Dar es Salaam. Baadhi ya wachambuzi wa siasa wametaja sababu tatu za mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu kubanwa na wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wakati akichangia hoja za bajeti za ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora).
Kwa mujibu wachambuzi hao, wingi wa wabunge wa CCM, masilahi ya Serikali, chama pamoja na kuepuka hoja zinazoibua mjadala, ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha Ado kukatizwa katizwa hotuba yake.
Mara ya kwanza Ado ambaye ni mbunge wa ACT- Wazalendo, alibanwa baada ya kugusa hoja ya Katiba mpya Aprili 13, 2026 wakati akichangia makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya Sh12.5 trilioni akisema haijapewa uzito katika bajeti hiyo.
Hali hiyo ya mvutano ilijitokeza tena Aprili 17, 2026 wakati alipogusia suala la watu kupotea na kutekwa wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora).
Tukio au changamoto anayoipitia Ado bungeni imeshawahi kuwatokea kina Zitto Kabwe, Tundu Lissu (Mwenyekiti wa Chadema), John Mnyika, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ Halima Mdee na John Heche (Makamu mwenyekiti wa Chadema, bara) wakati wakiwemo wabunge kwa nyakati tofauti.
Wachambuzi hao wametoa sababu hizo leo Jumamosi Aprili 18, 2026 wakati wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti.
Kati yao wapo waliosema kama upinzani, wanataka Katiba mpya basi wanatakiwa kuimarisha demokrasia katika vyama vyao.
Mchambuzi wa siasa, Rainery Songea amesema wabunge wa CCM miongoni mwa kazi yao ni kutetea masilahi ya chama hicho, hivyo zinapoibuka hoja za namna hiyo zinaanzisha mvutano.
“Hoja yoyote inayoleta au kuibua mjadala mara nyingi CCM hawapendi iendelee kujadiliwa,” amesema Songea.
Hata hivyo, Songea ana matumiani kuwa awamu ya pili ya Rais Samia Suluhu Hassan mchakato wa Katiba mpya utafanyika kutokana na mazingira ya siasa yaliyopo.
“Suala la Ado la kukatizwa wakati akichangia hotuba yake ni jambo la kawaida ili wamtoe kwenye reli. Unajua kuna mambo kama Taifa, hatupendi kabisa kuyajadili, kuna hoja fulani za…hazitakiwa kujadiliwa,” ameeleza Songea.
Songea ameeleza kuwa, sehemu pekee Ado kuzungumzia hoja hizo ni bungeni ambako ana kinga, ndiyo maana amekumbana na mvutano kutoka kwa wabunge wa CCM na Serikali.
Dk Onesmo Kyauke amesema Bunge likishakuwa na wingi wa wabunge wa chama tawala, hali hiyo lazima ijitokeze ukilinganisha wapinzani wapo wachache.
“Sio hapa tu, hata mabunge mengine duniani kwa sababu Bunge ni chombo cha kisiasa pia. Mkiwa wachache sana wale walio wengi wanatumia nafasi, kwa sababu Spika ni wa kwao na wenyeviti wa kwao pia.
“Hivyo, wakiona hoja inayolenga kuharibu taswira ya chama chao, lazima wata…Ingawa ni kawaida ya mabunge, lakini waliowa chache wanatakiwa kupewa nafasi ya kuwasilisha hoja zao bila kusumbuliwa.”
“Hata hivyo, siku zote wapinzani hawawezi kuzungumza mambo ya kuisifia Serikali, pamoja na udogo wao haki ya kuzungumza inatakiwa izingatiwe, hata kama hana namba kuipitisha hiyo hoja,” ameeleza Dk Kyauke.
Mchambuzi Seif Nassor alikuwa na maoni tofauti na wenzake akidai baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani si wakweli, akisema wapo wanaoishinikiza Serikali kuanzisha mchakato wa Katiba mpya, lakini vyama vyao hakuna demokrasia ya kweli.
“Ukweli wa mambo ukiangalia katika vyama vyote vya upinzani demokrasia ya kweli haipo, ndio maana kuna wengine wanang’ang’ania kuwa viongozi kwa muda mrefu,” amedai Nassor.
Nassor amesisitiza uchaguzi wa haki ndani ya vyama vya upinzani ili kupata uhalali wa kudai Katiba mpya au kuongoza Serikali.
