Necta: Itakuwa aibu mwanafunzi wa darasa la nne kutojua kusoma na kuandika

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limesema endapo juhudi za sasa zitaendelezwa ipasavyo, itakuwa ni aibu kubwa kuona mwanafunzi yeyote wa darasa la nne hajui kusoma na kuandika, kufuatia mafanikio ya mfumo mpya wa upimaji wa awali wa wanafunzi.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni jijini Dodoma na Katibu Mtendaji wa Necta, Profesa Said Mohamed wakati wa uwasilishaji wa taarifa kuhusu tathmini ya ujifunzaji ngazi ya elimu msingi.

Profesa Mohamed amesema hatua ya kuwapima wanafunzi wakiwa darasa la pili imeiwezesha Serikali kuwatambua mapema wale wenye changamoto za kusoma na kuandika na kuanza kuwachukulia hatua stahiki.

Amesema wanafunzi waliopimwa mwaka 2025, ambao sasa wako darasa la tatu, tayari wanajulikana uwezo wao, hivyo hakuna sababu ya kuwa na mwanafunzi asiyejua kusoma na kuandika anapofika darasa la nne.

Kwa mara ya kwanza mwaka 2025 baraza liliendesha upimaji wa kitaifa wa darasa la pili kwa ngazi ya shule, shule 20,865 zilishiriki wanafunzi wakiwa 1,788, 045 ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 89.9 na ubora wa ufaulu ulkuwa asilimia 75.6.

“Hii maana yake sasa hivi tunafahamu watoto wote ambao hawajui kusoma na kuandika waliofika darasa la pili, hivyo hatutakuwa tunasubiri kumtambua mtoto asiyejua kusoma na kuandika akiwa darasa la nne. Taarifa hizi tunazo kitaifa, kimkoa, halmashauri na ngazi ya shule, amesema na kuongeza

“Ukiangalia hiyo takwimu ya ufaulu utaona asilimia 10.1 ya waolipimwa hawajui kusoma na kuandika, hivyo tuna jukumu la kufanya ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha wanapewa programu za ziada za kutosha ili kuhakikisha waweze kupata umahiri wa kusoma na kuandika kabla ya kufika darasa la nne.

“Kwa hiki tulichokifanya mwaka jana ambao mwaka huu wako darasa la tatu, kama kazi itafanyika kwelikweli mwakani itakuwa aibu kubwa tukiwa na namba yeyote ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika,” amesema Profesa Mohamed.

Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa na Katibu Mtendaji huyo, idadi ya wanafunzi wasioweza kusoma na kuandika imeendelea kupungua kwa kasi katika miaka ya karibuni, ikitoka wanafunzi 25,841 mwaka 2022 hadi 15,616 mwaka 2023, kisha 8,960 mwaka 2024 na kufikia 5,847 mwaka 2025.

“Kumekuwa na maboresho makubwa na tunashuhudia idadi ya wanafunzi wanaofika darasa la nne wakiwa hawana umahiri wa kusoma na kuandika inapungua  mwaka hadi mwaka, huko nyuma ilikuwa ikisemwa kwamba huenda mwanafunzi akapenya hadi darasa la saba akiwa hajui kusoma na kuandika,”

Hivi karibuni Shirika la Uwezo Tanzania liliwasilisha matokeo ya utafiti wake uliofanyika mwaka 2025 ukionesha asilimia 65.5 ya wanafunzi wenye umri wa miaka sita hadi 16 hawana umahiri wa kusoma na kufanya hesabu rahisi.

Utafiti huo uliofanyika nchi nzima umehusisha watoto wa umri huo walio shuleni na wale walio nje ya shule huku mikoa ya Rukwa, Simiyu, Manyara, Morogoro, Kigoma, Tabora, Lindi, Shinyanga Mtwara na Songwe ikiwa na hali mbaya zaidi.

Wakizungumza na Mwananchi wadau wa elimu wamesema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna haja ya kuongeza nguvu katika utekelezaji ili kuhakikisha changamoto hiyo inaondolewa kabisa.

Mhadhiri wa elimu, Dk Asha Mrema, amesema pamoja na utambuzi wa mapema, bado kuna umuhimu wa kuwekeza katika mafunzo endelevu ya walimu wa madarasa ya awali.

“Walimu wanapaswa kupewa mbinu bunifu za kufundisha kusoma na kuandika, hasa kwa kutumia njia shirikishi zinazomfanya mtoto ajifunze kwa urahisi,” amesema Dk Mrema.

Mtaalamu wa elimu ya msingi, Josephat Mlay, ameweka mkazi kwenye ushiriki wa wazazi akieleza kuwa  bila mazingira rafiki ya kujifunzia nyumbani, jitihada za shule pekee hazitoshi.

“Mzazi anatakiwa kufuatilia maendeleo ya mtoto wake kila siku, kumtia moyo kusoma na kuhakikisha anapata muda wa kujifunza hata akiwa nyumbani,” amesema Mlay.

Kwa upande wake, mwalimu wa shule ya msingi Kitangwi wilayani Mkuranga, Rehema Nchimbi, amesema wakati mwingine inakuwa vigumu kwa watoto wote darasani kujua kusoma na kuandika kutokana na changamoto ya  msongamano wa wanafunzi darasani na uhaba wa vifaa vya kufundishia.

“Ni vigumu kumsaidia kila mwanafunzi kwa ufanisi darasa linapokuwa na wanafunzi wengi sana. Hii inahitaji uwekezaji zaidi katika miundombinu na rasilimali za elimu,” amesema mwalimu huyo.

Akizungumzia hilo mtafiti wa masuala ya elimu, Dk John Kessy, ameshauri kuanzishwa kwa mifumo ya tathmini endelevu shuleni badala ya kutegemea vipimo vya mara moja pekee.

“Ni muhimu kufuatilia maendeleo ya mtoto mara kwa mara ili kubaini changamoto mapema na kuchukua hatua kwa wakati,” amesema Dk Kessy.

Naye mratibu wa shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na elimu, Neema Lwoga, amesisitiza umuhimu wa kuongeza programu za usomaji shuleni na jamii, ikiwemo klabu za kusoma na maktaba za jamii.

“Watoto wanahitaji mazingira yanayochochea utamaduni wa kusoma, si darasani tu bali hata katika jamii wanamoishi,” amesema.

Neema ameongeza pia kuna umuhimu wa kutumia teknolojia katika kufundisha, hasa kupitia vifaa vya kidijitali vinavyorahisisha ujifunzaji kwa watoto wa kizazi cha sasa.

“Matumizi ya Tehama yanaweza kusaidia kuwafikia wanafunzi wengi zaidi kwa wakati mmoja na kwa njia rahisi kueleweka,” amesema Neema.