Global Publishers
April 19, 2026
0 Comments
Waziri Ulega akiongoza Harambee kuchangia ujenzi wa shule na Zahanati Kijiji cha Musati
Waziri wa Ujenzi, Abdalah Ulega ameongoza harambee iliyokusanya jumla ya sh.bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na shule katika kijiji cha Musati wilayani Serengeti mkoani Mara.
Harambee hiyo imefanyika jumamosi Aprili 18, 2026 kijijini Musati na imeandaliwa na Taasisi ya Nyansaho Nyansaho Foundation ambayo Mwanzilishi na Mwenyekiti wake ni Dk. Rhimo Nyansaho ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Akizungumza katika harambee hiyo, Ulega amempongeza Dk. Rhimo Nyansaho, kwa juhudi zake za kuwaletea maendeleo watanzania wakiwemo wananchi wa Serengeti na mkoa mzima wa Mara.
“Wana Mara hongereni sana kwa kuwa na Dk. Nyansaho, kazi anazofanya ni kubwa na za kupigiwa mfano. Watu wa Mara mnaye mtu wa kujivunia,” amesema Ulega katika harambee hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania George Masaju; Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob Mkunda; na Dk. David Mpwani, Askofu Kanisa la Waadventista Wasabato, Mara Kaskazini na viongozi wengine.
Katika harambee hiyo, Waziri Ulega pamoja na marafiki zake walichangia Sh.milioni 100 na kuongoza uchangiaji kutoka kwa wafanyabiashara, taasisi za fedha, wageni waalikwa na wananchi wa kawaida ambao kwa ujumla walichangia Sh.bilioni 1.4.
Hafla hiyo ya harambee ilitanguliwa na uzinduzi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato – Musati Central na nyumba ya mchungaji vilivyopo katika kijiji cha Musati, wilayani Serengeti mkoani Mara ambavyo kanisa na nyumba hiyo vimejengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Nyansaho kwa thamani ya Sh.milioni 500.
Kwa upande wake, Mwenyekiti na Muanzilishi wa Taasisi ya Nyansaho, Dk. Rhimo Nyasanho amesema uamuzi wa taasisi hiyo ambayo imejikiti katika kusaidia miradi ya kijamii kama vile elimu na afya imedhamiria kujenga shule na zahanati kwa lengo la kutoa huduma bora za afya na elimu kwa wananchi.
Amesema baada ya kujenga kanisa, sasa nguvu za Taasisi ya Nyansaho, inaelekezwa kujenga zahanati na shule ambavyo vyote kwa pamoja vitatoa huduma kwa watu wote bila kujali dini zao.
“Tunawashukuru sana kwa michango hii, lengo letu ni kujenga shule kuanzia nursery (chekechea) hadi kidato cha sita ili vijana wetu wote, bila kujali dini zao, wapate elimu na huduma za afya kutoka katika shule na zahanati hiyo,” amesema Dk. Nyansaho.