Ameeleza kuwa, si sahihi kuilaumu Serikali kuhusu Katiba mpya bali wanapaswa kuimarisha demokrasia kwanza katika vyama vyao ikiwamo kurekebisha Katiba zao.
Juzi akichangia mjadala wa Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Ado alijikutana akivutana na wabunge wa CCM, hali inayotafsiriwa kupunguza makali ya hoja zake.
Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, mbunge anaruhusiwa kuomba taarifa akiwa amesimama na kupatiwa; hata hivyo, muda wa majadiliano ya mbunge anayechangia hujumuisha pia muda wa wale wanaoomba taarifa.
Katika mchango wake, Ado amejikuta mara kadhaa akikatizwa kutokana na maombi ya taarifa kutoka kwa wabunge wa CCM, akiwamo wa Kaliua pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi.
Kwenye mjadala huo, Ado ametoa tuhuma kuhusu utekaji wa watu na vitendo vya ufisadi nchini.
Ameeleza kutokuwa na imani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), akidai kuwa licha ya kuwepo kwa upotevu mkubwa wa fedha za umma, taasisi hiyo haijaonesha nguvu ya kutosha katika kupambana na rushwa.
Ado amesisitiza kuwa hoja yake inatokana na wajibu wake wa kupinga rushwa, akirejea ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinazoonesha kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma.
Ametolea mfano uchambuzi wa chama chake katika ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha 2023/24, unaoonesha kuwa Sh2.5 trilioni zilipotea kutokana na ubadhirifu, huku Takukuru ikiokoa Sh14 bilioni pekee.
Mbunge wa Kaliua, Joseph Tama alimpa taarifa akidai hoja yake haina msingi kwa kuwa Waziri ameeleza juhudi za Takukuru katika kitabu chake. Hata hivyo, Ado alikataa taarifa hiyo.
Haikuishia kwa Ado ambaye ni Katibu Mkuu wa ACT -Wazalendo, bali aligusia utekaji, akidai kuwa bado kuna watu wanatekwa na kupotea bila hatua madhubuti za Serikali na kupendekeza kuundwa kwa Tume Huru ya Kijaji kuchunguza matukio hayo.
Hoja hiyo ilizua mjadala mkali, wabunge wengi waliomba kutoa taarifa, lakini mwenyekiti alimpa nafasi Waziri Katambi aliyesema kuna uchunguzi na kesi mbalimbali za jinai zinaendelea kuhusu matukio ya utekaji na kudai kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakijiteka wenyewe.
Hata hivyo, Ado hakukubaliana na maelezo hayo, akisisitiza kuwa, anachodai ni uchunguzi huru kupitia Tume ya Kijaji, badala ya uchunguzi wa kawaida wa kipolisi.
Sio bajeti hiyo tu pekee, bali hata Ofisi ya Waziri Mkuu, Ado alijikuta akibanwa na wabunge wa CCM, hali iliyosababisha kukwama kwama kwa mara kadhaa kutowasilisha mchango wake kwa ufanisi.
Kilichofanya wabunge wa CCM kuanza kusimama na kumbana Ado ni baada ya mbunge huyo, alipogusia suala la Katiba mpya akisema hajaona likitiliwa mkazo kwenye hotuba ya Waziri Mkuu.
Hoja hiyo iliwagusa wabunge wa kadhaa wa CCM akiwamo Ester Bulaya (Bunda Mjini) na Timotheo Mzava (Korogwe Vijijini), kila mmoja aliposimama alionesha kutokubaliana na maelezo ya Ado, kwa kuwa jambo hilo lipo kwenye Ilani ya CCM 2025/30.
Lakini, katika mchango wake, Ado amesema haoni nia njema ya Serikali katika utungwaji wa Katiba mpya kwa kuwa, jambo hilo halikuzungumzwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu licha ya kuwa ilikuwa ni ahadi ya Serikali.
“Mheshimiwa mwenyekiti, sioni nia njema ya Serikali katika hili, ikumbukwe suala la Katiba mpya siyo takwa la CCM wala Serikali pekee, ni dai la Watanzania, sioni mahali popote kwenye hotuba ya Waziri Mkuu ambapo imezungumzwa kuhusu Katiba mpya,” amesema Shaibu.
Hatua hiyo ilifanya Bulaya kusimama kwa mujibu wa kanuni za kibunge kuomba ampe taarifa mzungumzaji na alimweleza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia ina nia njema na kwamba jambo hilo litakuja kwa wakati wake.
