Matarajio ya wananchi tume ya Jaji Chande ikikabidhi ripoti yake

Dar es Salaam. Baada ya kusubiriwa kwa takriban miezi mitano, hatimaye ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 itawekwa hadharani leo.

Hatua hiyo ni baada ya tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan Novemba 20 mwaka jana kufanya uchunguzi wa matukio hayo kukamilisha kazi yake, na leo inakabidhi ripoti hiyo.

Ndani ya ripoti hiyo ndipo kutakapojulikana undani wa nini kilitokea, chanzo na kwa nini yalifanyika matukio hayo kabla na baada ya uchaguzi, kama zilivyo hadidu za rejea ilizokabidhiwa tume hiyo.

Mwenyekiti wa Tume Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande (wa pili kushoto) akiwa pamoja na Wajumbe wa Tume hiyo kabla ya kuzinduliwa Novemba 20, 2025 na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Imechukua miezi mitano kwa tume kuikamilisha kazi hiyo, baada ya muda wa awali wa miezi mitatu kumalizika kabla ya kazi kukamilika. Ikaongezewa siku 42 ambazo hazikutosha, na baadaye ikapewa nyingine 21 zinazoishia keshokutwa.

Pamoja na yote hayo, bado baadhi ya wadau wana mashaka kuhusu kilichomo ndani ya ripoti hiyo, baadhi wakisema huenda isijibu maswali ya msingi, na wengine wakisema wanaisubiri waione kujua utimamu wake.

Kwa nyakati tofauti, tume hiyo inayoongozwa na Jaji Othman Chande imekuwa ikisisitiza kuwa inafanya kazi zake kwa weledi, huku ikitaka Watanzania kuamini na kutoa ushirikiano pale ulipohitajika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga, akizungumzia hilo anasema ingawa hawakutoa ushirikiano kwa tume hiyo, matarajio yao ni kwamba iseme ukweli kuhusu kilichotokea.

“Tunataka waseme ukweli kuhusu kile kilichotokea, japo hatuna uhakika kutokana na aina ya wajumbe wanaounda tume hiyo, uhuru wao wa kufanya kazi huenda usilete matokeo yanayotarajiwa na wengi,” anasema.

Anasema taasisi hiyo haikutoa ushirikiano kwa tume hiyo kwa sababu ya muundo wa wajumbe wanaoiunda. Hata hivyo, anasema kuna watu wengi waliotoa ushirikiano, hivyo ni muhimu kwa tume hiyo kusema ukweli ili kuliponya Taifa.

Mwenyekiti wa Tume Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande.

Wakili wa kujitegemea, Warehema Kibaha, anasema matarajio yao yataweza kutathminiwa baada ya ripoti ya tume hiyo kutolewa na kuchambuliwa, ili kubaini imefikia kiwango gani katika uchunguzi wake.

“Kwa sasa ni vigumu kueleza matarajio kabla ya tume kuwasilisha ripoti yake baada ya kukusanya taarifa mbalimbali. Ripoti itakapotolewa hadharani ndipo tutakapopima kama imekidhi matarajio yetu, ingawa kwa sasa nina imani nayo,” amesema.

Kibaha anasema kutoa maoni kabla ya ripoti kutoka kutakuwa ni kuongozwa na hisia zisizo na uhalisia, ingawa katika hatua za awali walishuhudia watu wakihojiwa na taasisi mbalimbali.

“Ikitoka tutaiangalia kuona kama imefanya uchunguzi wa kina na kisha kutoa maoni yetu kama wadau. Kwa sasa tunaamini tu kuwa imekamilika, lakini hatujui yaliyomo ndani yake,” anasema.

Geroud Nombo, mkazi wa Tabata- Magengeni, jijini Dar es Salaam, anasema kuwa kwa muundo wa tume hiyo ana mashaka kama itakidhi matarajio na matamanio ya wananchi, ingawa kwa yaliyotokea amemuachia Mungu.

“Ili ionekane kweli tume imetenda kazi kwa ufanisi, iwapo kuna watu waliuawa iseme ukweli kwa kutaja idadi, kama kuna walioumia iseme pia ukweli huo, na hatimaye itoe suluhisho ili wahusika wasaidiwe,” anasema.

Anasema matukio yaliyojiri kabla na baada ya Oktoba 29, 2025 hayawezi kusahaulika kwa wengi, kwani baadhi ya watu walipoteza ndugu zao, huku wengine wakipata ulemavu wa kudumu.

“Hata ripoti itakapotolewa itakuwa vigumu kuwaridhisha wananchi wote, na wale ambao hawajaona miili ya ndugu zao itakuwaje, Mungu ndiye jaji mzuri katika jambo hili, lakini acha tuone,” anasema.

