Waliohukumiwa miaka 30 jela kwa kusafirisha heroini waachiwa

Arusha. Mahakama ya Rufani imewaachia huru watu wawili, Maria Mtumbuka na mkwe wake, Hamis Awadhi, waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa zaidi ya kilo 12.

Washtakiwa hao walikamatwa Aprili 2, 2021 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakiwa safarini kutoka Harare, Zimbabwe kuelekea Mumbai, nchini India.

Ilidaiwa kuwa katika hatua ya ukaguzi wa mizigo, kabla ya kupakiwa kwenye ndege, mifuko yao miwili ilibainika kuwa na vitu vya kutia shaka, ambavyo baada ya uchunguzi vilithibitishwa kuwa ni dawa za kulevya.

Uamuzi wa kuwaachia huru ulitolewa Aprili 10, 2026 na jopo la majaji watatu, Barke Sehel, Leila Mgonya na Khamis Shaaban.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Sehel alisisitiza kuwa mnyororo wa ulinzi wa ushahidi ni kipengele muhimu katika kesi za jinai, kwani huhakikisha vielelezo vinavyowasilishwa mahakamani ni vilevile vilivyokamatwa bila kuingiliwa au kubadilishwa.

Katika kesi ya msingi, Mahakama Kuu ilikuwa imewatia hatiani warufani hao wawili kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya, ambapo kila mmoja alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Ilidaiwa kuwa Maria alipatikana na hatia ya kusafirisha kilo 6.65 za heroini, huku Hamis akikutwa na kilo 6.75 za dawa hizo.

Shahidi wa nne, ambaye ni Ofisa Usalama wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), aliieleza mahakama kuwa siku ya tukio akiwa kazini katika mashine ya ukaguzi (scanner), alibaini mifuko miwili katika mizigo yao iliyokuwa na viashiria vya mashaka.

Alidai kuwa aliripoti kwa msimamizi wake wa zamu, ambaye naye aliwataarifu polisi.

Shahidi wa pili, ambaye ni Ofisa wa Polisi anayesimamia zamu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), alidai kupokea taarifa kwa njia ya simu kuhusu mifuko hiyo inayotiliwa shaka, kisha kuwaagiza maofisa polisi kwenda eneo hilo pamoja naye. Baadaye, Maria na Hamis waliitwa na kutambua mifuko hiyo kuwa ni sehemu ya mizigo yao.

Baada ya kukamatwa, vielelezo vilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi, ambapo ripoti ilithibitisha kuwa vilikuwa ni dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito uliotajwa.

Akijitetea mahakamani hapo, Maria alikiri kusafiri kutoka Zimbabwe kuelekea nchini India huku akikana kutenda kosa hilo na kudai safari yake ilikuwa kwa ajili ya kwenda kwenye matibabu.

Alidai alisafiri na mkwewe (Hamis) ambaye alipofika JNIA kulizuka ugomvi baina yake na maofisa uhamiaji ambao walitilia shaka uraia wake wa Tanzania, ambapo alipojaribu kuingilia kati walijikuta wakishtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya.

Hamis ambaye ni mfanyabiashara anayeuza rangi za magari mkoani Morogoro, alidai alikuwa akienda nchini India kwa ajili ya uchunguzi wa moyo na matibabu akiwa uwanjani hapo, ulitokea ugomvi na maofisa uhamiaji ambapo alipigwa na polisi na kulazimishwa kusaini nyaraka kadhaa huku akikana kukutwa na dawa hizo.

Katika rufaa hiyo warufani hao walikuwa na sababu tano za rufaa ikiwemo Mahakama ilikosea kuwatia hatiani na kuwahukumu huku mnyororo wa ulinzi wa vielelezo (chain of custody) ulivunjika, jambo lililofanya ushahidi huo kukosa uaminifu.

Walieleza kuwa haikuonyeshwa wazi ni nani aliyekuwa akihifadhi vielelezo hivyo katika hatua mbalimbali hadi vilipowasilishwa mahakamani.

Nyingine ni mahakama ilikosea kuwatia hatiani bila kuzingatia ushahidi wake, mahakama ilitegemea vielelezo vilivyoandaliwa kinyume cha sheria na kuwa kesi hiyo haikuthibitishwa bila kuacha shaka.

Upande wa Jamhuri ulipinga hoja hizo ukisisitiza kuwa ushahidi ulikuwa thabiti na tofauti ndogo zilizojitokeza hazikuathiri kiini cha kesi.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani ilikubaliana na hoja za warufani na kubaini kuwa kulikuwa na mapengo makubwa katika mnyororo wa ushahidi wa vielelezo muhimu vilivyotumika kuthibitisha shtaka hilo.

Katika uchambuzi wake, mahakama ilieleza kuwa haikubainika wazi ni nani aliyesafirisha vielelezo kutoka kwa mhifadhi hadi mahakamani wala jinsi vilivyofikishwa kwa shahidi wa aliyechunguza vielelezo hivyo.

Jaji Sehel amesema mnyororo wa ulinzi wa ushahidi ni muhimu sana katika kesi za jinai, kwani unahakikisha kuwa vielelezo vinavyowasilishwa mahakamani ni vilevile vilivyokamatwa bila kuingiliwa au kubadilishwa.

“Mapengo yasiyoelezeka katika mnyororo wa ulinzi yanaacha uwezekano mkubwa wa ushahidi kuingiliwa, hivyo kufanya isiwe salama kuutegemea katika kutoa hukumu ya hatia,” ilieleza mahakama katika uamuzi wake.

Mahakama ilieleza kuwa shahidi wa kwanza aliyewasilisha vielelezo hivyo mahakamani wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo alipohojiwa alidai hajui vimefikaje mahakamani huku shahidi wa tano akidai alimkabidhi shahidi wa pili.

Kutokana na dosari hizo, mahakama ilihitimisha kuwa haikuwa salama kisheria kuendelea kuamini kuwa vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani ndivyo vilivyokamatwa kwa warufani.

Kwa msingi huo, Mahakama ya Rufani iliamua kuruhusu rufaa, kufuta hukumu ya awali, na kuwaachia huru warufani hao mara moja isipokuwa kama wanashikiliwa kwa sababu nyingine za kisheria.

“Kwa kuwa msingi huu pekee wa rufaa unasuluhisha rufaa nzima, hatuoni haja ya kuendelea na misingi iliyobaki, mwishowe tunaruhusu rufaa, kufuta hukumu na kuamuru kuachiliwa huru kwa warufani isipokuwa kama wanashikiliwa kwa sababu nyingine za kisheria,” ilihitimisha Mahakama.