Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema wizara yake imejipanga kutekeleza vipaumbele vinne katika mwaka wa fedha 2026/27, vikilenga kuwawezesha vijana kiuchumi, kijamii na kisera.
Katika utekelezwaji wa vipaumbele hivyo, Nanauka ameliomba Bunge limuidhinishie zaidi ya Sh35.9 bilioni. Kati ya hizo zaidi ya Sh30.1 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh5.85 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Nanauka amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo, Jumatatu Aprili 20, 2026 wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Amesema mpango wa wizara yake utajikita katika kuimarisha ukuzaji wa biashara na uwezeshaji wa vijana kiuchumi, hatua inayolenga kuongeza idadi ya vijana wanaojiajiri na kuajiriwa katika sekta za uzalishaji na biashara.
“Hii inahusisha utoaji wa mikopo nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, mafunzo ya ujasiriamali na uanzishwaji wa vituo vya ubunifu vitakavyowaunganisha vijana na masoko, mitaji na teknolojia,” amesema.
Kipaumbele kingine, amesema ni kuimarisha uratibu na ushirikishaji wa vijana katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Katika eneo hilo, Nanauka amesema wizara imepanga kuandaa mfumo wa Taifa wa uratibu wa masuala ya vijana, kuanzisha kanzidata ya kitaifa ya taarifa za vijana na kupitia Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa ili kupanua wigo wa ushiriki wao katika maamuzi.
Amekitaja kipaumbele kingine ni kuweka mkazo katika kuimarisha elimu ya uraia, uzalendo na uratibu wa Mwenge wa Uhuru, ikiwa ni pamoja na kuratibu majukwaa ya vijana katika halmashauri mbalimbali.
Nanauka amesema kipaumbele kingine ni kuimarisha ustawi na makuzi ya vijana kupitia programu za stadi za maisha, msaada wa kisaikolojia na afua zinazolenga kujenga kizazi chenye uwezo wa kufanya uamuzi sahihi na kukabiliana na changamoto.
Katika hotuba yake hiyo, amesema fedha za maendeleo zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo utoaji wa mikopo kwa vijana, ukarabati wa vituo vya mafunzo ya vijana vya Sasanda, Ilonga na Marangu na kuanzisha mifumo ya kidijitali ya kuwawezesha vijana kupata fursa za kiuchumi.
