WAZIRI DEOGRATIUS NDEJEMBI AWASILISHA BAJETI YA TRILIONI 2.5 YA NISHATI KWA MWAKA 2026/2027

Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amewasilisha bungeni mjini Dodoma makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2026/2027, akieleza kuwa jumla ya Shilingi trilioni 2.525 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo.

Akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri Ndejembi amesema kati ya fedha hizo, Shilingi trilioni 2.462 sawa na asilimia 97.5 ya bajeti yote ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Kati ya fedha za maendeleo, Shilingi trilioni 1.602 ni fedha za ndani, huku Shilingi bilioni 859.9 zikiwa ni fedha kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya kimkakati katika sekta ya nishati.

Aidha, amesema jumla ya Shilingi bilioni 63.036 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, sawa na asilimia 2.5 ya bajeti yote ya wizara. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 52.939 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi (PE), wakati Shilingi bilioni 10.097 zikitengwa kwa matumizi mengineyo ya kawaida (OC) kwa Wizara ya Nishati na taasisi zake, ikiwemo PURA.

Waziri Ndejembi alisisitiza kuwa bajeti hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, kuendeleza miradi ya kimkakati na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia sekta ya nishati.