hayo Mwananchi ilizungumza na baadhi ya mafundi katika majengo yanayoendelea kujengwa na majibu yalikuwa endapo kutakuwa na ukaguzi hutoa namba za simu na kila kitu humalizika huko.
“Sisi ni vibarua hatuna nguvu wakija wahusika tukiambiwa tusimamishe ujenzi tunapiga simu sehemu husika na hatuwaoni tena wahusika,” anasema.
Anasema jambo hilo halijawahi kutokea mara moja hivyo hawezi kueleza moja kwa moja kuwa kuna kiashiria cha rushwa kwani wahusika hawatokei tena.
Mwananchi ilipojaribu kuwatafuta Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Ilala mwishoni mwa Novemba, 2025 wakati wa uchunguzi wa awali ilihitaji kupatiwa muda kwa ajili ya kufuatilia
“Tunaomba kufuatilia jambo hili, tutatuma timu yetu ya uchunguzi kufuatilia jambo hili ambalo umetueleza na kisha tutakupeni majibu,”anasema Mkuu wa Takukuru Ilala, Faustine Maijo.
Desemba 2025 Mwananchi ilirudi tena kwa mkuu wa Takukuru kuomba mrejesho alidai yupo likizo, hivyo kuelekeza kwa mtu mwingine lakini tofauti na matarajio mtu huyo alielekeza kwa ofisa mwingine.
Hata hivyo, Januari 7, 2026 Mwananchi ilimtafuta ofisa huyo kwa ajili ya kutoa majibu ya maswali, lakini alihitaji kuelezwa majengo husika ambayo yanaashiria uwepo wa rushwa.
“Fuatilia utuambie ni sehemu ipi haswa au majengo yapi yanahusika ili tufuatilie tukupe taarifa nzuri,” anasema ofisa huyo na kuongeza.
“Ukiniambia Kariakoo kunashida ya matumizi ya majengo yasiyokamilika nashindwa kukuelewa maana Kariakoo ni kubwa, nikupe muda ulipate ni eneo gani maaalumu lenye changamoto tutaenda ili tukapate taarifa sahihi, kwa jumla hivi hivi ni ngumu kujua tuanzie wapi,” alisema bila kutaja jina lake.
Akizungumza na Mwananchi, Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam, Isack Mtega anasema wamiliki wengi wanahisi hatua hii ni kuingiliwa katika majengo yao na kushindwa kuelewa umuhimu wake.
Moja ya jengo linaloendelea kufanyiwa ukarabati Kariakoo.
Aidha, anasema baadhi ya wenyeji wanapopata kibali cha ujenzi mara moja, hawana muda wa kupitia taratibu zote za kiutaratibu, jambo linalosababisha kuingizwa watu kwenye majengo bila ukaguzi wa halmashauri.
“Tatizo kubwa ni elimu kwa wamiliki wa majengo, wengi wanahisi kwamba, kurudi halmashauri kwa ukaguzi ni kuingiliwa kwenye majengo yao, hivyo kushindwa kufuata taratibu za Sura ya 288 ya Sheria ya Serikali za Mitaa,” anasema Mtega.
Mtega anasema ni wachache wanaofuata utaratibu kwa makini, na hawa ni wawekezaji wa Kihindi.
“Wenyeji wengi wanapopata kibali hawana muda wa kupitia hatua hizi. Lakini Wakihindi wanapenda kusoma sheria na kufuata taratibu, ndio sababu pekee wanazingatia masharti ya Sura ya 288,” anasema.
Changamoto nyingine anasema ni hali ya kifedha ya wawekezaji kwani wengi hujenga kwa kutumia mkopo au kuingia ubia na inapotokea jengo halijakamilika, wanahitaji kupata kipato kwa kuanza kupangisha sehemu ndogo.
“Wawekezaji wa majengo pesa zao ni za kujitafuta, wengine wanapojenga wamekopa au kuingia ubia. Hivyo, ni vigumu kusubiri hadi jengo lote likamilike,” anasema Mtega.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Ilala, Peter Mabusi anasema wafanyabiashara wengi wanaweka mbele faida na kuacha kuzingatia taratibu za kiusalama, jambo linalohatarisha maisha ya watu na mali zao.
“Kariakoo ishaungua mara nyingi, sababu kubwa ni mahitaji ya biashara, watu wanaingia kujenga na kuanza biashara kabla majengo hayajakamilika au kukaguliwa. Mteja anaambiwa ajikamate mwenyewe, mradi biashara ianze,” anasema Mabusi.
Anasema mara nyingi wamiliki wa majengo huanza kujenga ghorofa chache, kwa ajili ya kuendelea kupata kipato, kwani hajui ni lini anaweza kumaliza.
“Mtu anajenga ghorofa mbili au tatu kisha anapangisha watu ili aendelee kupata kipato kwa sabbau anaweza kusimamisha jengo hata miaka miwili au zaidi wakati huo kuna uhitaji wa wateja pamoja na ushindani,”anasema.
