SGR yahusishwa na mafuriko Morogoro, Serikali yajibu

Morogoro. Serikali imesema inachukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto ya mafuriko katika baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Morogoro, ikiwamo kata za Kihonda na Lukobe.

Pia ameahidi kuboresha miundombinu ya vivuko ili kurahisisha usafiri wa wananchi.

Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma leo, Jumatatu, Aprili 20, 2026, na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mkoa wa Morogoro, Sheila Lukuba.

Katika swali lake, Lukuba ameeleza kuwa kata za Kihonda na Lukobe hazikuwa zikikumbwa na mafuriko hapo awali, lakini hali imebadilika kufuatia ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ambao kwa kiasi kikubwa umechangia kuziba au kubadili mifumo ya asili ya mtiririko wa maji.

Amesema mafuriko hayo yamekuwa yakisababisha madhara makubwa kwa wananchi, ikiwamo kuharibika kwa mali na kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi katika maeneo ya Wagogo, Azimio na Makorongoni.

“Je, ni lini Serikali itajenga miundombinu imara ya kudhibiti mafuriko haya ili kunusuru maisha na mali za wananchi?” amehoji Lukuba.

Akijibu swali hilo, Dk Dugange amesema Serikali imetambua uwepo wa tatizo hilo na imechukua hatua ya awali kwa kutuma timu ya wataalamu kufanya tathmini ya kina katika maeneo yaliyoathirika.

“Tumeshatuma wataalamu ambao wanafanya tathmini kubaini maeneo yanayohitaji miundombinu, aina ya miundombinu inayotakiwa pamoja na gharama husika. Baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kudhibiti na kuelekeza maji katika Mto Ngerengere,” amesema.

Amesisitiza kuwa lengo la hatua hiyo ni kupunguza athari za mafuriko na kurejesha hali ya usalama kwa wakazi wa maeneo hayo.

Mbali na changamoto ya mafuriko, mbunge huyo pia ameibua suala la ukosefu wa vivuko salama katika baadhi ya maeneo ya mji huo, akitaja eneo la Tushikamane karibu na Shule ya Sekondari Mji Mpya pamoja na mtaa wa Kambitano, uliopo mpakani mwa Wilaya ya Mvomero na Manispaa ya Morogoro.

Akijibu hoja hiyo, Dk Dugange amekiri kuwepo kwa changamoto ya vivuko na kueleza kuwa Serikali ina mpango wa kujenga miundombinu hiyo sambamba na utekelezaji wa miradi ya kudhibiti mafuriko.

“Tunafahamu kuwa kuna uhitaji wa vivuko katika maeneo hayo. Wakati wa utekelezaji wa mradi wa mifereji ya maji, Serikali itaandaa kifurushi (package) kitakachojumuisha pia ujenzi wa vivuko katika maeneo ya Tushikamane na Kambitano,” amesema.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuboresha mawasiliano ya wananchi na kupunguza adha wanazokumbana nazo wakati wa mvua, hususan kukatika kwa njia za usafiri.

Katika swali la msingi, Lukuba ameuliza ni lini Serikali itajenga mfereji mkubwa wa kuelekeza maji katika Mto Ngerengere ili kunusuru wakazi wa kata za Kihonda na Lukobe ambao wamekuwa wakikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara nyakati za mvua.

Akijibu swali hilo, Dk Dugange amesema kata hizo zimeendelea kuathiriwa na mafuriko, na kwamba Serikali imepanga kujenga mfereji wa kuyaelekeza maji katika Mto Ngerengere kama suluhisho la kudumu. Ameeleza kuwa tayari timu ya wataalamu imeundwa kufanya tathmini na kuandaa andiko la mradi litakaloainisha mahitaji halisi pamoja na mbinu sahihi ya utekelezaji.

Ameongeza kuwa kazi ya tathmini inatarajiwa kukamilika kabla au ifikapo Septemba 2026, hatua itakayofungua njia kwa utekelezaji wa mradi huo.

Serikali imewataka wananchi kuendelea kuwa na subira wakati taratibu za tathmini na upangaji wa bajeti zikiendelea, huku ikiahidi kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto hizo.