******
Uongozi wa Kyela FM Radio umetoa taarifa kwa umma kuthibitisha kuwa wafanyakazi wake wawili, Tumsifu Katina na Emmy Eliud, wanaofanya kipindi cha bando la asubuhi, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watangazaji hao wamechukuliwa leo majira ya saa tisa alasiri katika ofisi za redio hiyo zilizopo Mtaa wa Mikoroshoni, Kyela Mjini, wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ya uandishi na utangazaji wa habari.
Uongozi wa kituo hicho umeeleza kuwa bado unaendelea kufuatilia kwa karibu tukio hilo ili kubaini sababu za kushikiliwa kwa wafanyakazi hao, huku ukifanya mawasiliano na Jeshi la Polisi Tanzania ili kupata ufafanuzi wa kina juu ya hatua hiyo.
Aidha, Kyela FM Radio imewataka wadau wake, wasikilizaji na umma kwa ujumla kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho suala hilo linaendelea kushughulikiwa, ikisisitiza kuwa taarifa zaidi zitatolewa pindi zitakapopatikana.
Uongozi umeongeza kuwa unaendelea kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha haki inatendeka na ukweli kuhusu tukio hilo unajulikana, huku ukiahidi kuendelea kulinda taaluma ya habari na maslahi ya wafanyakazi wake.