Papa atua Angola mzimu wa Trump ukimfuata

Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo wa XIV amewasili nchini Angola tayari kuanza ziara yake ya kitume kuanzia Aprili 18 hadi 21, 2026 ikiwa ni nchi ya tatu tangu aanze ziara hiyo barani Afrika.

Akizungumza na waandishi habari kabla ya kuanza safari yake ya Angola, Pape Leo XIV amesema anajutia matamshi yake ya kupinga vita duniani, kuchukuliwa kama ugomvi wa maneno na Rais wa Marekani, Donald Trump.

Hata hivyo, kwa mujibu wa DW, Papa ambaye ni kiongozi wa kwanza wa Kanisa hilo kutoka nchini Marekani amesema hana muda wa kugombana na Rais huyo huku akizidi kusisitiza amani.

Ikumbukwe hivi karibuni, Rais Trump na Papa waliingia katika mzozo usio wa kawaida kuhusu msimamo wa Vatican dhidi ya vita vinavyoendelea kati ya Marekani, Israel dhidi ya Iran na Mashariki ya Kati.

Mzozo huo ulizidi pale Trump alipomshambulia Papa katika chapisho refu kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, akisema ni “Dhaifu kupambana na uhalifu, na haelewi sera za kigeni. Sitaki Papa anayefikiri ni sawa kwa Iran kuwa na silaha za nyuklia.”

“Sitaki Papa anayefikiri ni jambo baya Marekani kuishambulia Venezuela, nchi ambayo ilikuwa ikituma kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kwenda Marekani na mbaya zaidi, imekuwa ikawaachilia wahalifu kutoka magerezani (ili kuwatuma) nchini mwetu, wakiwemo wauaji, wafanyabiashara wa dawa za kulevya, na wahalifu,” aliongeza.

Kwa upande wake, Papa alisema hana hofu yoyote na Rais Trump, kufuatia mashambulizi hayo ya maneno huku akikisisitiza umuhimu wa amani na mazungumzo, huku akilaani matamshi ya kisiasa yanayochochea migogoro.

Papa huyo amekuwa mkosoaji wa vita dhidi ya Iran, akieleza vitisho vya Trump vya kuangamiza ustaarabu wa Iran ni visivyokubalika na kumtaka atafute njia ya kupunguza mvutano huo.

Kwa kawaida, ni nadra kwa Papa kujibu moja kwa moja kauli za viongozi wa kisiasa, jambo linalofanya mvutano huu kuwa wa kipekee.

Papa Leo anasisitiza jukumu lake si la kisiasa bali la kiroho, akilenga kulinda utu wa binadamu na kuhimiza suluhu za amani akisema watu wengi wanateseka duniani kuna njia bora ya kushughulikia migogoro kuliko vita.

Papa huyo pia amewahi kukosoa sera kali za uhamiaji za Trump, akihoji kama mtu anaweza kujiita mtetezi wa uhai huku akiunga mkono kile alichokiita unyanyasaji wa wahamiaji.

Papa anatarajiwa kukaa Angola kwa siku tatu kabla ya kuelekea katika kituo chake cha nne na cha mwisho cha ziara hiyo, ambacho ni Equatorial Guinea.

Akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Luanda, Papa alipokewa na Rais João Lourenço ambapo amelakiwa na watoto wawili waliomkabidhi maua kama ishara ya ukaribisho.

Katika ratiba yake ya leo Jumapili, Aprili 19,2026 Papa ataongoza Ibada ya Misa Takatifu katika eneo la Kilamba, kisha atasafiri kuelekea katika Madhabahu ya Muxima ambako ataongoza Rozari na kusali pamoja na waumini.

Kesho Jumatatu, atasafiri kwenda Saurimo, ambako atatembelea wazee na kuongoza ibada ya misa, kabla ya kurejea Luanda, na hivyo kuhitimisha ziara yake nchini Angola, kwa mujibu wa Vatican News.

Angola inakadiriwa kuwa na waumini milioni 15 wa Kikatoliki ikiwa ni takriban asilimia 44 ya idadi ya watu nchini humo.