Mara. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda amesema mamlaka hiyo itaendelea kupambana na watu wote wanaokwepa kodi ili kuwalinda wafanyabiashara wanaozingatia sheria za kodi.
Akizungumza na walipakodi mkoani Mara jana Jumanne, Aprili 14, 2026 kwenye kikao kilichofanyika wilayani Bunda, Mwenda amesema watu wanaokwepa kodi wamekuwa wakiondoa ushindani wa biashara sokoni, hivyo TRA itaendelea kupambana nao na kuwachukulia hatua za kisheria.
“Tutawatafuta popote walipo watu wanaokwepa kodi maana wamekuwa wakiwaumiza walipakodi wanaozingatia sheria, huwezi kukwepa kodi milele, ipo siku tutakukamata. Na ninatoa wito kwa yeyote anayewafahamu watu wanaokwepa kodi awasiliane na TRA ili achukuliwe hatua,” amesisitiza.
Aidha, amewaonya wafanyabiashara wanaojihusisha na uingizaji wa bidhaa za magendo kwenye mpaka wa Sirali na mipaka mingine, na kueleza kuwa TRA ipo kazini kupambana na magendo na itawafikia.
Kuhusu uhusiano na walipakodi Kamishna Mkuu Mwenda amesema wataendelea kuboresha, kuwasikiliza, kutatua changamoto zao pamoja na kuwezesha biashara nchini.
Amesema TRA itaendelea kuongeza wigo wa kodi nchini kwa kusajili walipakodi wapya na hii ni kutokana na nguvu kazi iliyopo nchini kutowiana na idadi ya walipakodi ambao ni milioni nane huku nguvu kazi ikiwa ni zaidi ya milioni 30.
Kwa upande wake, Kamishna wa Kodi za ndani, Michael Muhoja amesema TRA itaendelea kutoa elimu ya kodi kwa wananchi ili kuwawezesha kutambua umuhimu wa kulipa kodi.
Miongoni mwa walipakodi waliohudhuria mkutano huo wameipongeza TRA kwa kuendelea kuwa karibu nao na kuwapatia elimu ya kodi kila inapohitajika.
Aidha akiwa mkoani Mara, Mwenda ametembelea makumbusho ya hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwenye kijini cha Mwitongo Butiama wilayani Musoma na kuwataka Watanzania waendelee kumuenzi kwa kulipa kodi kwa hiari.
Amesema miongoni mwa vitu vilivyokuwa vikitiliwa mkazo na Baba wa Taifa enzi za uhai wake ni kulipa kodi ambapo aliwataka wote wenye nguvu za kufanya kazi kila mmoja achangie kodi kulingana na uwezo wake.
Amesema ili kuonyesha kuendelea kuenziwa kwa busara za Mwalimu Nyerere, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa miongozo mbalimbali kwa TRA kuhusu ukusanyaji wa kodi ambayo imeiwezesha kukusanya kwa wingi.
Akiwa katika Makumbusho ya Mwalimu Nyerere Mwitongo, Kamishna Mwenda ameweka shada la maua kwenye kaburi la Baba wa Taifa.
Katika hatua nyingine, Mwenda amekagua ujenzi wa ofisi ya TRA Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza na kutoa muda wa mwezi mmoja kuanzia Aprili 15, 2026 kwa Mkandarasi wa Kampuni ya C.F.Builders Ltd anayejenga ofisi hiyo kukamilisha ujenzi.
Mwenda amemtaka mkandarasi huyo ambaye alitakiwa kukamilisha ujenzi na kukabidhi jengo hilo tangu mwishoni mwa mwaka 2024 kukamilisha ujenzi huo ndani ya mwezi mmoja la sivyo hatua zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha ameagiza kufanyika kwa uchunguzi ndani ya mamlaka ili kuona kama mkandarasi huyo kama amepewa kazi nyingine ya kujenga majengo ya TRA.
“Hatuwezi kuvumilia kuwa na mkandarasi ambaye hawajibiki ipasavyo, kinachotakiwa hapa ni kukamilisha ujenzi ndani ya mwezi mmoja na afuatiliwe ili kuona kama kuna kazi yoyote amepewa na mamlaka, na asipewe kazi nyingine yoyote maana ufanyaji kazi wake hauridhishi,” amesema Mwenda.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya C.F.Builders Ltd, Fred Chacha amesema watajitahidi kukamilisha ujenzi huo kwa muda uliotolewa.
