Mbunge wa Marekani, Eric Swalwell, ametangaza rasmi mpango wake wa kujiuzulu kutoka Bunge la Marekani kufuatia tuhuma za unyanyasaji wa kingono na mienendo isiyofaa, zilizozua mjadala mkubwa kisiasa.
Katika taarifa aliyochapisha kupitia mtandao wa X, Swalwell alisema uamuzi huo umechochewa na shinikizo kutoka kwa wabunge wa pande zote mbili za kisiasa waliomtaka aachie ngazi, pamoja na kuanza kwa uchunguzi wa House Ethics Committee.
“Ni makosa kumfukuza mtu bila kufuata taratibu za haki, lakini pia si sahihi kwa wapiga kura wangu kuniona nikiwa nimevurugwa na majukumu yangu. Hivyo, nimeamua kujiuzulu,” alisema Swalwell.
Hata hivyo, alikiri kufanya makosa ya maamuzi katika maisha yake ya zamani, huku akisisitiza kuwa baadhi ya tuhuma dhidi yake si za kweli na ataendelea kupambana nazo kisheria.
Hatua hiyo imekuja muda mfupi baada ya Swalwell kusitisha kampeni yake ya kugombea ugavana wa California, huku uchunguzi wa tuhuma hizo ukiendelea.
Swalwell, ambaye amehudumu bungeni tangu mwaka 2013, hakutaja tarehe rasmi ya kuondoka madarakani lakini alisema atahakikisha ofisi yake inaendelea kuwahudumia wakazi wa jimbo lake la 14 hadi pale atakapoondoka rasmi.
Kwa mujibu wa sheria za California, uamuzi wa kuitisha uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi hiyo uko mikononi mwa Gavana Gavin Newsom.
Wakati huo huo, wanasiasa wengine pia wamehusishwa na tuhuma za aina hiyo, akiwemo Tony Gonzales, ambaye anakabiliwa na madai ya kuwa na uhusiano usiofaa na mfanyakazi wake wa zamani—jambo linalokiuka kanuni za Bunge la Marekani.
Baadhi ya viongozi waandamizi wa chama chake wameunga mkono uamuzi huo. Miongoni mwao ni aliyekuwa Spika wa Bunge, Nancy Pelosi, aliyesema Swalwell amefanya uamuzi sahihi kujiuzulu.
Kashfa hiyo imeendelea kutikisa siasa za Marekani, huku ikizua mjadala mpana kuhusu uwajibikaji na maadili ya viongozi wa umma.