Rais Samia aihakikishia AFLN mageuzi na demokrasia Tanzania

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameuambia ujumbe wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Afrika (AFLN) kuwa Serikali itaendelea kupanua fursa za uongozi kwa wanawake na vijana.

Mbali na hilo, Rais Samia ameieleza AFLN kuwa Serikali itaendelea kushikilia misingi ya demokrasia, ushirikishwaji na maendeleo endelevu.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, jana Jumatatu, Aprili 20, 2026, imeeleza kuwa Rais Samia alikutana na ujumbe huo siku hiyo Ikulu, jijini Dar es Salaam.

AFLN inaundwa na marais wastaafu na viongozi wanawake waandamizi kutoka Afrika na taasisi za kimataifa, akiwemo Rais mstaafu wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf; Rais mstaafu wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde, Joyce Mends-Cole na Hawine Amdissa.

Katika mazungumzo hayo, Rais Samia ameiambia AFLN kuwa, pamoja na mambo mengine, Serikali ya Tanzania itaendelea kulinda amani, kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

“Nchi itaendelea kuimarisha ushirikiano na wadau katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa,” ameeleza Rais Samia.

Rais wa Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Uongozi wa Mtandao wa Wanawake Viongozi Afrika (AWLN) uliongozwa na mlezi wake, Rais Mstaafu wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, jana Aprili 20, 2026 Ikulu Jijini Dar es Salaam.

AFLN ni jukwaa linalowaunganisha viongozi wanawake wa sasa na wastaafu wa bara la Afrika kwa lengo la kuendeleza uongozi wa wanawake, ujenzi wa amani na utawala bora barani Afrika.

Katika ujumbe wao, AFLN imeipongeza Serikali ya Tanzania kwa kurejesha hali ya amani na utulivu kufuatia matukio ya vurugu ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Pia, wamepongeza juhudi za Serikali katika kulinda umoja wa kitaifa na kurejesha shughuli za kawaida za kiuchumi na kijamii.

Wameeleza kuwa Tanzania imeendelea kujijengea sifa ya kuwa nchi ya amani na utulivu barani Afrika, wakipongeza uongozi thabiti wa Samia katika kuiongoza nchi katika kipindi kigumu bila kuyumbisha utendaji wa taasisi na utulivu wa ndani.

Katika mazungumzo hayo, ujumbe wa AFLN umeelekeza msisitizo katika umuhimu wa kuendeleza mageuzi ya kisiasa na kiutawala ili kuimarisha demokrasia, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wadau.

“Pia umehimiza kukuza nafasi za uongozi kwa wanawake na kuimarisha ushiriki wao katika ngazi mbalimbali za uamuzi,” imeeleza.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Uongozi wa Mtandao wa Wanawake Viongozi Afrika (AWLN), uliongozwa na mlezi wake, Rais Mstaafu wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, jana Aprili 20, 2026 Ikulu Jijini Dar es Salaam.

“AFLN ipo tayari kuisaidia Tanzania kulea kizazi kipya cha viongozi wanawake, ikisisitiza umuhimu wa kuweka mifumo itakayowawezesha si tu kufika kwenye nafasi za uongozi, bali pia kuzitumikia vizuri nafasi hizo,” imeeleza taarifa hiyo.

Kabla ya kuonana na Rais Samia, ujumbe wa AFLN siku hiyo hiyo ya jana Jumatatu ulikutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ulioongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche, na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

Wengine ni manaibu makatibu wakuu Bara, Amani Golugwa na Ali Ibrahimu (Zanzibar) na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema, Suzan Lyimo.

Katika kikao hicho, Chadema iliwasilisha msimamo wake rasmi kama ulivyoazimiwa na Kamati Kuu ya chama na kueleza kwa kina matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu na vitendo vya ukatili vinavyodaiwa kutokea kabla, wakati na baada ya Oktoba 29, 2025.

Uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika picha ya pamoja na ujumbe wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Afrika (AFLN) uliokuwa ukiongozwa na aliyekuwa Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, akiwa ameambatana na aliyekuwa Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde walipokutana Jana Jumatatu, Aprili 20, 2026 jijini Dar es Salaam.

Chadema kilisisitiza umuhimu wa uchunguzi huru na haki, uwajibikaji kwa wote waliohusika, pamoja na kulindwa  misingi ya demokrasia, haki na utawala wa sheria nchini.