Dar es Salaam/Iringa. Wakati Ofisi ya Bunge ikitangaza nafasi tatu za wajumbe watakaoiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewaita wanachama wake kuwania mchakato huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Bunge leo, Ijumaa, Aprili 17, 2026, nafasi hizo tatu zitajazwa katika mkutano wa tatu unaoendelea jijini Dodoma.
Nafasi hizo zinajazwa baada ya waliokuwa wajumbe, Angela Kizigha, Ng’waru Maghembe na James Ole Millya kuteuliwa na kuchaguliwa kuwa wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa hiyo ya Bunge imefafanua kuwa katika nafasi hizo, mbili ni za kundi la wagombea wa Tanzania Bara na moja ni ya kundi la wanawake, ambapo zote zitapitia CCM.
“Aprili 30 saa 10 jioni ni uteuzi na Mei 4 saa tano asubuhi ni uchaguzi baada ya kipindi cha maswali,”
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Katibu wa Bunge, ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi huo, atatoa tangazo kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa masharti yanayohusu siku ya uteuzi na uchaguzi.
Katika tangazo hilo, Katibu wa Bunge atatoa masharti yanayopaswa kuzingatiwa na wagombea wa chama cha siasa chenye sifa ya kujaza nafasi za wajumbe ili kukiwezesha kuanza mchakato wa kuwapata wagombea kupitia chama hicho na majina yao yatawasilishwa bungeni kupigiwa kura.
“Kwa taarifa hii, watu ambao wanazo sifa za kugombea na kuchaguliwa kuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, kundi la wagombea Tanzania Bara na kundi la wagombea wanawake wanaweza kuanza mchakato wa kuteuliwa kushiriki katika uchaguzi kupitia CCM,”
“Chama au wagombea walioshinda katika ngazi ya chama wanapaswa kujaza fomu ya uteuzi kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza na kuiwasilisha kwa Katibu wa Bunge,” imeeleza.
CCM yafungua pazia uchukuaji fomu EALA
Katika hatua nyingine, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi amesema uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuomba uteuzi wa kuwania ubunge wa Afrika Mashariki utaanza Aprili 18 hadi Aprili 21 saa 10 jioni.
“Nafasi zilizopo wazi ni tatu zitakazojazwa na kundi la wabunge wanaotoka Tanzania Bara. Taratibu nyingine za kina zitafafanuliwa na Katibu wa Bunge. Fomu zinaweza kuchukuliwa Ofisi Ndogo Lumumba, Dar es Salaam au Makao Makuu ya CCM, Dodoma,” amesema Kihongosi.
Wakati huo huo, CCM Wilaya ya Iringa Vijijini kimetangaza rasmi kuanza kwa mchakato wa ndani wa kuwapata wanachama watakaowania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Isimani, baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Lukuvi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 16, 2026 na Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Sure Mwasanguti, wanachama wote wenye sifa wametakiwa kujitokeza kuchukua na kurejesha fomu za kuomba uteuzi kuanzia Aprili 17 hadi Aprili 18, 2026.
Amesema fomu zitatolewa kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni katika ofisi za chama wilayani humo, likiwa ni sehemu ya maandalizi ya kujaza nafasi hiyo kupitia taratibu za chama.