Wahimizwa kujitolea kusaidia upandikizaji uroto kwa watoto

Dodoma. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa imewahamasisha walimbwende wa Miss World Tanzania 2026 kuunga nao katika kuchangia gharama za matibabu ya upandikizaji uroto kwa watoto.

Ombi hilo limetolewa na Kaimu Mkurungenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Theophory Mbilinyi ambaye amesema kuwa gharama za chini kupatindikizaji wa uroto kwa mtoto moja katika hospitali hiyo ni Sh75 milioni ambapo wadau wanatakiwa kujitokeza kwenye harambee ya uchangiaji.

Warembo hao wa Miss World Tanzania 2026 wametembelea hospitali hiyo kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali zinazotolewa hospitalini hapo na hasa huduma za watoto.

“Kutokana na gharama hizo kuwa kubwa, hospitali imeona iandae harambee hiyo na nyinyi wenzetu tunaomba muungane nasi katika jambo hili jema kwa lengo la kusaidia afya za watu wetu,” amesema Mbilinyi.

Kwa mujibu wa Mbilinyi, hadi sasa hospitali hiyo wamefanya upandikizaji wa watoto 29 na wawili wapo wodini wakiendelea na maandalizi ya kuwafanyia matibabu watoto hao kwa matibabu yanayofanyika kwa ufadhili wa Serikali kutokana na wagonjwa kushindwa kumudu gharama za matibabu.

Amesema upandikizaji wa sasa bado wanatumia kutoa uloto kwa ndugu wa damu wa familia ya mgonjwa husika na mgonjwa hukaa siku 30 huku wataalamu wakiendelea na utafiti wa kusaidia matibabu kwa watu nje ya ndugu.

Kiongozi wa msafara huo, Mustafa Hassanali amesema jambo hilo ni jema na kwamba walimbwende hao na timu yao watashiriki kwenye harambee hiyo akiahidi kushiriki moja kwa moja siku ya tukio.

Amesema mazingira ya hospitali ya Benjamin Mkapa yamekaa vizuri na kuvutia wagonjwa ambao wanaweza kupata faraja wakifika kwenye mazingira hayo hata kabla ya kuanza kupata matibabu au watu wanaopeleka wagonjwa kupata sehemu ya utulivu.

Ameahidi kuwatumia warembo wa shindano la Miss World 2026 kutangaza vivutio vya utalii wa matibabu na hifadhi zilizopo nchini wakati wa mashindano hayo ndani na nje ya nchi.