Sheria zipo, utekelezaji changamoto
Mabusi anasema Jeshi la Zimamoto lina mamlaka ya kusitisha matumizi ya majengo yasiyokidhi viwango vya usalama, kwa mujibu wa sheria za zimamoto za mwaka 2007 zinazotaka majengo yakaguliwe kabla ya kutumika.
Hata hivyo, anasema hali ya kiuchumi na utegemezi wa biashara Kariakoo huwafanya wadau kuwa katika mkwamo wa kiuamuzi.
“Sheria zipo na tunaweza kuchukua hatua, lakini ukisema usiruhusu biashara ifanyike kabisa, unakutana na changamoto kubwa watu wanaitegemea Kariakoo kwa maisha yao,” anasema.
Kamanda Mabusi anasema tatizo lingine kubwa ni kutokuwapo kwa muafaka wa kanuni za ujenzi na usalama kati ya taasisi mbalimbali za Serikali, hali inayosababisha kila mmoja kufanya lake.
Anasema mkanganyiko huo huwafanya wamiliki wa majengo na makandarasi kuchagua kanuni zinazowapa unafuu wa haraka, badala ya zile zinazolinda usalama wa watu.
“Unaweza kukuta Zimamoto tunasema lingine na wengine na wao wanasema linguine, kwa hiyo tunajikuta tunampa mzigo mtumiaji na ndiyo anachukua uamuzi wa kufanya anachokiona,” anasema Mabusi.
Anasema bila kanuni kusomana na kusimamiwa kwa pamoja, hatari zinazojitokeza Kariakoo zitaendelea kujirudia na kusababisha hasara kwa wafanyabisahara nan chi kwa ujumla.
“Suluhisho si kukata biashara, bali kuhakikisha kanuni zote za ujenzi na usalama zinasomana na zinatekelezwa kikamilifu kabla jengo halijaanza kutumika,” anasema Mabusi.
Kauli hii ya Mabusi inaungwa mkono na Mkuu wa Kitengo cha Mipango Chama cha Usalama na Afya Mahala pa Kazi Tanzania (Tohasa), Manyanda Maziku anayesema tatizo hilo ni sugu na linatokana na kila taasisi kutunga sheria au kanuni kwa kuzingatia mahitaji yake pekee bila kuangalia masilahi mapana ya taasisi nyingine au usalama wa jamii kwa jumla.
Kwa mujibu wa Kanuni za Usalama na Afya Kazini (Sekta ya Ujenzi na Majengo) inayojulikana kama GN No. 73 ya mwaka 2015, mkazo mkubwa umewekwa katika usalama wa wafanyakazi waliopo eneo la kazi.
Hata hivyo, anasema kanuni hiyo haijaweka wazi zuio la kutumia jengo ambalo halijakamilika, bali inaelekeza kuchukua tahadhari kama kuweka uzio nyavu, kudhibiti njia za kuingia au kuzuia watu wasiokuwa na uhusiano na ujenzi kufika eneo hatarishi.
“Kauli ya kwa kiwango kinachowezekana ni dhaifu kisheria, kila mtu anaweza kuitafsiri kwa namna yake,” anasema.
Kwa upande mwingine, Maziku anasema Kanuni za Mipango Miji za mwaka 2018 zinaelekeza wazi hakuna mtu anayeruhusiwa kutumia jengo au eneo ambalo halijakamilika bila kupata Cheti cha Matumizi (Certificate of Occupancy), kinachotolewa kupitia Fomu Na. 10. Kisheria, jengo linapaswa kukamilika kwanza kabla ya kuruhusiwa kutumika.
Hapa ndipo mgongano mkubwa wa kisheria unapojitokeza, sheria za usalama na afya kazini hazizungumzi lugha moja na sheria za mipango miji.
“Ni kama taasisi mbili zinazoongea lugha tofauti, mipango miji inasema hairuhusiwi kabisa kutumia jengo ambalo halijakamilika, wakati upande wa usalama kazini unaelekeza tahadhari zichukuliwe tu,” anasema Maziku.
Athari za mkanganyiko huo zinaonekana wazi katika majengo mengi, ujenzi unaendelea juu, huku chini watu wakiendelea kufanya biashara au shughuli nyingine za kiraia. Katika mazingira hayo, hatari kwa wananchi ni kubwa zaidi kuliko hata kwa wafanyakazi wa ujenzi.
“Wafanyakazi wa ujenzi tayari wanakuwa wameandaliwa, wamefunzwa na wana vifaa vya kujikinga. Lakini raia wa kawaida anayepita au anayefanya biashara chini ya jengo linalojengwa, hana kinga yoyote,” anasema.
Anatoa mfano wa vifaa vinavyoweza kudondoka kutoka juu kama nyundo, mbao au vyuma na kusababisha majeraha au vifo kwa watu wasiokuwa na hatia.
Anasema sheria nyingi hazijaweka ulinzi wa kutosha kwa wapita njia au wageni.
