Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Tanzania (Latra) imetoa onyo kwa watoa huduma wanaotoza nauli mpya kabla ya muda rasmi, ikisema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Onyo hilo linakuja baada ya kuibuka kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi, hasa wa jiji la Dar es Salaam, kwamba baadhi ya vyombo vya usafiri, hususan daladala, bajaji na bodaboda, zimepandisha nauli kwa kigezo cha tangazo la Serikali.
Akizungumza na Mwananchi Aprili 22, 2026, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Latra, Salum Pazzy amesisitiza kuwa utekelezaji rasmi wa nauli mpya utaanza Mei Mosi kama sheria inavyoelekeza.
“Kwa mujibu wa sheria, nauli mpya huanza kutumika baada ya siku 14 tangu tangazo rasmi la Serikali, hivyo muda huo bado haujakamilika na utekelezaji unaanza Mei Mosi,” amesema Pazzy.
Pazzy amesema watoa huduma wa usafirishaji wanaotoza nauli mpya kabla ya tarehe hiyo wanakiuka sheria na wanaweza kuchukuliwa hatua.
“Imesemwa wazi kuwa nauli mpya zinaanza kutumika Mei Mosi baada ya kukamilika kwa siku 14 tangu tangazo la Gazeti la Serikali. Hivyo, yeyote anayetoza kwa sasa anafanya makosa na ni kinyume cha sheria,” amesema.
Amesema mamlaka hiyo ina jukumu la kusimamia usalama na uchumi wa sekta ya usafiri, hivyo uamuzi wowote unazingatia maslahi ya wananchi na wadau wa sekta kwa ujumla.
Pia amesema hawajapokea pingamizi wala maoni yoyote kuhusu mabadiliko hayo ya nauli kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Marekebisho ya nauli mpya yamefanyika kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413, kinachoiruhusu Latra kupanga na kurekebisha viwango vya nauli na tozo mbalimbali za huduma za usafiri.
Katika tangazo la Serikali lililotolewa Aprili 17, 2026, Latra ilibainisha viwango vipya vya nauli kwa mabasi ya masafa marefu, mabasi ya mijini (daladala), teksi mtandao pamoja na pikipiki mtandao.
Kwa mujibu wa viwango hivyo, nauli ya daladala kwa safari ya hadi kilomita 10 imepanda kutoka Sh600 hadi Sh700, huku safari ya kilomita 36 hadi 40 ikifikia Sh1,500 kutoka Sh1,400 ya awali. Wanafunzi wataendelea kulipa Sh200 bila kujali umbali.
Hata hivyo, baadhi ya watoa huduma wameanza kutoza nauli hizo mpya kabla ya muda rasmi kuanza, hali inayozua malalamiko kwa wananchi.
Mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam, Irene Daniel, amesema nauli mpya zimeanza kutumika kabla ya wakati baada ya kutozwa Sh700 kwa safari ya kutoka Sinza Madukani hadi Mabibo Mwisho badala ya Sh600.
“Tuliambiwa nauli mpya zinaanza baada ya siku 14 tangu kutolewa kwa tangazo, lakini makondakta wanatoza nauli mpya kabla ya kufikia siku hiyo, hivyo tunahitaji kufahamu kama zimeanza rasmi,” amesema.
Naye, Godwin Omega, mkazi wa Msumi wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam, amesema wanatozwa Sh1,000 tofauti na kiwango halisi cha Sh700, jambo linalowapa ukakasi kuhusu tangazo lililotolewa.
“Sisi huku kabla ya tangazo tulishapandishiwa nauli, na hali hii iliyopo badala ya kuongezeka Sh100, tunaendelea na mateso ya kulipa Sh1,000 bila hatua kuchukuliwa; ni kama hakuna anayesikiliza,” amesema Omega.
