Simiyu. Katika ukanda wa Ziwa unaojulikana kwa shughuli za kilimo na ufugaji, Mkoa wa Simiyu unakabiliwa na tishio linalokua kwa kasi la ukataji miti holela, hali inayoendelea kuathiri mazingira, vyanzo vya maji na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Mwananchi Digital imetembelea maeneo mbalimbali ya Wilaya za Maswa, Bariadi, Meatu na Itilima imebaini kuwa kasi ya ukataji miti imeongezeka kutokana na mahitaji ya kuni, mkaa, upanuzi wa mashamba na ujenzi.
Katika baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Meatu, maeneo yaliyokuwa na misitu miaka michache iliyopita sasa yamebaki wazi, yakiwa na mashamba au ardhi kavu isiyo na uoto wa asili.
Mkazi wa kijiji cha Longalonigha, Jisena Dagadaga amesema kuwa kwa sasa misitu inatoweka kutokana na kukithiri kwa shughuli za kibinadamu.
Sehemu ya Msitu katika kijiji cha Nanga wilaya ya Itilima ambapo miti inakatwa kwa ajili ya matumizi ya shughuli za kibinadamu. Picha na Samwel Mwanga
“Tulikuwa na miti mingi sana hapa, lakini sasa imekatwa kwa ajili ya mkaa na mashamba. Hata mvua imekuwa haitabiriki,” amesema.
Kwa upande wake mfanyabiashara wa mkaa kijiji cha Isaghenge wilayani Maswa, Mathias Nghamba amekiri kuwa biashara hiyo imekuwa chanzo kikuu cha kipato licha ya athari zake kwa mazingira.
“Hii ndiyo kazi inayotulisha. Bila mkaa hatuna njia nyingine ya kipato,” amesema.
Mkulima wa kijiji cha Nanga wilayani Meatu, Maliganya Cherahani amesema kuwa mavuno yamepungua kutokana na mabadiliko ya mvua.
Eneo la msitu wa Mwanghui ambao kuna chanzo cha maji katika wilaya ya Maswa kikiwa kimevamiwa na watu ambao wanachana mbao. Picha na Samwel Mwanga
“Mvua haiji kama zamani. Ardhi imekuwa ngumu na mazao hayafanyi vizuri na pia kwa mifugo kuna upungufu wa malisho na maji kwa mifugo,” amesema.
Hata hivyo Wakala wa Misitu nchini (TFS) Mkoa wa Simiyu, Fabian Mosha amesema kuwa ukataji miti holela unasababisha madhara makubwa yakiwemo kupungua kwa mvua na mabadiliko ya tabianchi, kukauka kwa vyanzo vya maji, kuongezeka kwa jangwa na kupotea kwa viumbe hai.
Amesema kuwa miti ina jukumu muhimu katika kuhifadhi unyevunyevu wa udongo na kusawazisha hali ya hewa.
“Miti inapokatwa kwa kiwango kikubwa bila kupandwa mingine, mazingira yanaharibika na athari zake huonekana kwa muda mfupi na mrefu,” amesema.
Kwa upande wake, Dutu Lubinza Ofisa Mazingira Wilaya ya Maswa amesema kuwa hatua zinaendelea kuchukuliwa kudhibiti ukataji miti holela.
“Tunatoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na kupanda miti. Pia tunachukua hatua kwa wanaokata miti bila vibali,” amesema.
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano akiwa anapanda miti katika eneo la jengo jipya la halmashauri ya wilaya hiyo lililopo eneo la Nghami. Picha na Samwel Mwanga
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano amesema kuwa licha ya wilaya hicho kupanda miti lakini wanasisitiza itunzwe na kuhakikisha taasisi zote za Serikali zinapanda miti ili kuweza kufikia malengo ya kupanda miti milioni moja na nusu kwa mwaka.
Amesema kuwa Serikali imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kama majiko banifu ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
“Suluhisho la kudumu la utunzaji wa misitu yetu linahitaji ushirikiano wa wadau wote, kuanzia wananchi hadi Serikali pamoja na kuimarisha kampeni za upandaji miti, kutoa elimu ya mazingira kwa jamii, kuweka udhibiti mkali wa ukataji miti na kukuza matumizi ya nishati mbadala,” amesema.
