Katika kuendelea kuimarisha uwekezaji wa umma, Serikali imepanga kukamilisha Muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma katika mwaka wa fedha 2026/27, kama sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha utendaji wa taasisi na mashirika ya umma ili yaweze kujiendesha kwa tija, kuongeza mapato ya Serikali na kuchangia utekelezaji wa Dira 2050.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ameeleza kuwa Sh1.792 trilioni za bajeti yake zitakavyofanyia kazi mambo matano likiwemo la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Dira 2050 kwa mwaka 2026/27.
Profesa Mkumbo amesema Muswada huo unalenga kuweka mfumo mpya wa kisheria wa usimamizi wa uwekezaji wa umma, utakaosaidia kuongeza ufanisi, uwajibikaji na mchango wa mashirika ya umma katika uchumi wa Taifa.
Amefafanua kuwa, pamoja na mambo mengine, Muswada huo utapendekeza kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma itakayoratibu na kusimamia uwekezaji wa Serikali kupitia taasisi zake kwa mtazamo wa kitaifa.
Aidha, utapendekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma utakaosaidia upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya uwekezaji kupitia mashirika ya umma, bila kuhatarisha vyanzo vya msingi vya mapato vinavyoingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Katika eneo la uongozi na utawala, Muswada huo utaweka mfumo wa ushindani katika upatikanaji wa watendaji wakuu na wajumbe wa bodi za wakurugenzi za mashirika ya umma, hatua inayolenga kuongeza weledi, uwajibikaji na ufanisi katika uendeshaji wa taasisi hizo.
Pia, Serikali inalenga kuongeza uhuru wa kiutendaji kwa mashirika ya umma yanayofanya biashara, ili kuyawezesha kujiendesha kwa tija zaidi, kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali na kuimarisha ushindani katika sekta zake.
Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia jumla ya mashirika na kampuni 308 zikiwemo zile ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache zenye thamani ya uwekezaji ya Sh92.3 trilioni ambapo kati yake 91 ni mashirika ya kibiashara.
Hata hivyo, Profesa Mkumbo amesisitiza kuwa uhuru kwa mashirika hayo utaambatana na mifumo madhubuti ya upimaji utendaji ili kuhakikisha mashirika hayo yanabaki kuwajibika na kutoa matokeo yanayotarajiwa.
Katika mwaka wa fedha 2026/27, Serikali pia itaendelea na hatua ya tathimini kwa kina utendaji wa mashirika na taasisi za umma, ambapo itachukua hatua stahiki ikiwemo kuunganisha taasisi na mashirika yenye majukumu yanayofanana, kufuta yale ambayo malengo yake yamepitwa na wakati au majukumu yake yanaweza kutekelezwa na taasisi nyingine, pamoja na kuboresha yale yenye changamoto za kiutendaji.
Kufuatia tathimini ya utendaji na majukumu ya mashirika ya umma iliyofanyika mwaka 2023, Serikali ilielekeza kuunganishwa kwa mashirika ya umma 14 na kufutwa mengine matatu.
Hadi sasa, mashirika matatu yameshafutwa na mengine mawili yameunganishwa, ambapo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) ziliunganishwa na kuunda Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza).
Aidha, amesema kwa mwaka wa fedha 2026/27 Ofisi ya Msajili wa Hazina inatarajia kukusanya mapato yasiyo ya kodi ya Sh1.79 trilioni yatakayochangia Mfuko Mkuu wa Serikali, ikilinganishwa na lengo la Sh1.69 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Katika hatua nyingine, Ofisi hiyo imeendelea na ubinafsishaji wa viwanda sita vilivyorejeshwa serikalini ambavyo ni NMC Mzizima, NMC Isaka, CDA Integrated Industry Limited, Kilimanjaro Paddy, Moshi Pesticides na Unique Steel Rolling, ambapo taratibu za kisheria za kukamilisha mchakato huo zinaendelea ili kuhakikisha Serikali inanufaika ipasavyo na mali hizo.
Pia, imefanya uthamini wa mali mbalimbali zilizorejeshwa serikalini zikiwemo kiwanda cha Tembo Chipboards, mashamba ya maua ya Malalua, Kili Flora Chekereni na USA River Arusha, shamba la Basuto Manyara, mashamba ya Nafco West Kilimanjaro pamoja na shamba la KPL Mngeta Morogoro, hatua inayolenga kuvutia wawekezaji wenye tija katika maeneo hayo.
Profesa Mkumbo alisema Serikali itaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa uwekezaji wa umma pamoja na mageuzi ya kiutendaji ili kuongeza mchango wa mashirika katika uchumi wa Taifa, likiwamo lengo la kufikia asilimia nane ya mchango katika Pato la Taifa ifikapo 2050.