UNDP na Finland Wawekeza Katika Biashara Endelevu Tanzania

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dr Linda Salekwa (katikati) na wageni wengine wakipiga makofi wakati Shirika la UNDP pamoja na Serikali ya Finland wakitambulisha biashara bunifu 14 ndogo ndogo na za kati (MSMES) kupitia mpango wa #GreenCatalyst. Hafla hiyo ilifanyika Mjini Njombe.

United Nations Development Programme (UNDP) Tanzania, kupitia programu yake ya ubunifu ya FUNGUO, imezindua rasmi Biashara Ndogo, Ndogo na za Kati (MSMEs) bunifu 14 chini ya mpango wa #GreenCatalyst unaofadhiliwa kwa ushirikiano na European Union, Foreign, Commonwealth & Development Office (FCDO) na Serikali ya Finland.

Hatua hiyo inaashiria mafanikio makubwa katika juhudi za kukuza ujasiriamali endelevu na uzalishaji wa ajira ndani ya mnyororo wa thamani wa misitu nchini Tanzania.

Uzinduzi huo ulifanyika chini ya kaulimbiu “Kuchochea Ubunifu na Ujasiriamali katika Mnyororo wa Thamani wa Misitu”, ukileta pamoja wadau kutoka Nyanda za Juu Kusini na maeneo mengine ili kuonesha biashara zilizochaguliwa na kuangazia fursa mpya za uwekezaji katika sekta hiyo.

Meneja wa Programu ya FUNGUO, Joseph Manirakiza.

Aidha, tukio hilo lilitumika pia kuzindua rasmi awamu ya pili ya maombi ya ruzuku ya kuchochea ukuaji, ambapo wabunifu wapya wa biashara rafiki kwa mazingira wanahimizwa kuwasilisha maombi yao.

Mpango wa #GreenCatalyst, unaofadhiliwa mahsusi na Finland, unalenga kuchochea ubunifu na ujasiriamali katika sekta ya misitu huku ukihamasisha ajira vijijini na kufungua fursa za uwekezaji kwa MSMEs. Mpango huu pia unakamilisha juhudi za mradi wa FORLAND unaolenga usimamizi endelevu wa misitu, matumizi bora ya ardhi na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji, zaidi ya maombi 160 yalipokelewa mwaka 2025, ambapo biashara 14 zilichaguliwa kupitia mchakato makini uliosimamiwa na kamati huru ya uwekezaji. Biashara hizo zilipokea zaidi ya shilingi bilioni moja kama ruzuku pamoja na msaada wa kiufundi.

Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa UNDP, John Rutere akiongea jambo.

Ubunifu wa biashara hizo unahusisha sekta mbalimbali ikiwemo uchakataji wa mbao rafiki kwa mazingira, ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali, bidhaa za mianzi, uzalishaji wa mafuta kwa matumizi mbalimbali, pamoja na huduma za kidijitali zinazohusiana na misitu.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja wa Programu ya FUNGUO, Joseph Manirakiza, alisema awamu ya pili ya maombi itakayofungwa Mei 31, 2026 inalenga kusaidia MSMEs zilizo katika hatua za awali au zinazokua ili kufungua fursa za biashara endelevu, kuongeza ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa vijijini.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa UNDP Tanzania, John Rutere, alisisitiza umuhimu wa kutumia rasilimali za misitu kwa uwajibikaji ili kuchochea ajira na ukuaji wa uchumi huku ukilinda mazingira kwa vizazi vijavyo.

Akithibitisha dhamira ya Finland, William Nambiza alisema nchi hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za kukuza mnyororo wa thamani wa misitu endelevu nchini Tanzania.

Kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dr. Linda Salekwa, aliahidi ushirikiano wa serikali katika kuhakikisha biashara hizo zinakua na kuchangia maendeleo ya uchumi pamoja na uhifadhi wa mazingira.

Biashara bunifu zinazofanya shughuli zake katika mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma na Lindi zimehimizwa kuwasilisha maombi ya ufadhili kupitia tovuti ya FUNGUO kabla ya Mei 31, 2026.

Programu ya FUNGUO inalenga kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini kwa kusaidia biashara changa, hususan zinazoongozwa na vijana na wanawake, kupata mitaji, ujuzi na masoko, na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi shirikishi na endelevu Tanzania.