Spika akemea ukiukwaji wa kanuni bungeni, amtaja Ado Shaibu

Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Mussa Zungu, amewakumbusha wabunge kuzingatia kikamilifu taratibu na kanuni za uendeshaji wa Bunge, akionya kuwa ukiukwaji wa maelekezo ya kiti hautavumiliwa, huku akitoa mfano wa tukio lililomhusisha Mbunge wa Tunduru Kusini, Ado Shaibu.

Akitoa mwongozo bungeni leo Aprili 21, 2022 kutokana na hoja ya utaratibu iliyoibuliwa na Mbunge Timothy Mzava, Spika amesema kitendo cha Ado kuendelea kuchangia baada ya muda wake kuisha ni kinyume cha kanuni za Bunge na maelekezo ya kiti.

Tukio hilo lilitokea Aprili 17, 2026 wakati mbunge huyo alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Licha ya kupewa taarifa kuwa muda wake umefika mwisho ili kutoa nafasi kwa wabunge wengine, aliendelea kuzungumza.

“Kiti kina mamlaka ya kuhakikisha utaratibu wa uendeshaji bora wa shughuli za Bunge unazingatiwa wakati wa mjadala. Kanuni zimeweka wazi kuwa uamuzi wa Spika kuhusu utaratibu ni wa mwisho,” amesema Zungu.

Amesisitiza  kuwa wabunge wote wanapaswa kuheshimu muda wao wa kuchangia na kutii maelekezo ya kiti kila yanapotolewa, akibainisha kuwa Ado hakuzingatia masharti hayo kwa kuendelea kuzungumza hata baada ya kuonywa.

Amesema bado kuna baadhi ya wabunge wanaendelea kufanya makosa kama hayo, akiwataka kujirekebisha na kujiepusha na vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyoweza kuvuruga mwenendo wa mijadala ya Bunge.

Spika ameonya kuwa iwapo hali hiyo itaendelea, hatua za kikanuni zitachukuliwa kwa mujibu wa Kanuni ya 86 ya Kanuni za Bunge za mwaka 2025.

Hata hivyo, Zungu amesema  amemsamehe Ado kutokana na kuwa miongoni mwa wabunge wapya, akiwataka wabunge wengine kujifunza na kuzingatia taratibu.

Katika hatua nyingine, Spika amegusia mchango wa Ado uliorejea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2023/2024, akieleza kuwa suala hilo tayari lipo katika kamati husika za Bunge kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Amebainisha kuwa taarifa hiyo pamoja na ile ya mwaka 2024/2025 zimewasilishwa kwenye kamati za kudumu zinazosimamia matumizi ya fedha za umma, ikiwemo Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambayo inaongozwa na Ado.

Spika amesisitiza kuwa masuala yaliyoko kwenye kamati hayapaswi kujadiliwa nje ya vikao vya kamati husika, hasa na wenyeviti wa kamati hizo.

“Niwaombe sana wabunge, nafahamu tuna ugeni lakini tuendelee kujifunza,” amesema Zungu.