Fikiri Elias aweka rekodi ya kwanza Coastal

KOCHA Fikiri Elias, ameanza na mguu mzuri ndani ya Coastal Union akifanikiwa kuweka rekodi ambayo watangulizi wake wameishindwa.

Elias ambaye Aprili 11, 2026 alianza kuiongoza Coastal Union akichukua nafasi ya Mohamed Muya, ameweka rekodi ya kushinda mechi mbili mfululizo kikosini hapo zote Coastal Union ikiwa nyumbani.

Kabla ya ujio wa Elias, Coastal Union chini ya Ali Mohammed Ameir na Muya, haikuwahi kushinda mechi mfululizo, hali ambayo mabosi wa timu hiyo kwa nyakati tofauti walifikia makubaliano ya kuachana na makocha hao.

Pengine unaweza kusema uamuzi wa mabosi hao kumleta Elias ulikuwa sahihi kwani Jumatano ya Aprili 15, 2026, kocha huyo ameiongoza Coastal Union kuichapa Dodoma Jiji mabao 3-1 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kabla ya hapo, Aprili 11, 2026 aliiongoza kwa mara ya kwanza Coastal Union tangu arejee kikosini hapo na kushinda 2-0 dhidi ya Pamba Jiji ikiwa ni hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB.

Katika mechi ya dhidi ya Dodoma Jiji, Coastal Union ilikwenda mapumziko ikiongoza kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Greyson Gwalala dakika ya 15 na Maabad Maulid (dk 32) yote kwa mashuti makali nje ya boksi.

Timu hizo ziliporudi kipindi cha pili, tahadhari ilikuwa kubwa kiasi cha kufanya hadi zinafika dakika 90 za kawaida, hakuna bao lingine lililofungwa.

Katika muda wa nyongeza baada ya dakika tisini kutimia, Wazir Junior aliipatia Dodoma Jiji bao kwa kichwa dakika ya 90+1, kisha Geofrey Manyac wa Coastal Union dakika ya 90+4 akahitimisha ushindi huo kufuatia kuanzishiwa kona fupi.

Ushindi huo unaifanya Coastal Union kutoka nafasi ya 13 hadi 12 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikifikisha pointi 19, wakati Dodoma Jiji ikisalia nafasi ya nane na pointi 24 huku zote zikicheza mechi 19.

Hivi sasa Coastal Union imeshinda mechi nne za Ligi Kuu Bara, sare saba na kupoteza nane, bado haipo salama zaidi ikipambana kutoka chini ya msimamo wa ligi hiyo ijinusuru na janga la kushuka daraja.