Maswa. Wananchi zaidi ya 12,000 wa vijiji vya Mwabayanda ‘S’ na Mwasita, wilayani Maswa mkoani Simiyu, wanatarajia kunufaika na mradi mkubwa wa maji safi na salama unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh2.1 bilioni chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (Mauwasa).
Mradi huo unahusisha ujenzi wa tenki la kuhifadhi na kusambaza maji kwenye mnara wa urefu wa mita 12, lenye uwezo wa kuhifadhi lita 200,000 pamoja na ulazaji wa bomba kwa umbali wa kilomita 17.
Pia utajumuisha ujenzi wa vituo 10 vya kuchotea maji, ambapo kila kijiji kitapata vituo vitano.
Akizungumza leo Aprili 18, 2026 kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi wa Mauwasa, Juvenary Paschal amesema kuwa kazi hiyo itafanywa na mkandarasi Zhongii Contractor Ltd na inalenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa maeneo hayo.
Amesema ni muhimu kwa wananchi kujiandaa kuvuta huduma ya maji hadi majumbani mwao pindi mradi huo utakapokamilika Mei 2027 ili kuongeza ufanisi na urahisi wa matumizi ya huduma hiyo.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mwasita, wilayani Maswa, waliohudhuria mkutano wa hadhara kuhusu ujenzi wa mradi wa maji kijijini hapo. Picha na Samwel Mwanga.
Kwa upande wake, Ofisa maendeleo ya jamii wa Mauwasa, Quen Mlagala amesema kuwa manufaa yatakayopatikana mara baada ya mradi huo kukamilika ni pamoja na kupunguza magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.
“Tutaongeza muda wa upatikanaji wa maji katika maeneo ya vijiji hivi kutoka siku tatu hadi siku saba kwa wiki ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji ya uhakika,” amesema.
Diwani wa Kata ya Ngwighwa, Stephen Dwese, ameishukuru Serikali kwa kupeleka mradi huo, akieleza kuwa utasaidia kumaliza changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa maji katika vijiji hivyo.
“Mradi huu ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wetu. Kwa muda mrefu tumekuwa tukikabiliwa na uhaba wa maji, lakini sasa tuna matumaini ya kupata huduma ya uhakika,” amesema.
Paulina Petro, mkazi wa kijiji cha Mwasita, amesema kuwa mradi huo utawarahisishia maisha yao na kupunguza adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
“Maji yakipatikana kwa urahisi katika mazingira yetu tutapata muda wa kufanya shughuli zetu za uzalishaji mali, hasa sisi wanawake ambao ndiyo tuna jukumu la kuyatafuta maji,” amesema.
Naye Zacharia Bufumbe, mkazi wa kijiji hicho, amesema kuwa mradi huo unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya ya kijamii na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuboresha afya za wananchi na kuongeza muda wa kushiriki shughuli za maendeleo badala ya kutafuta maji.