SAMIA AAGIZA MAGEUZI KUWAINUA MAMA NA BABA LISHE.

Na Karama Kenyunko – Michuzi Tv.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amezielekeza wizara tano muhimu kuchukua hatua za haraka kuimarisha ustawi wa mama na baba lishe, akiwatambua kama mhimili muhimu wa uchumi.

Akizungumza leo Aprili 21, 2026 katika Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba lishe lililofanyika Dar es Salaam, Rais almeagiza Wizara za Fedha, Afya, Nishati, Maendeleo ya Jamii (Wanawake, Jinsia, Wazee na Makundi Maalum), pamoja na Habari na TEHAMA, na Ofisi ya Waziri Mkuu–Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kushirikiana kuboresha mazingira ya kazi, heshima na ulinzi kwa wafanyabiashara hao.

Ameisema mama na baba lishe ni nguzo muhimu ya ajira na uchumi wa maeneo ya mijini na vijijini, hivyo wanapaswa kuheshimiwa na kulindwa dhidi ya manyanyaso.

Rais ameelekeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii kushirikiana na taasisi za kifedha kupanua mikopo na mafunzo kwa wafanyabiashara hao, huku TAMISEMI ikitakiwa kuhakikisha upatikanaji wa maeneo rasmi ya kufanyia biashara yenye miundombinu rafiki.

Aidha, Wizara ya Afya imeagizwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, wakati Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ukitakiwa kuongeza uhamasishaji wa uandikishaji wa wanachama.

Wizara ya Fedha imehimizwa kuimarisha huduma za kifedha zinazolengwa kwa makundi haya pamoja na kujenga uwezo wao, huku Wizara ya Nishati ikitakiwa kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Rais pia amesisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa vituo vya malezi ya watoto (daycare) ili kusaidia wazazi wanaofanya biashara hizo.

Alithibitisha dhamira ya serikali kushirikiana na sekta binafsi ili kuirasimisha sekta hii na kuifanya kuwa mchangiaji rasmi na endelevu wa uchumi.

Ameeleza kuwa mageuzi hayo ni sehemu ya ajenda pana ya serikali ya kuimarisha maisha ya sekta isiyo rasmi, kuboresha mazingira ya kazi mijini, na kuhakikisha ukuaji wa uchumi jumuishi usiomwacha mtu nyuma.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Jinsia, Wazee na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima, amesema mama na baba lishe ni nguvu kubwa katika uchumi usio rasmi, wakichangia ajira na kipato kwa wananchi wengi.

Amesema tayari juhudi zinaendelea kuboresha utambuzi wa wafanyabiashara hao, kupanua matumizi ya nishati safi ya kupikia, na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na vyama vyao nchi nzima.

Katibu wa Chama cha Wauza Chakula (UMALITA), Havijawa Omary, amesema kongamano hilo linaashiria mwanzo mpya wa ujumuishaji na heshima kwa wafanyabiashara hao.

Ameupongeza uongozi wa Rais Samia, akimtaja kama kiongozi wa mabadiliko. Aliongeza kuwa UMALITA, kilichoanzishwa mwaka 2002, kina wanachama 5,000 kwa sasa na kinatarajia kufikia 100,000 ifikapo mwaka 2030. Pia alibainisha kuwa programu ya simu (App) ya UMALITA itarahisisha upatikanaji wa mikopo na urasimishaji wa biashara, licha ya changamoto za mitaji na masharti ya mikopo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema wafanyabiashara hao wanaendelea kupata heshima kutokana na mageuzi yanayoendelea pamoja na matumizi ya nishati safi.

Alisema pia maelekezo ya matumizi ya nishati safi yameanza kutekelezwa hata mashuleni, ambapo takribani shule 300 tayari zinatumia gesi ya kupikia.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu, amesema kongamano hilo la kwanza la kitaifa limewaleta pamoja wafanyabiashara hao kujifunza na kupanga mustakabali wa sekta hiyo.

Kaulimbiu ya kongamano hilo ilikuwa kulinda amani na umoja, ikisisitiza kuwa amani ni hazina ya pamoja kwa wafanyabiashara, na ni msingi wa maendeleo ya taifa na uchumi jumuishi.

Kwa ujumla, kongamano hilo limeelezwa kuwa hatua muhimu katika kuirasimisha sekta ya wauza chakula, kukuza heshima, ujumuishaji na fursa za kiuchumi kwa maelfu ya wafanyabiashara wadogo nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Profesa Riziki Shemdoe mfano wa hundi ya Shilingi bilioni 94.158,250,400/= kwa ajili ya mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kwenye Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba lishe, lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima ya Malkia wa Nishati safi kutoka kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) Bi. Havijawa Omary katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026