Dodoma. Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi amesema Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa watalaamu wa dawa ya usingizi tiba na ganzi salama nchini na tayari imeanza kuchukua hatua za kukabiliana nayo kwa kuanzisha stashahada itakayosaidia kuzalisha wataalamu wengi zaidi katika kada hiyo muhimu.
Naibu waziri huyo amesema kila kituo cha afya na hospitali kinatakiwa kuwa na angalau watalaamu wawili wa usingizi na ganzi, lakini hali halisi inaonesha kuwa nchini kuna watalaamu 2,950 pekee wanaohudumia hospitali zote za Serikali zipatazo 8,000, hali inayosababisha pengo kubwa la wataalamu hao.
Dk Samizi ametoa kauli hiyo leo Jumatano Aprili 22, 2026 jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu wa nne wa Chama cha Wataalamu wa Dawa za Usingizi Tiba na Ganzi Salama Tanzania (TANPA).
Amesema mchango wa wataalamu hao ni mkubwa katika sekta ya afya kwani bila wao huduma za upasuaji wa magonjwa mbalimbali pamoja na huduma za uzazi kwa akina mama wajawazito haziwezi kufanyika kwa usalama.
“Nyie ni kundi muhimu sana kwenye hospitali zetu na duniani kwa ujumla kwani bila nyie maisha ya mama na mtoto anayehitaji kufanyiwa upasuaji ili kumtoa mtoto tumboni yangekuwa hatarini, kwa sababu hakuna upasuaji unaofanyika bila nyie,” amesema Dk Samizi.
Aidha, amesema Serikali imeanzisha huduma za upasuaji wa dharura katika vituo vya afya 580 kwa ajili ya kuwasaidia akina mama wanaohitaji kujifungua kwa njia ya upasuaji, jambo linaloongeza uhitaji wa wataalamu hao ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Kwa upande wake, rais wa TANPA, Julia Mahemba amesema changamoto kubwa inayowakabili wataalamu hao ni uchache wao, hali inayowalazimu kufanya kazi kwa muda mrefu bila mapumziko.
Naibu Waziri wa wizara ya Afya Dk Florence Samizi (katikati) akiwa na viongozi wa chama cha wataalam wa dawa za usingizi tiba na ganzi salama Tanzania (TANPA) kwenye mkutano mkuu wa nne wa chama hicho uliofanyika leo Aprili 22, 2026 Jijini Dodoma. Picha na Rachel Chibwete
Ameeleza kuwa majukumu yao ni nyeti na yanahitaji umakini wa hali ya juu katika kuhakikisha mgonjwa anapata huduma sahihi wakati wa upasuaji na matibabu mengine yanayohitaji dawa za usingizi na ganzi.
“Hizi dawa zinahitaji wataalam waliobobea kwenye eneo hili, siyo kila mtu anaweza kutoa huduma hii, hivyo unakuta watalaamu hawa wanalazimika kufanya kazi hadi muda wa ziada ambao mara nyingi huwa hawalipwi tofauti na kada nyingine za afya,” amesema Mahemba.
Ameongeza kuwa kutokana na uhaba huo, baadhi ya vituo vya afya hushindwa kutoa huduma za upasuaji na kulazimika kuwapa rufaa wagonjwa kwenda katika vituo vyenye wataalamu hao, jambo linalohatarisha maisha ya wagonjwa, hasa akina mama wajawazito.
Pia ameeleza kuwa wataalamu hao wakati mwingine hupangiwa majukumu mengine nje ya taaluma yao, hali inayodhoofisha ufanisi wa kada hiyo muhimu.
Naye mtaalamu wa dawa za usingizi na ganzi salama kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dk Venance Pesa amesema hata katika hospitali kubwa kama hiyo, bado kuna upungufu mkubwa wa wataalamu, huku hospitali hiyo ikiwa na wataalamu watatu pekee katika eneo hilo.
Dk Pesa amesema taaluma ya dawa za usingizi tiba na ganzi salama ni mhimili muhimu katika huduma za afya, hususan katika upasuaji na huduma za uzazi amesema bila uwepo wa wataalamu hawa, utekelezaji wa upasuaji salama hauwezekani, hali inayoweza kuhatarisha maisha ya wagonjwa.
“Hivyo, uwekezaji katika mafunzo na ajira ya wataalamu wa kada hii ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya nchini na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika, hasa kwa akina mama na watoto wachanga,” amesema Dk Pesa.