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Parfait Onanga Anyanga (kulia) akizungumza alipokutana na Mwenyekiti wa Tume Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande jijini Dar es Salaam.

Mwanahabari Neville Meena, anasema baada ya Oktoba 29, 2025 kumekuwa na maneno na tuhuma nyingi miongoni mwa watu, kila mmoja akimlaumu mwenzake.

“Nasubiri ripoti hiyo ili kuona itapendekeza nini kuhusu mustakabali wa Taifa letu, kisha tuangalie utashi wa Serikali katika kuyatekeleza yatakayowasilishwa. Kwa sababu kulikuwa na Tume ya Haki Jinai iliyopendekeza mambo mengi mazuri, lakini hatujaona utekelezaji wake,” anasema.

Anasema tume hiyo bado haijaonesha matokeo yake kwa uhalisia, huenda inahitaji muda, lakini hata mambo ya haraka bado hayaonekani.

“Mambo ya polisi bado yako vilevile. Katika suala hili la Oktoba 29, 2025, tunahitaji kuona mapendekezo na kasi ya Serikali katika kuyatekeleza, kwani yasipofanyika kutakuwa na matatizo,” anasema.

Meena anasema anatamani kuona mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi, nafasi ya vyombo vya dola na wadau wengine kama vyama vya upinzani.

“Kuna mambo mengi tunayotamani kuyasikia kupitia ripoti hiyo. Tumesikia viongozi wakubwa wakizungumzia nani alikuwa nyuma ya matukio yale, wengine wanasema yalikuwa maandamano, huku wengine wakidai yalikuwa vurugu,” anasema.

Anasema kutokana na mkanganyiko huo anatarajia kuona ni mapendekezo gani yatatolewa na tume hiyo.

“Nina maswali mengi kuhusu ripoti hiyo. Baadhi yanaweza kujibiwa au yasijibiwe, lakini bado nipo njia panda, sijui watakuja na kitu gani. Labda wataleta majibu yatakayokuwa faraja moyoni mwangu,” anasema.

Mbali na mwenyekiti wa tume hiyo, wajumbe wengine ni ni Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue.

Wengine ni Balozi Radhia Msuya na Luteni Jenerali Paul Meela ambaye ni Mwanadiplomasia na Balozi mstaafu.

Pia wamo, Said Mwema (Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu), Balozi David Kapya (Mwanadiplomasia na Balozi mstaafu) na Dk Stergomena Tax, aliyewahi kuwa Waziri wa Ulinzi, na pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Rais Samia aliunda tume hiyo kutokana na matukio ya maandamano yaliyozaa vurugu siku ya uchaguzi wa Oktoba 29, mwaka jana na kusababisha vifo na uharibifu wa mali.

Hadidu rejea ambazo tume hiyo, ambayo baada ya kutangazwa iliandamwa na baadhi ya wadau wakitilia shaka aina ya wajumbe wake waliowahi kuwa watumishi wa umma, ni kuchunguza chanzo cha matukio hayo.

Pili, kuchambua mwenendo wa matukio hayo, kutathmini madhara, kuchunguza utekelezaji wa sheria na taratibu, kubaini uwajibikaji, kukusanya maoni ya wadau, kutoa mapendekezo na kuwasilisha ripoti yenyewe ndani ya muda uliopangwa.

Baada ya kufanya kazi kwa jumla ya miezi mitano, ikiwemo kuongezewa muda mara mbili, mwenyekiti wa tume hiyo juzi alisema kuwa uchunguzi umekamilika na ripoti iko tayari kuwekwa hadharani leo.

Kwa mujibu wa Jaji Chande, tume hiyo iliwafikia watu 63,603 kwa namna mbalimbali, wakiwemo waliokwenda kutoa ushahidi wa matukio hayo na wataalamu waliotumika kushauri.

Pia ilifikia watu katika wilaya 21 na mikoa 11 na mashahidi wengi waliofikiwa ni waathirika wa matukio husika.

Alisema kati ya watu tume ilikutana nao, 553 walitoa ushahidi kwa kiapo cha maandishi, huku 1,323 wakitoa ushahidi wa kiapo cha ana kwa ana mbele ya tume.

Wengine 4,891, alisema wametoa ushahidi wao kwa njia ya madodoso kwa maana hawakuandika majina yao wala kujulikana na wananchi 1,317 walihudhuria mikutano ya hadhara ilivyofanywa katika mikoa iliyoathirika.

Jaji Chande, alisema wananchi 56,445 walituma ushahidi wao kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi na wataalamu 3,505 wa fani mbalimbali walishiriki kutoa ushauri kwa tume.